Balama Mapinduzi akipiga shuli lilizoo goli baada ya kumpokonya mpira Mzamiru Yassin
Blog

Mapinduzi Balama: Tangawizi kwenye juice ya miwa Jangwani

Sambaza....

Tupilia mbali kazi ya Tshishimbi na Feisal pale dimba la chini Yanga, Sahau udambwi na pasi zenye macho za Niyonzima, hapa namuongelea jamaa anayevaa jezi ya Yanga iliyochapishwa namba saba (7) Mgongoni.

Ndio, anaitwa Mapinduzi Balama, kiungo mwenye umbo dogo asiyeshikika wala kutabirika, miguu yake na akili vinawasiliana kwa haraka sana jambo linalompa uwezo wa kuuchezea mpira anavyotaka.
Mikimbio, pasi za uongo uongo(Chanya) ,mashuti na uwezo wa kufunga ndio silaha zake pale jangwani, Msimbazi wanamkumbuka vizuri.

Ukiwa ni msimu wake wa kwanza pale jangwani ambapo alisajiliwa akitokea Alliance ya Mwanza, Mapinduzi ameweza kujihakikishia nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza chini ya makocha wote waliokuepo na waliopo.

Balama Mapinduzi akishangilia goli alilowafunga Simba.                                                                                  Akiwa na umri wa miaka 26, Anaweza kucheza kama kiungo mchezeshaji, Winga zote na hata mshambuliaji wa pili. Ukisikia kampa kampa tena za Nugaz basi jua jeuri hio anaipata kwa kijana huyu akichagizwa na mafundi wengine pale Dimbani.

Akiwa kwenye eneo la kiungo ananesa na kupotea kama upepo, viungo wanaokutana naye shughuli yake wanaijua, HASHIKIKI.
Kuna jama yangu anamfananisha Balama na Mrisho Ngassa Anko enzi za ubora wake, Hapana kabisa nakataa. Uncle ni uncle na Balama ni Balama ambae anazidi kuingia mioyoni mwa Wanajangwani kwa utaalam wa mguu wake huku kimo chake kimizidi kumsaidia kutokana na aina ya mpira anayocheza.

Balama Mapinduzi.

Hii ni Tangawizi inayochagiza utamu wa juisi ya miwa pale jangwani aisee, umbo dogo akili nyingi, kama akiendelea hivi na Yanga ikafanya sajili za maana na zenye tija msimu ujao basi “WAPE SALAAAAM” utakua msemo mashuhuri na maarufu saana VPL msimu ujao.

Hakika mtoto kutoka  “Rock City” ataendelea kutupa kile ambacho tumekikosa kwa muda mrefu Watanzania kwa kupata  “Driving midfielder” na  mtundu mtundu kama yeye.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.