Aziz Ki akiwaacha wachezaji wa Simba
Stori

Kivumbi Leoo Mkwakwani, Ni Simba au Yanga?

Sambaza....

Tanga kunani, leo mechi Mkwakwani, Simba na Yanga hapatoshi, Singida FG na Azam ni mafuta na ukwaju, wadigo watajiramba sana.

Ni ule utamu, sio feki ni halisi, ni yale mahaba niue, roho yangu ondoka nayo. Ni burudani ya macho , moyo ndo unafurahi, akili inapata ujasiri ama uoga lakini mwili ni mtikisiko  bila kujali ni furaha ama huzuni kiasi gani.

 

Ni zile dakika 90 za jasho na damu, kivumbi leoo! Ni historia kwao Waziri Oddo, ni pale kwa mwenye michezo yake hata ukiweka muziki yeye ndo FA ya vina na mizani.

Ndio pale pale kilipofukiwa kitovu cha Roma sio Italia wala Israel, wala sio Los Angeles na Miami, USA mafichoni. Leo mambo hadharani, hatukusemei kwa Mama, kama uzuri wa Tunito na sauti yake.

Hii ni Burudani ya soka na wahafidhina wake, haya ni mahaba na utupu wake. Hakuna rangi utaacha ona lakini leo ni ama nyekundu na nyeupe ama njano na kijani, nani atajua kuna alizeti ya Singida ama bahari na boti za Azam?

Prince Dube na Pascal Wawa

Ukiskia nipe funguo, masela wenye geto watajisachi, ni sholi gani zaidi ya kisukari cha mashuti ya Ki Aziz kwa Wananchi, ni mlimbwende yupi akaribie fenti za Chama na mikogo yake kwa Lunyasi? Diarra na ngome yake Kibu na kimbunga chake?

Ni uvumilivu wa Gamondi ama jeuri ya Robertinho? Ni mizimu ya Maradona ama malaika wa Pele?

Kama bado umelala amka, kama bado unaota hicho choo usikitumie ndotoni baadae utanishukuru, usiende na chakula chako mfukoni, Tanga wapika bwana!

Khalid Aucho mbele ya Israel Mwenda.

Mechi za derby ni zaidi ya dakika 90 za Jonesia Rukya kuziamua, nje ya uwanja kuna vihendo sio vya Mbwiga na Uzaramo wake bali wahafidhina na tamaduni zao.

Watakubali ama watakataa, hawana wa mkumdai kwani kila upande umeshiba na kilichotoka sokoni, mchawi wamtafute nani, wapishi ama muda umewawahi, majibu yote Mkwakwani.

Ni Ngao ya Jamii jijini Tanga, siku kubwa, siku ya kihistoria, siku ya Ntu na Ntuwe, wali nazi na chai ya mdarasini, maji ya kuoga na iriki, lakini Leo ni Mkwakwani na Wenyenchi ama Mkwakwani na Wananchi.? Derby ya Kariakoo Simba vs Yanga.

John Master Plan.

Sambaza....