Sambaza....

Timu ya Yanga imerejea jijini Dar Es Salaam ikitokea mkoani Mbeya kupepetana na maafande wa Magereza, Tanzania Prisons na kufanikiwa kupata ushindi wa magoli 3-1. Baada ya mchezo huo Yanga ilipitia mkoani Rukwa na kucheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Sumbawanga United na kuichapa goli 2-0.

Kikosi kizima kimewasili kikiwa na furaha na hata mapokezi yake yalikuwa mazuri lakini kilichotokea katika mechi dhidi ya prisons kilichosababisha Mrisho Ngasa kulimwa kadi nyekundu na Kocha wa Yanga,  Mwinyi Zahera kuingia uwanjani ndilo gumzo hasa na huenda kwa siku za usoni furaha ya ushindi huo ikatibuliwa.

Kinachosubiliwa kwa sasa ni kamati ya  uendeshaji na usimamizi wa ligi ya bodi ya ligi kuu Tanzania bara (TPLB) kukaa na kufanya maamuzi yake hasa kwa upande wa adhabu na faini mbalimbali kutokana na vurugu zilizotokea katika mchezo huo.

Kwa upande wake Zahera amesema kuwa yuko tayari kusikiliza na kufuata maagizo yatakayotolewa na kamati hiyo juu yake na hata kwa wachezaji wake.

“Wakisema nilipe nitalipa, Klopp wa Uingereza kwani alifungiwa mechi?, kwani hata mechi tuliyocheza wachezaji wanne walikosekana, Tshishimbi, Gadiel, Kakolanya na Kelvin, tutaendelea na wale watakaokuwepo,”

“Tulishinda bila wao, kwahiyo  timu itaendelea kucheza ikiwa na malengo yaleyale ya kushinda kila mechi”

Kwa kiasi kikubwa kocha huyo alitupa lawama zake kwa Waamuzi na kudai kuwa huwa wanaingia mchezoni wakiwa na matokeo yao ndio maana hata wachezaji walipandwa na jazba kiasi cha kushindwa kujizuia na kufanya  walichokifanya.

“ilitakiwa tupate penati tatu, waamuzi wanapiga filimbi kwa makosa yetu kwa timu pinzani, wakati wao wanatufanyia refa hapulizi filimbi”

“Mnajua kuwa mchezo unaonekana maeneo mengi ya Afrika, na nimepokea simu za makocha wengi na hata  Rais wa shirikisho la soka nchini Congo wote wananiuliza juu ya kilichotokea, waamuzi wanashusha hadhi ya ligi”

Baada ya mchezo huo, Zahera alionekana kupandwa na jazba na hata kulia, mbele ya waandishi wa habari. Akielezea hali hiyo kocha huyo amesema kuwa amepatwa na hali hiyo kuona mashabiki wa Yanga wanaipenda timu yao lakini kuna baadhi ya watu (Waamuzi) wanaamua kuwaangusha.

Je nini kitafuata juu ya hatma ya Zahera na wachezaji wake? Endelea kutufuatilia kutakupasha haraka iwezekanavyo.

Sambaza....