Mataifa Afrika

Katika dua zetu tusimsahahu mchizi Cape Verde.

Sambaza....

Mwaka 1980 fainali za 12 za mataifa ya Afrika zilikuwa zinafanyika nchini Nigeria na kwa mara ya kwanza katika historia ya michuano hii Watanzania tulipata nafasi ya kupeleka timu baada ya Peter Tino kutufungia bao muhimu sana pale mjini Ndola Zambia bao lililotupatia ticket ya kushiriki michuano hii baada ya mechi yetu dhidi ya Zambia kumalizika kwa sare ya bao moja kwa moja kongole kwa mwalimu Slowmir Work na msaidizi wake Joel Bendera.

Katika michuano ile nakumbuka vizuri Tanzania tulipangwa katika kundi A tukiwa na wenyeji Nigeria ambao mwisho wa Mashindano walitawazwa kuwa mabingwa baada ya kuifunga timu ya taifa ya Algeria kwa jumla ya mabao 3-0 huku timu nyingine katika kundi letu zikiwa ni Misri pamoja na Ivory Coast

Tanzania tulimaliza nafasi ya mwisho katika kundi letu tukiwa na alama 1 baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya wenyeji Nigeria kwa mabao 3-1 bao la Tanzania katika mchezo huo likifungwa na kiungo Juma Mkambi baada ya hapo tulipoteza mchezo wa pili dhidi ya Misri kwa mabao 2-1 na kisha tukatoka suluhu ya bao 1-1 dhidi ya Ivory Coast na katika mechi hizi mbili za mwisho mabao ya Tanzania yalifungwa na mshambuliaji Thuwein Waziri.

Msimamo kundi L (Livescore.com)

Baada kuikosa kwa miaka takribani 38(awamu 19) safari hii timu yetu ya taifa imekaribia mno kufuzu na kuingia katika fainali za michuano hii inayotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu katika nchi ya Misri na kinachosubiriwa ni ushindi katika mchezo wa mwisho na wa muhimu sana dhidi ya majirani zetu wa Uganda utakaopigwa jumapili hii jijini Dar es salaam.

Watanzania wengi wanaonekena kuiombea kheri na kila aina ya dua timu yetu ili iweze kushinda na kufuta msemo ulioasisiwa na mzee Mwinyi wa “Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu” lakini dua zetu hizi hazitokuwa na maana yoyote ile endapo timu ya Cape Verde itapoteza mchezo wake dhidi ya Lesotho ambao kimahesabu ndio washindani wetu wakuu katika kugombea nafasi ya pili sasa basi kwa uwingi na umoja wetu naomba tusimsahau Cape Verde katika dua na sala zetu kwasababu kufuri letu la #AFCON2019 lina funguo mbili moja iko Uganda na nyingine iko Cape Verde.

Imeandikwa na Mbuke


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.