Mabingwa Afrika

Kumbe Aussems ‘ali-bet’ aisee..!

Sambaza kwa marafiki....

Wikiendi hii Simba alisafiri mpaka Lubumbashi nchini Congo, kumvaa TP Mazembe katika mchezo wa kufuzu nusu fainali klabu bingwa Afrika.
Mchezo ambao, mbinu ndizo zilizoamua mshindi wa mtanange huo. Mbinu pekee za kocha Pamphile Mihayo Kazembe na Patrick Aussems zilikuwa ndio ufunguo halisi wa ushindi.

Ulikuwa ni mchezo wa kuvutia kwa macho kwa dakika 45 za awali pekee, baada ya hapo hakukuwa na mvuto tena kwani TP Mazembe tayari walikwisha tawala mchezo wote.
Simba walianza vizuri katika dakika 15 za awali, wakichagizwa na goli la Emmanuel Okwi dakika ya pili tu ya mchezo. Aisee!… mpira ungekuwa unaishia dakika ya 20 huenda tungekuwa tunaitaja Simba katika hatua ya nusu fainali.
Kama ilivyo ada, kocha Patrick Aussems alijaribu kuingia na nidhamu ya ulinzi katika game hiyo.
Alianza na mfumo wa 4-1-4-1 yaani kiungo wa chini kabisa alikuwa James Kotei, lakini mfumo huo ulibadilika haraka sana dakika ya pili tu ya mchezo kwenda 4-3-2-1 yaani Kotei aliungana na Jonas Mkude na Mzamiru Yassin, wakiwaacha Okwi na Haruna Niyonzima wakicheza pembeni wakitokea katikati.

Aussems, kocha wa Simba

Mfumo huu ulionekana kuleta uhai kwa kikosi cha Simba hasa katika eneo la kati kwa Dakika 20 za kipindi cha Kwanza kabla ya Beki wa kati, Kabaso Chongo kuisawazishia TP Mazembe.
Katika kipindi chote cha kwanza, Simba walicheza kwa nidhamu ya hali ya juu, wakijaribu kupunguza idadi ya makosa hasa katika eneo lao la hatari. Lakini hata hivyo haikuwa na tija sana kwani makosa yaliendelea kufanyika hasa kwa beki wa kulia, Zana Coulibaly.

Simba walitegemea mashambulizi ya kushitukiza hasa wakimtegemea Okwi, kutokana na kasi yake na uwezo wa kumiliki mpira na kupiga mashuti, hata hivyo naye alikosa msaada kwakuwa watu waliokuwa wanamzunguuka hawakuwa na kasi kama yake.

Mfano, John Raphael Bocco hakuonekana kabisa uwanjani, na Niyonzima naye alipiga back-pass nyingi, kwa mantiki hiyo hawa wachezaji wawili hawakuwa na msaada katika mfumo wa kushambulia kwa kushtukiza.

Kwa ujumla katika kipindi chote cha kwanza, Simba walipaki basi, walikuwa wakichezea eneo lao na hata mipira iliyoenda mbele haikuwa na macho. Kuna wakati Bocco alijikuta yuko peke yake akizunguukwa na wachezaji watatu, na asijue la kufanya.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, TP Mazembe tayari walikuwa wameshaliteka eneo la kati, viungo kama Nathani Sinkala na Mike Mika walipata nafasi ya kwenda kumsalimia Aishi Manula golini, na kuhakikisha Simba hawaleti madhara katika eneo lao.

Simba walimaliza kipindi cha kwanza, wakishambulia kwa kulitawala eneo la kati, walijaza viungo watano katika eneo hilo walioungana na mabeki wa pembeni na kuunda jumla ya wachezaji 7 katika eneo hilo.

Haikuwa kazi rahisi kwa Simba kufungwa goli mbili katika kipindi cha kwanza isipokuwa ni makosa kwa beki Zana Coulibaly na viungo wa chini kama Jonas Mkude na James Kotei.
Kipindi cha pili, Aussems alibadili kabisa aina ya uchezaji na game plan nzima. Alimtoa kiungo mkabaji na mshambuliaji, Mzamiru Yassin na kumuingiza Straika, Meddie Kagere, hapo ndipo balaa lilipoanzia.

