Blog

Msimu ujao SIMBA wasimtegemee WAWA

Sambaza....

Mechi ya mwisho ya ligi kuu  Simba walikuwa wanacheza na Coastal Union katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga ambapo timu zote zilitoka suluhu , katika mchezo huo tukio kubwa lilikuwa la beki wa Simba , Pascal Wawa kupewa kadi nyekundu.

Pascal Wawa alipewa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya mshambuliaji wa Coastal Union , Ayoub Lyanga. Imekuwa ni mara nyingi sana kwa Pascal Wawa kufanya madhambi dhidi ya wachezaji ambao wanamzidi mbio kwenye mchezo. Hata jana kasi ya Ayoub Lyanga ilikuwa inampa wakati mgumu Pascal Wawa.

Tuachane na tukio la yeye kupewa kadi nyekundu , tuachane na tukio la yeye kuzidiwa kazi na Ayoub Lyanga kitu ambacho kilimlazimisha yeye kufanya madhambi yaliyosababisha kupewa kadi nyekundu katika mchezo wa jana , tujiulize hili swali kwa pamoja , Pascal Wawa kazeeka ? Kabla ya kupata hilo jibu tujiulize haya maswali tena , upi ubora na udhaifu wa Pascal Wawa ? Tuanzie hapa kwenye ubora na udhaifu wa Pascal Wawa.

UBORA WA PASCAL WAWA.

1: UTULIVU AKIWA NA MPIRA.

Moja ya silaha kubwa ya Pascal Wawa ni pale anapomiliki mpira mguuni , huwa na utulivu mkubwa , utulivu ambao husababisha asipokonywe mpira. Ukiachana na utulivu wa Pascal Wawa akiwa na mpira pia Pascal Wawa anaweza kutembea na mpira mpaka eneo la katikati ya uwanja.

Faida kubwa ya beki wa kati kuwa na utulivu katika umiliki wa mpira na kutembea nao kwenda mbele ni kutengeneza uwazi kwa wapinzani. Unatengenezaje uwazi ? Wachezaji wa timu pinzani hulazimisha kusogea kumkaba, wanaposogea kumkaba huacha uwazi eneo lao , uwazi ambao mara nyingi huwa na faida kwa Simba kupitia Pascal Wawa.

Wawa

2: KUPIGA PASI FUPI NA NDEFU

Moja ya ubora wa Pascal Wawa ni kwenye upigaji wa pasi , mara nyingi huwa Simba huwa inaanzisha mashambulizi kwa kuanzia nyuma. Unayokuwa unaanzisha mashambulizi kuanzia nyuma unatakiwa uwe na mabeki wa kati ambao wana uwezo wa kupiga pasi. Pascal Wawa ni mzuri kwenye hili la kupiga pasi fupi na ndefu.

3: ONE AGAINST ONE

Hii inaweza kusimama kama faida kwa Pascal Wawa , pia inaweza kusimama kama hasara kwa Pascal Wawa. Tuanze kuitazama kama faida. Pascal Wawa amekuwa mzuri anapokutana na mshambuliaji karibu (one against one), lakini kama mshambuliaji hana kasi sana hapa Pascal Wawa ana uwezo wa kushindana naye nguvu na kupokonyana mpira.

Pascal Wawa

UDHAIFU WA PASCAL WAWA.

1: MIPIRA YA JUU

Umbo la Pascal Wawa halimpi nafasi kubwa kwake yeye kuwa mzuri kwenye mipira ya juu kwa sababu ya ufupi wake. Hivo kuna wakati Simba inawagharimu kwenye suala la ulinzi na Simba hawanufaiki na Pascal Wawa wanapokuwa wanashambulia kwa kutumia mipira ya juu mfano kushambulia kupitia kona na mipira ya adhabu ndogo.

2: ONE AGAINST ONE

Kama nilivyosema huko juu, hoja ya One against One inaweza ikatumika kama ubora au udhaifu wa Pascal Wawa. Pascal Wawa anapokutana na mshambuliaji ambaye hana kasi kubwa ndani ya uwanja ana uwezo mkubwa wa kupambana naye lakini tatizo huja pale anapokutana na mchezaji ambaye ana kasi kubwa uwanjani huwa ni ngumu kwa Pascal Wawa kupambana naye kama ambavyo ilivyotokea jana dhidi ya Ayoub Lyanga ambaye alimlazimisha kufanya makosa.

3: DHAIFU KWENYE BOX LA MPINZANI .

Kama nilivyosema Pascal Wawa hana uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya juu kutokana na umbo lake , kitu ambacho kinakuwa hakina msaada kwa kiasi kikubwa kwenye kujilinda na kushambulia. Ni mara chache sana kwake yeye kuwa hatari kwenye box la mpinzani kama mabeki wengine wa kati wanavyokuwaga hatari.

4: FREE-KICK

Ukitazama Erasto Nyoni, Virgil Van Djik ni baadhi ya mabeki wa kati ambao wana uwezo mkubwa wa kucheza mipira ya adhabu ndogo (yani mipira iliyokufa). Hii imekuwa tofauti kabisa kwa Pascal Wawa ambaye amekuwa siyo mzuri sana kwenye uchezaji wa mipira ya adhabu ndogo.

MWISHO

Simba wamepata nafasi tena ya kutuwakilisha kwenye michuano ya kimataifa, michuano ambayo ina washambuliaji wenye kasi uwanjani , ili kukabiliana na washambuliaji hawa unatakiwa uwe na mabeki wenye kasi pia.

Sambaza....