Tulimwamini sana, tulimpa kila kitu. Mioyo yetu ilimpa mahaba yote. Kibaya zaidi tulimwamini kuliko mtu yeyote kwa sababu tu 3-5-2. Nadhani huu mfumo ulitutia upofu sana, tulimwona kocha wa kisasa kwa sababu tu mfumo huo ndiyo ulikuwa umeshika kasi duniani.
Ndiyo mfumo ambayo ulimpa taji Antonio Conte. Kila tulipokuwa tunaitazama Chelsea ya Antonio Conte tukawa tunaifananisha na Simba. Tukaamini Masoud Djuma ametuletea uzungu katika ligi yetu ya kiswahili. Tulizoea uswahili sana kwenye ligi yetu.
Tulizoea mifumo ya kawaida sana kwenye ligi yetu. Ni kocha yupi ambaye alidhubutu kupanga mfumo tofauti na mfumo wa 4-4-2?
Hakuna ambaye aliyedhubutu, utaanzaje kutambulisha mfumo mpya tena mbele ya wachezaji ambayo hawana misingi mizuri ya soka?
Wachezaji ambao makocha wengi wanaamini hawafundishiki mbinu mpya za kisasa za kimpira?, wachezaji ambao wanacheza mpira kwa kukariri?.
Ilikuwa ngumu sana, lakini Masoud Djuma aliweza. Tena siyo kuweza tu alifanikiwa kupata matokeo chanya kupitia mfumo huo huo mpya kabisa.
Aliifanya timu icheze mpira mzuri kupitia mfumo huo huo. Na mwisho wa siku akawafanya mashabiki wa Simba wachizike sana na aina yake ya mpira.
Aliwafanya mashabiki wa Simba wamwamini sana kuzidi mtu yeyote pale msimbazi. Aliwafanya mashabiki wampende sana.
Alikuwa na wafuasi wake katika klabu ya Simba. Wafuasi ambao walikuwa wamekunywa damu inayoitwa Masoud Djuma.
Ilikuwa ni ngumu kuwaambia chochote kibaya na wakakuelewa kuhusu Masoud Djuma. Walikuwa wamelewa haswaa na huba la Masoud Djuma.
Walikuwa tayari aondoke mtu yeyote ila yeye tu abaki, walikuwa tayari kabisa kushuhudia Masoud Djuma abaki kuwa kocha milele.
Hawakuwa tayari kumuona akiondoka. Ndiyo Pierre Lenchantre aliondoka na kumuacha yeye akiwa anaitumikia Simba.
Hata Patrick Assumes alipokuja, wengi hawakuwa tayari kumuona akikaa kwenye kiti cha kocha mkuu. Hawakutaka kabisa hata dakika moja.
Matamanio yao makubwa yalikuwa kumuona Masoud Djuma kuwa kama kocha mkuu. Huyu ndiye ambaye alikuwa amejijengea ufalme ndani ya mioyo ya mashabiki wa Simba.
Wakati mashabiki wakiamini Masoud Djuma ndiye kila kitu lakini viongozi wa Simba waliamini wanaweza kuishi bila Masoud Djuma.
Waliamini Simba inaweza kufanya vizuri bila ya Masoud Djuma. Hiki ndicho walichokiamini na ndicho ambacho walikifanya.
Tulisubiri maisha ya Simba bila ya Masoud Djuma. Wengi tuliamini yatakuwa maisha magumu sana katika kikosi cha Simba.
Lakini ilikuwa tofauti kabisa, Leo hii Simba inafanya vyema zaidi kuliko hata kipindi cha Masoud Djuma na inawezekana yeye ndiye aliyechelewesha kuifikisha hapa Simba.