Hili ndilo kosa la awali kabisa kulifanya Kocha Aussems, alimtoa Mdhamiru ambaye tayari alikuwa na kiwango kizuri katika eneo la kulia na la kati, alijaribu kushuka chini kusaidia ulinzi hasa upande wa Coulibaly uliokuwa umekwisha mezwa.

Hadi Mzamiru anatoka tayari alikwishapiga pasi sahihi 6 sawa na asilimia 66.7, alipiga mipira Mirefu miwili, alifanikiwa kupokonya mipira miwili ya hamsini kwa hamsini, na kufanya ‘clearance’ moja.
Katika kipindi chote cha kwanza, Mdhamiru ndiye aliye ng’aa ukilinganisha na viungo kama Kotei na Mkude. Mdhamiru ni mzuri akiwa hana mpira, yaani kukaba na kutumia nguvu anapokaribiana na adui ndio maana alifanikiwa ku-win mipira yote ya ‘one against one’ aliyokutana nayo.

Kumtoa Mzamiru maana yake, Aussems alitaka kushambulia, yaani kucheza 4-4-2, akimuacha kotei na mkude eneo la chini, huku Okwi na Niyonzima wakitanua eneo la kulia na la kushoto.
Aina hii ya uchezaji, ni tofauti na ile aliyoanza nayo, Aussems aliamua kufunguka, kwa Kiswahili tunasema “ liwalo na liwe”

Dakika ya 53, Aussems alifanya ‘technical Switching’, alimtoa beki Juuko Murshid na kumuingiza kiungo mshambuliaji Clatus Chama,
Na hapo ndipo alilazimika kumshusha James Kotei kuwa beki wa kati akiungana na Erasto nyoni katika eneo la kati la ulinzi.

Mabadiliko haya, ndiyo yaliyokuwa mabaya zaidi kwani athari yake ilikuwa kubwa. Mkude alishuka chini, akiwa kama kiungo wa ulinzi, peke yake na kuunda mfumo wa 4-1-3-2.

Mabadiliko haya yaliwafanya viungo wa Mazembe, Mika, Sinkala, Meschak Eliya, Tresor Mputu na Rainford Kalaba kupumua, na kushambulia kwa kasi, kwa kuwa, katikati hakukuwa na changamoto tena.

Hadi Juuko anatoka alikuwa tayari amekwisha fanya kazi kubwa hasa kumsaidia Zana Coulibaly eneo la kulia lilikokuwa linavuja kila wakati. Juuko alifanya ‘Clearance 9’, akicheza ‘tackle’ 1 iliyofanikiwa, alifanikiwa kupokonya mipira miwili kati ya minne ya hamsini kwa hamsini na kufanya faulo mara moja pekee..

Alipiga mpira mrefu mmoja sahihi, alipiga pasi 7 na zote zilikuwa sahihi kwa asilimia 100, katika kipindi chote cha kwanza, Juuko ndiye aliyefanya kazi kubwa zaidi katika safu ya ulinzi.

‘Sub’ ya Juuko ilikuwa na madhara katika sehemu tatu muhimu za Simba,kwanza ni eneo la ulinzi. Kama wote tunavyomjua, Juuko ni beki mtukutu, hutumia nguvu wakati wa kukaba na hana masihara katika uokoaji.

Kutoka kwake kulilifanya eneo la kulia kuendelea kuwa bovu kiasi cha mashambulizi yote kupitia huko. Kutolewa kwa Juuko kulipunguza msaada kwa Zana Coulibaly.

Pili Juuko aliliathiri eneo la kati, yaani Kotei na Mkude wakicheza pamoja eneo la chini hufanya vizuri zaidi kuliko mkude akicheza peke yake. Baada ya kutolewa kwa Juuko, Mkude alibaki peke yake matokeo yake ni kufungwa goli walizofungwa.

Ukisikia Kubeti, ni kumuamini Mkude aliyekwisha potea uwanjani, na kumtoa Mdhamiru mwenye japo uhai, kubeti ni kumtoa Juuko na kumuingiza kiungo mshambuliaji, kubeti ni kumuacha Mkude eneo la chini peke yake hali yakuwa amekwisha potea, kubeti ni kuamua kushambulia bila kuimarisha eneo la ulinzi, kubeti ni kumuamini Coulibaly licha ya kuwa na madhaifu mengi.

