Sambaza....

Fundi!, ndilo neno ambalo nililisikia kutoka kwa jirani yangu. Niligeuka kumwangalia, kwa bahati nzuri au mbaya tukakutanisha naye macho.

Hapo ndipo ukawa mwanzo wa yeye kuniambia, aliongea kwa hisia kali sana ambazo zilionesha dhahiri maneno yake yalikuwa yanatoka moyoni.

Mazungumzo yake yalikuwa yametawaliwa na neno Mohammed Ibrahim, na haya yote yalitokea kipindi ambacho tunaangalia mechi ya kirafiki kati ya Simba na AFC Leopards.

Hakuwa mbali na mawazo yangu, alichokuwa anakiwaza kilikuwa hakijatofautiana sana na kile ambacho kilikuwa kinapita kichwani mwangu wakati mpira unaendelea.

Kichwa changu kilikuwa kinapitisha kila aina ya swali, swali kubwa ambalo lilikuwa linapita kichwani mwangu, ni kwanini Mohammed Ibrahim hana nafasi?

Mchezaji mwenye kipaji kikubwa lakini hana nafasi !?. Unakumbuka kipindi cha Joseph Omong? , namaanisha msimu juzi?.

Msimu ambao Simba walikuwa hawana hali nzuri ya kiuchumi ukilinganisha na kipindi hiki, ndicho kipindi ambacho Simba walikuwa hawana uwezo mkubwa wa kusajili wachezaji wenye majina makubwa.

Unajua kipi walichokifanya ?, ni kitu kidogo tu kilichofanyika nacho ni kuwatumia wachezaji vijana wenye vipaji.

Waliamini katika vipaji vikubwa na kupuuzia kuamini katika majina makubwa na hii ilisababishwa kwa kiasi kikubwa na hali ya uchumi waliyokuwa wanaipitia.

Hali yao kiuchumi haikuwa nzuri sana kulinganisha na kipindi hiki, hawakuwa na uwezo mkubwa wa kutunisha misuli yao minene ya pesa katika usajili.

Hivo ikawa nafasi kwa vijana wenye vipaji kuanza kutumika katika kikosi cha Simba, ndipo hapo macho yangu yalipata kuona muunganiko wa watu watatu.

Muunganiko ambao ni bora! , muunganiko ambao ulileta ushindani mkubwa kwenye ligi licha ya Simba kuwa na hali ya kawaida kiuchumi.

Muunganiko ambao ulisababisha Simba kupoteza nafasi ya ubingwa dhidi ya Yanga kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.

Kwa kifupi Mzamiru Yasin, Shiza Kichuya na Mohammed Ibrahim walikuwa nguzo kubwa ya timu ya Simba.

Waliweza kuipa uhai Simba, ilipigana! Kwa nguvu zote na ilicheza soka la kuvutia kwa sababu moja tu hawa vijana waliaminiwa.

Benchi la ufundi liliwaamini, viongozi waliwaamini na wenyewe wakalipa fadhila ya kuaminiwa na kufanya kazi yao kubwa uwanjani.

Ndiyo ukawa mwanzo wa Shiza Kichuya kuibuka mfungaji bora wa Simba msimu ule huku Mohammed Ibrahim akifunga na kutengeneza nafasi muhimu za magoli.

Kwa kifupi walikuwa mchezaji muhimu ndani ya kikosi cha Joseph Omong.

Na Joseph Omong alimwamini sana kupitia kipaji chake ndiyo maana alimpa nafasi ya kukionesha kipaji chake.

Maisha yanaenda mbele, hatuwezi kuishi kwa kurudi nyuma hata siku moja. Ili maisha yaende lazima siku ziende mbele.

Historia huja kutukumbusha lakini haiji kukamilisha leo. Leo itakamilishwa na leo na siyo jana iliyopita.

Jana yenye furaha na huzuni. Jana na juzi ya Mohammed Ibrahim ilikuwa yenye furaha kwa sababu alikuwa anapata nafasi kubwa ndani ya kikosi cha Simba kwa sababu ya kuaminiwa!.

Leo hii hadithi imekuwa tofauti sana, kuna nafasi finyu kwake ndani ya kikosi cha Simba.

Hii inasababishwa na nini?, ushindani uliopo ndani ya kikosi? Utovu wa nidhamu wa Mohammed Ibrahim?.

Yote yanaweza majibu sahihi lakini ukweli unabaki pale pale kuwa kwa sasa Mohammed Ibrahim amekosa imani kuanzia kwenye benchi la ufundi, mashabiki na viongozi wa Simba.

Hakuna anayemwamini tena kama ambavyo alikuwa anaaminiwa kipindi cha nyuma.

Hakuna anayeamini kwa kiasi kikubwa ndani ya miguu yake ingawa wapo ambao bado wanamuita fundi.

Kuna watu ambao wamepewa nafasi ndani ya kikosi cha Simba, wakaitumia na kushika imani ya watu wengi.

Wanaaminika sana!, wanahusudiwa sana!, kwa kifupi wanapendwa sana kwa sababu walifanya kitu ambacho kiliwapendeza watu baada ya kupewa nafasi.

Hiki ndicho ambacho kinampa wakati mgumu Mohammed Ibrahim. Siyo kwamba hana kipaji kikubwa, siyo kwamba hajitumi.

Ila nafasi anayocheza ni ngumu kuaminiwa kwa sasa kulingana na washindani wake.

Kitu pekee ambacho Mohammed Ibrahim anakosa kwa sasa ni kuaminiwa ndani ya kikosi cha Simba.

Hawezi kupata nafasi kubwa ya kucheza kwa sababu haaminiwi ndani ya kikosi cha Simba na kibaya zaidi nafasi ambayo anacheza kuna watu ambao wameweka mizizi yao.

Sawa nakubaliana kabisa kuwa sifa ya mwanajeshi ni kupigana, na mchezaji ni kama mwanajeshi anatakiwa kupigania namba yake ndani ya kikosi.

Tuangalie umri wa Mohammed Ibrahim, ni umri ambao anatakiwa kupata muda mwingi wa kucheza au ni.muda ambao atautumia kwa ajili ya kupigania namba?

Kuna wakati mwingine ni bora uende sehemu ambayo utapata malisho ambayo yataimarisha afya yako.

Hiki ni kipindi ambacho Mohammed Ibrahim anatakiwa kupata sehemu ambayo itamwamini na kumpa nafasi ambayo itaimarisha kiwango chake.

Bado naamini Mohammed Ibrahim ni fundi bora aliyekosa kuaminika ndani ya kikosi cha Simba.

Sambaza....