Sambaza....

Mwamuzi wa soka Victor Marah amefariki wakati akiamua mpambano wa ligi ya Jamii nchini Sierra Leone kati ya Kroo Bay  FC na Falcon 12 FC siku ya Jumanne mjini Freetown.

Victor mwenye umri wa miaka 27 alidondoka uwanjani wakati mchezo huo ukiwa umebakia dakika chache kabla ya kumalizika na alipatiwa huduma ya kwanza kabla ya kukimbizwa hospitali lakini alitangazwa kufariki wakiwa njiani kuelekea huko.

Bado sababu hasa ya kifo cha mwamuzi huyo hazijawekwa wazi, lakini kimekuja majuma machache toka arejee kutoka nchini Misri alipohudhuria kozi ya waamuzi wa shirikisho la soka barani Afrika ‘CAF’.

Mkufunzi wa waamuzi nchini Sierra Leone Sanusi Rachid ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza ‘BBC’ kuwa kifo cha mwamuzi huyo kijana ni pigo kwa soka la nchini humo na Afrika kwa Ujumla.

“Alikuwa na kipaji cha pekee, na tulimuhitaji kwa siku za usoni, bado siamini kama hili kweli limetokea, alikuwa ni miongoni mwa vijana ambao nchini ingenufaika nao kwa siku za usoni, na ndio maana alichaguliwa kuhudhuria mafunzo ya CAF mwezi uliopita,” Sanusi amesema.

Tayari familia ya mwamuzi huyo imethibitisha kuwa Marah atazikwa siku ya Ijumaa, nah ii ni mara ya kwanza kwa historia ya soka nchini Sierra Leone kwa mwamuzi kufariki akiwa katika majukumu yake uwanjani.

Sambaza....