Kuna kitu ambacho huwa na kitazama sana, na kila nikikitazama naona hiki kitu kina nafasi kubwa sana ya kuifanya mechi ya Simba na Yanga iwe tukio na isiishie kuwa mechi.
Hisia huwakamata mashabiki wa pande zote mbili (Simba na Yanga) kwa kifupi vilabu hivi viwili vimeigawa Tanzania pande mbili.
Upande wa kwanza ni wa Msimbazi na upande wa pili ni wa Jangwani, kila mtu hujivunia kuishi kwenye upande ambao anaishi.
Hakuna anayekubali kushindwa kuanzia mdomoni mpaka uwanjani, ndiyo maana upinzani wao huanzia kabla hata ligi haijaanza.
Dirisha la usajili likifunguliwa tu, upinzani wao ndipo unapoanza!, utaona viongozi ambavyo wanavyohangaika kusajili kila jina ambalo litawafurahisha mashabiki wao.
Mashabiki nao utawaona kwenye vijiwe vya kahawa wakiwa na vipande vya magazeti wakiwa wanatambiana kwa vichwa vya habari vilivyopambwa na maneno matamu.
Huyu atajivunia gazeti lililoandika usajili wa beki mpya ambaye anakaba watu wanne kwa wakati mmoja, na mwingine atajisifia na kichwa cha habari cha gazeti lililoandika kuhusu mshanbuliaji anayefunga magoli mpaka kero.
Hii yote ni kuonesha ni jinsi gani ambavyo kila mtu anavyopenda klabu yake. Wana mapenzi mazito sana! , mapenzi ambayo muda mwingine huwafanya wawe vipofu ndiyo maana viongozi hutumia mwanya huo kusajili kwa ajili ya kuwafurahisha wao tu!.
Hata baada ya usajili kukamilika, tambo huendelea na tena hupamba moto tofauti na awali. Kila mmoja huamini ana uwezo mkubwa kuzidi mwenzake.
Huyu atajivunia Meddie Kagere wake , na huyu atakuja na Makambo wake, Leo Emmanuel Okwi akifunga kesho kelele zake zitazimwa na pasi nyingi za mwisho za Ibrahim Ajib.
Tena ataitwa fundi ambaye hajawahi kutokea duniani, fundi ambaye alishiriki kuijenga Roma katika ustadi wa hali ya juu ili mradi tu kuwepo na kukerana.
Na ni ngumu sana kuacha kuzipa nafasi timu hizi mbili kuchukua ubingwa hata kama wana hali gani mbaya ya uchumi.
Lazima uwape nafasi ya kubeba ubingwa tu! , huu ni utamaduni wao kubadilishana kombe, leo atabeba Simba kesho atampa mwenzake Yanga.
Na wakati mwingine mechi kati yao huonekana ni mechi ambayo inaweza kutoa dalili za nani anaweza kuwa bingwa, ni mechi inayotoa maamuzi kwa asilimia kadhaa.
Ndiyo maana inapofika kila kiungo cha miili yetu hujitayalisha kwa ajili ya hii mechi. Macho yetu yatakuwa na shauku ya kumshuhudia mmoja kati yao akipoteza mechi hii hili tu afanyiwe kero mtaani.
Midomo yenu hujiandaa kwa tambo kabla ya mechi na baada ya mechi. Kabla ya mechi kila mmoja hujiamini sana, huamini yeye ndiye bora kuzidi mwenzake, kuongea kwa kujiamini huwa ni kawaida sana kwao.
Kujiamini kwao husababisha wao kuitumia miguu yao kusogea mpaka sehemu ya kutazama mpira ili kushuhudia hukumu ya mechi hii.
Siku hii kuna vitu vingi sana husimama Tanzania. Maduka hufungwa kwa muda, barabrani gari hupambwa na bendera za Simba na Yanga.
Kwenye vijiwe mbalimbali bendera hupepea bila uoga, tambo huwa zinakuwa kila kona. Watu wako tayari kuweka nyumba , pesa mpaka wake zao tu kwa kujiamini kuwa wanauwezo mkubwa wa kushinda hiyo mechi.
Kwa kifupi ni mechi ambayo hubeba hisia za watu wengi sana hapa nchini. Hisia ambazo hatujaamua kuzitumia kama biashara.
Hii mechi hatujaamua kuifanya mechi ya kibiashara, ni bidhaa ambayo hatujaiuza na hatufikirii kuanza kuiuza zaidi ya kuikodisha kwa bei ya kawaida sana.
Hakuna biashara nzuri duniani kama biashara ya kuuza hisia, kitu hiki UEFA , FIFA na baadhi ya maeneo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Michuano ya kombe la dunia iliyofanyika Russia, FIFA walifanikiwa kuuza hisia kwa mashabiki wengi wa soka. Walifanya michuano hiyo iwe tukio, iwe sherehe ambayo kila mmoja anatakiwa kuisherehekea.
Sherehe ambayo kama utaikosa unaweza kulia huku ukilaumu kwanini hujaenda kuisherehekea? , ndiyo maana kuna mashabiki walikopa Mali ili waende Russia tu kusherehekea sikukuu ya kombe la dunia.
Hawakujali hasara ambayo wataipata kwao wao kushirki sherehe ya kombe la dunia ni kitu cha muhimu sana kama ambavyo ilivyo kwa watu wa ulaya na usiku wao wa ulaya .
Ni usiku maalumu kwao, usiku wa kusherehekea mpira wa miguu na ni usiku ambao una msisimko mkubwa sana. Msisimko wenye hisia kubwa sana.
Hisia ambazo zipo hata kwenye mechi kati ya Simba na Yanga, mashabiki huwa na nguvu na hisia kubwa kuanzia wiki mbili kabla ya mechi.
Hii inaonesha wako tayari kusherehekea sikukuu hii lakini hawajatengenezewa mazingira bora ya wao kusherehekea sikukuu hii. Wazazi wao hawataki kununua mchele kwa ajili ya kuwapikia pilau, hawataki kuwanunulia nguo mpya watoto wao ndiyo maana watoto wao hupenda vya majirani.
Tutabaki kusifia vya wenzetu wakati vya kwetu vina nafasi kubwa sana vya kuvifanya kuwa vikubwa. Hatutaki kuwekeza kwenye kuitengeneza mechi hii kuwa nembo inayojiuza yenyewe. Matangazo ni machache sana.
Hatujaamua kuitangaza mechi hii kama tukio maalumu, tunaitangaza kama sherehe ya harusi tu mwisho wa siku itahudhuliwa na wenye kadi tu ambao ni ndugu na jamaa wa maharusi, hatujataka kuifanya iwe sikukuu ya Tanzania nzima.