Ukitaka kujua kuwa, Aussems alikata tamaa ni dakika ya 71 alipoamua kumtoa Emmanuel Okwi na kumuingiza Rashid Juma hii ilikuwa ni kabla ya goli la nne la Jackson Muleka kwa pasi ya Tresor Mputu.
Kiufupi, Aussems alikosa nidhamu katika kipindi cha pili, aliamua kujilipua ugenini. Ni sawa na kumfukuza mwizi hali ya kuwa umeacha mlango wazo, lazima uibiwe tu..

Mabadiliko hayo ndiyo yaliyofanya Simba kuzidiwa kila eneo na kila idara, TP Mazembe walimiliki mpira kwa asilimia 58 ukilinganisha na 42 za Simba, walipiga mashuti 34 kwa 5 kati ya hato yaliyolenga lango yalikuwa 14, 15 yakitoka nje na matano wakizuliwa.
TP walipata kona 9, Simba wakipata 2 pekee, Simba walifanya madhambi mara nyingi na walizawadiwa kadi 3 za njano .
Kutokana na ubora wa kikosi cha Kazembe kupitia mfumo wa 4-2-3-1, viungo wa Mazembe walituliza presha ya timu na kupandisha vuguvugu la mashambulizi kupitia pembeni na katikati. TP walitengeneza nafasi 6 za wazi, na wakishindwa kuzitumia nafasi 3 za wazi, kwani waligongesha mwamba mara 3, na kupiga mashuti 24 ndani ya Box na 10 nje ya Box.

Kupiga mashuti mengi ndani ya box maana yake ni kuvuja kwa kiungo wa chini na safu ya ulinzi, na hii ni baada ya kutolewa kwa Juuko na Mdhamiru.
Takwimu zinamfanya TP Mazembe astahili kupata matokeo tena ya zaidi ya goli 6, wachezaji wa Simba walipoteza mipira mingi katika maeneo hatari, walifanya hivyo mara 14 ukilinganisha na mara 6 kwa TP Mazembe.

Shukrani za dhati zimfikie golikipa wa Simba, Aishi Salumu Manula, yeye alifanya kazi kubwa ya kuokoa mipira ambayo ilikuwa ni magoli, alifanya ‘save’ muhimu 10, 7 zikiwa ni ndani ya boksi, alipiga pasi 16 sawa na asilimia 53.3, alipiga mpira mirefu 29 kati ya hiyo 15 iliwafikia wachezaji wake.

Ukiachana na Manula, wengine aliyefanya vizuri zaidi ni Haruna Niyonzima, Erasto Nyoni, Juuko Murshid, Mzamiru Yassin na Emmanuel Okwi.
Mabeki wa Pembeni, Coulibali na Mohammedi Hussein walishindwa kuendana na kasi ya mchezo, Coulibaly alikuwa mzito wakati wa kurudi kulinda, hakuwa katika kiwango kizuri hata kidogo.

Tshabalala alifanya baadhi ya makosa, wakati timu ilipokuwa kwenye presha kubwa yeye alibaki sehemu yenye presha ndogo, mfano, mashambulizi yakiwa upande wa Coulibaly yeye alibaki juu sana bila kumkaba mchezaji yeyote. Kiwango chake naye kilikuwa hafifu ukilinganisha na mechi ya kwanza jijini Dar es salaam.

Mkude ndiye kiungo ambaye alipotea zaidi japo aliendelea kuaminiwa na mwalimu Aussems kwa dakika zote 90.

Haya! Mashindano haya yamemalizika, Simba anarudi nyumbani kuwaza jinsi gani atarejea tena kimataifa, muda wa kula viporo vyake. Hatua waliyofikia sio mbaya kwakuwa wenyewe wanadai wamepitiliza malengo yao.

Lakini hata hivyo mashindano haya yamekuwa Somo kubwa kwa vilabu vingi nchini na hata nje ya nchi. Kwanza ni matumizi mazuri ya uwanja wa nyumbani, pili ni kujitathmini kama aina ya wachezaji waliopo wanafaa kwa ushindani kimataifa na pia nchi imetangazika vyema.. ni muda wa nchi kuwekeza kwenye michezo.

Baada ya kufuzu, TP Mazembe watakutana na Esperance da Tunis ya Tunisia, Wydad Casablanca ya Morocco watakutana na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.