Sambaza....

Kuna kitu kimoja ambacho nakiamini sana na kinaweza kuwa na usahihi kwa asilimia kubwa sana kuwa Real Madrid na Barcelona ndiyo Hijja ya mpira ambapo kila mchezaji hutamani kwenda kufanya ibada ya mpira( Ku-Hijji).

Hakuna mchezaji asiyetamani kuchezea hizi timu kwa sababu ya historia kubwa zilizobebwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabeau na Nou Camp.

Unaweza kuikataa Real Madrid lakini moyo wako ukawepo Barcelona, au unaweza kuikataa Barcelona lakini moyo wako ukawepo Realmadrid.

Huu ndiyo uhalisia halisi wa mpira wa dunia, ndiyo maana ndiyo vilabu ambavyo wachezaji nyota wamepita sana.

Ndiyo vilabu ambavyo wachezaji wake wengi wamebeba tunzo nyingi za Ballon D’or na ile ya mchezaji bora wa dunia ya FIFA.

Ndiyo vilabu ambavyo vimebeba vikombe vingi kuzidi vilabu vyote ulaya, ni mara chache sana kwa msimu kumalizika bila kabati la Barcelona au Real Madrid kubeba kikombe.

Ndiyo vilabu ambavyo kwa miaka kumi iliyopita vimetoa wachezaji ambao wameshinda Ballon D’or.

Kwa kifupi Ballon D’or ilikuwa inavuka mji tu, leo itakuwepo katika jiji la Madrid kesho itaenda katika jimbo la Catelunya.

Ngassa (kulia)

Halikuwa jambo la kushangaza kwa sababu vilabu hivi vilikuwa vimebeba wachezaji wawili bora wa kizazi hiki na inawezekana ni bora kwa wakati wote yani Cristiano Ronaldo na Lionel Messi.

Siyo jambo la kushangaza sana kwa sababu vilabu hivi ndiyo sehemu kwa wachezaji wengi kuonesha kuwa wamecheza mpira.

Wengi historia yao ya kucheza mpira huwa bado haijakamilika kama hawajakanyaga nyasi za Santiago Bernabeau au Nou Camp, kwa kifupi mchezaji mpira hawezi kuitwa kacheza mpira bila ngozi yake kugusa jezi za hizi timu mbili (Real Madrid na Barcelona).

Ndiyo maana Thierry Henry aliacha mapenzi yote aliyokuwa anapewa Arsenal na kuamua kwenda Ku-Hijji katika mji wa Barcelona.

Alienda kukamilisha ibada yake ya mpira katika timu ya Barcelona, hapo ndipo ukamilifu wake katika kucheza mpira ulipoonekana.

Furaha yake ilikamilika hapo, ndoto yake ikatimia. Ni ndoto ya watu wengi sana!, lakini ni wachache sana huitimiza.

Ni wengi wanatamani kucheza katika vilabu hivi viwili lakini ni wachache sana wanaoweza kutimiza ndoto zao.

Ni kama ilivyo hapa nchini kwetu, vijana wengi wanatamani kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Wanatamani kufika sehemu ambayo wengi walifanikiwa kufika, na wengine wanatamani kufika angalau sehemu ambayo Mbwana Samatta yupo tu.

Matamanio na ukamilisho wa matamanio huwa ni vitu viwili tofauti, unaweza ukawa unatamani kitu ila ikawa ngumu kukifikia.

Nidhamu ndiyo nguzo muhimu ambayo inaweza kukufikisha sehemu ambayo unaitamani.

Nidhamu ya mazoezi, kuheshimu kila anayekuzunguka na nidhamu ya kuwa na washauri wazuri wanaokuzunguka.

Ndiyo maana kuna hadithi nyingi za wachezaji wengi ambao walikuwa na vipaji vikubwa lakini hawakufanikiwa kufika mbali pamoja na kuwa na vipaji vikubwa.

Kizazi chetu cha sasa kitamkumbuka sana Mrisho Khalfan Ngassa kama mchezaji aliyekuwa na kipaji kikubwa lakini hakufanikiwa kufika mbali.

Tuliona kitu kikubwa sana kwenye miguu ya Mrisho Khalfan Ngassa, miguu yake ilikuwa na uwezo mkubwa sana wa kufika mbali.

Alikuwa mchezaji wa kisasa, ni aina ya wachezaji wanaocheza pembeni lakini wenye uwezo wa kufunga na kutoa pasi za mwisho.

Ni mchezaji wa kisasa, hakuna timu ambayo isingetamani kuwa naye ndiyo maana hata hapa kwetu alifanikiwa kuvichezea vilabu vyetu vikubwa (Simba , Yanga na Azam).

Ndiyo maana alifanikiwa kwenda kufanya majaribio katika ligi kuu ya England kwenye klabu ya Westham United.

Alikuwa na kipaji haswaaa!, lakini mwisho wa siku hadithi yake ilikuwa haina ukamilifu bora kwa sababu hakufanikiwa kucheza katika ligi bora.

Aliishia kuzunguka zunguka, Tanzania, Marekani, England, Sudan na Afrika Kusikini lakini hakuwa na maisha mazuri sana yenye kustahili kipaji chake, sehemu pekee ambayo alionekana amefanikiwa sana ni Yanga.

Nahisi ni kwa sababu hapa ndipo moyo wake ulipoanzia kuumbwa, alizaliwa kwenye mitaa hii ya Jangwani, hata udongo uliotumika kuumba mwili wake ilikuwa udongo wa Jangwani.

Ndiyo maana kila akivaa jezi ya Yanga huwa na moyo sana wa kupigana kuliko anavyovaa jezi ya timu nyingine yoyote.

Inawezekana Mrisho Khalfan Ngassa alizaliwa kwa ajili ya kuichezea Yanga pekee.

Jana kwenye mechi dhidi ya Stand United alionesha hilo, alikuwa anacheza kwa moyo sana na kujituma.

Kuna wakati unaweza ukadhani Mrisho Khalfan Ngassa karudi kwenye nyakati zake tena.

Kuna wakati unaweza ukadhania kuwa Mrisho Khalfan Ngassa anaiwaza Yanga kama RealMadrid na Barcelona yake kuwa ndiyo sehemu yake sahihi ya kufanya ibada ya Ku-Hijji mpira.

Sambaza....