Mataifa Afrika

Kinachoniuma vitabu vitamwandika Msuva na kumsahau Bocco

Sambaza....

Jana wakati natazama hafla ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania kuna kitu kilinifanya nianze kumuonea huruma John Bocco.

John Bocco huyu ambaye aliwahi kufananishwa uchezaji wake na Emmanuel Adebayor, nyota wa zamani wa Realmadrid , Arsenal, Tottenham Hotspur’s.

John Bocco huyu ambaye mpaka sasa hivi ana idadi ya magoli mia moja (100) kwenye ligi kuu ya Tanzania bara akiwa ameshavaa jezi za Azam Fc na Simba sc tu.

John Bocco huyu ambaye ni nahodha wa klabu ya Simba. Nahodha ambaye ameiongoza vizuri timu ya Simba katika michuano ya klabu bingwa barani Afrika msimu huu.

Huwezi acha kutaja mafanikio ya Simba msimu huu bila kumtaja John Bocco. Ambaye ndiye mchezaji ambaye amehusika kwenye magoli mengi kuliko mchezaji yoyote kwenye timu ya Simba kwenye michuano hii ya klabu bingwa barani Afrika.

Haongeagi sana. Mpole sana. Hana makuu, jukumu lolote ambalo hupangiwa yeye hulitimiza ipasavyo bila kujali amepangiwa jukumu gani

Hata kama ukimchezesha mchezaji wa pembeni yeye hanuni. Hasusi, ila hutabasamu na kuongeza ukimya ndani yake kisha huingia uwanjani kutimiza majukumu yake ipasavyo.

John Bocco baada ya kumalizika mchezo dhidi ya Uganda

Huyu ni maana halisi ya nahodha bora. Nahodha ambaye Simba wanajivunia sana. Nahodha ambaye amefanya kazi kubwa sana kwenye safari yetu kama Taifa ya kwenda Misri.

Nahodha ambaye mpaka sasa hivi namuonea huruma sana kwa kutotambulika kwa kizazi kijacho cha mpira wa miguu.

Ulitzama ile Hafla iliyoandaliwa na mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli ?. Hapana shaka kama uliangalia basi utagundua kitu kimoja tu, kuwa John Bocco hatotambulika sana kwa miaka ijayo.

Kwanini nasema hivo ?, kwenye ile hafla, alikuwepo mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Peter Tino.

Mchezaji pekee aliyefunga goli mwaka 1979 , goli ambalo lilitupeleka Afcon ya mwaka 1980. Huyu ndiye mfungaji pekee wa goli hili.

John Bocco vs Al-Ahly

Huyu ndiye aliyekuwa anatambulika sana na vitabu vya kumbukumbu vya mpira wa miguu. Jina lake limedumu sana kwa kiasi kikubwa.

Kila kizazi kimekuja huku kikiwa kinamtambua Peter Tino ni nani. Kwa kifupi, Peter Tino aliweka alama kubwa ambayo haiwezi kufutika mpaka sasa hivi.

Alama ambayo ilisababisha Jana Mheshimiwa Raisi. Dkt. John Pombe Magufuli ampe zawadi ya kiwanja huko Dodoma na shilingi milioni tano.

Jambo ambalo ni jema kabisa, lakini kuna swali la kujiuliza, Peter Tino aliipeleka timu yetu ya Taifa peke yake kwenye michuano ya Afcon ?

Jibu ni hapana. Hakuwa Peter Tino peke yake. Kulikuwepo wachezaji wengine bora na muhimu katika kikosi kile cha timu ya Taifa.

Kulikuwepo na wachezaji ambao walipigana sana pia kwa ajili ya Taifa. Lakini historia inamkumbuka Peter Tino peke yake.

Msuva

Huu ndiyo usaliti wa historia. Usaliti usio kuwa na tija yoyote. Usaliti unaouma. Inauma sana kipindi ambapo Historia inapoacha kuona mchango wako mkubwa.

Moja ya kitu ambacho ni kibaya katika historia ni kuwa na ubaguzi kwenye baadhi ya matukio. Ubaguzi ambao umempa Peter Tino kiwanja kule Dodoma na kuwaacha wenzake .

Ubaguzi ambao utatokea pia na kwa John Bocco. Mchezaji ambaye alitoa pasi mbili za mwisho zilizozaa magoli ambayo alifunga Simon Msuva.

Hapa ndipo vitabu vya historia vitakavyomkatili John Bocco na kumwinua kwa kiasi kikubwa Simon Msuva.

Tutamsimulia sana Simon Msuva, tutamwandika sana Simon Msuva kama shujaa yetu na kumsahahu mtu kama John Bocco.

Kikawaida risasi ndiyo huwa inaheshimika na kutambuliwa sana kuliko bunduki inayobeba risasi. Huwezi kusahau umuhumi wa bunduki.

Bocco

Kwenye ile mechi John Bocco alionesha ukomavu mkubwa sana. Licha ya yeye kutoa pasi mbili za mwisho pia alionesha nidhamu ya kucheza vizuri eneo ambalo siyo lake.

Alicheza pembeni, bila kinyongo kabisa alicheza vizuri kwa kujituma. Alitimiza majukumu yake sana bila hata kukunja ndita kwa hasira kisa tu kacheza eneo ambalo siyo lake.

Mwisho wa siku akainyanyua Tanzania na Simon Msuva akaibeba Tanzania ikawa juu. Lakini cha kusikitisha Simon Msuva atakumbukwa zaidi ya John Bocco.

Ila Mimi wakati vitabu vikiandika kuhusu Simon Msuva , wajukuuu zangu nitawasimulia kuhusu John Bocco.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x