Sambaza....

Wachezaji wawili wa Mtibwa Sugar wamejumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania “Taifa Stars” kwa ajili ya mchezo wa kufuzu mataifa ya Afrika “AFCON” dhidi ya Uganda utakaopigwa jijini Kampala , Uganda.
Stars inayofundishwa na nyota wa zamani wa Nigeria Emanuel Amunike amewajumuisha katika kikosi chake mshambuliaji Kelvin Sabato Kongwe na kiungo mshambuliaji Salum Ramadhani Kihimbwa.
Kupitia mmoja wa watendaji wa klabu ya Mtibwa Sugar Swabr Abubakar amesema ni jambo la kheri Mtibwa Sugar kutoa mchango kwa taifa.
Katika kikosi cha awali kilichotajwa Agosti 21 wachezaji hawa hawakuwemo katika wachezaji 25 waliotajwa lakini kocha mkuu wa timu ya taifa amewafuatilia wachezaji hawa katika michezo yao na kuamua kuwaita katika kikosi cha Stars.
“Ni jambo la kheri Mtibwa kutoa mchango kwa taifa na ni furaha kwetu pia kuona vipaji vyetu vinawakilisha taifa, tunajivunia na tunawatakia kila lakheri katika uwakilishi wa Taifa”Swabur Abubakar.
Wengine walioitwa badala ya wachezaji sita wa Simba walioenguliwa kikosini ni pamoja na Ally Sonso, Paul Ngalema wa Lipuli FC ya Iringa, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons ya Mbeya, David Mwantiki na kiungo Frank Domayo wa Azam FC.

Sambaza....