Sambaza....

Utamwambia kipi kibaya Zlatan Ibrahimovich kuhusu Jose Mourinho akakuelewa vizuri?, hapana shaka hakuna.

Kwake yeye anaamini huyu ndiye kocha bora kuwahi kuja katika maisha yake. Ndiye kocha ambaye alikuja kumuonesha namna ya kuwa na njaa.

Njaa ya mafanikio!, njaa ambayo ni muhimu katika maisha ya mwanadamu yeyote. Jose Mourinho alimfundisha kutoridhika mapema.

Alimfundisha kutokata tamaa mapema. Alimfundisha kupigana mpaka hatua yake ya mwisho ya kuwepo duniani.

Kwa Jose Mourinho hakuna mchezaji ambaye alikuwa anauwezo wa kuikatia tamaa mechi ya aina yoyote, kila mchezaji alikuwa anatamani kushinda.

Wachezaji wengi walifanywa na Jose Mourinho kuona kila mechi iwe fainali katika mtazamo wao. Ndiyo maana walikuwa wanapigana sana.

Walikuwa waipigania timu yao, walimpigania kocha wao na mwisho kabisa wakawa wanapigania mafanikio yao binafsi.

Mafanikio ambayo yangebaki kama alama kubwa katika maisha yao. Alama ambayo ingeishi kwa muda mrefu kwa vizazi vingi.

MANCHESTER, ENGLAND – OCTOBER 02: Jose Mourinho, Ex-Manager of Manchester United gestures prior to the Group H match of the UEFA Champions League between Manchester United and Valencia at Old Trafford on October 2, 2018 in Manchester, United Kingdom. (Photo by Michael Regan/Getty Images)

Leo hii vizazi vinaikumbuka Fc Porto ya Jose Mourinho. Timu ambayo ilikuwa haitazamwi kwa kiasi kikubwa.

Lakini ndiyo timu ambayo ilikuja kushinda vizuri sana ligi ya mabingwa barani ulaya. Ligi ambayo ni ngumu, ligi ambayo imebeba vigogo imara.

Lilikuwa jambo la ajabu sana na la kustajabisha sana kwa timu kama FC Porto tena ikiwa na kocha ambaye alikuwa hana mafanikio makubwa lakini ikabeba kombe.

Tena kibaya zaidi ilibeba mbele ya Barcelona, Realmadrid, Bayern Munich na vilabu vingine. Hili liliwezekana kabisa mbele ya Jose Mourinho.

Ndiyo maana aliitwa “The Special One”, mtu maalumu. Na kweli alikuwa mtu maalumu, tena sana. Umaalumu ambao ulikuwa wa peke yake tu.

Upekee ambao ulikuwa na mtazamo wake wa kipekee. Yeye aliwaza kombe tu. Yeye aliamini kocha atakumbukwa kwa kutwaa makombe.

Aliamini wachezaji watakumbukwa kwa kutwaa makombe tu. Ndiyo maana alitumia muda mwingi sana kuwafundisha sanaa ya namna ya kushinda makombe.

Hapa ndipo alipofanikiwa, aliweka sumu kali sana. Sumu ambayo iliwafanya wachezaji wawe na uwezo wa kupigana sana.

Aliishi na wachezaji kirafiki sana kipindi ambacho alikuwa anaonekana ana uhitaji wa kuwafanya kitu bora kitu ambacho kilitengeneza urahisi kwa wachezaji kumpigania.

Kitu hiki nakiona kwa Mwinyi Zahera, yuko katika kipindi kigumu sana. Kipindi ambacho timu haipati morali kubwa wa kifedha kutoka kwa viongozi.

Hali ya uchumi wa Yanga siyo nzuri kabisa, haitii nguvu kwa mchezaji kupigana. Lakini Mwinyi Zahera ameligundua hilo.

Na anajua kabisa namna ambavyo anaweza kucheza na akili ya wachezaji ili wafanye vizuri. Hapa ndipo Jose Mourinho naye huwa anaonekana bora.

Anajua kucheza na akili ya wachezaji kuwafanya wapigane kwa kuwaaminisha kwenye kupigana ndiko kuna mafanikio makubwa.

Haijalishi ni aina gani ya gumu ambao mchezaji wa Yanga anakutana nao lakini hachoki kupigana kwa ajili yake , kwa ajili ya kocha na kwa ajili ya timu.

Leo hii Yanga inaongoza ligi kuu ya Tanzania bara kwa sababu tu ya Mwinyi Zahera. Huyu ameweka sumu kubwa kwa wachezaji wake.

Huyu ndiye amewafanya wachezaji wafikirie jinsi ya kupigana kwa ajili ya mafanikio bila kujalisha ugumu wowote ule ambao wanapitia.

Ndiyo maana Leo hii kila mchezaji ambaye anaingia kwenye kikosi cha Yanga anafikiria namna ya kuipa timu ubingwa.

Haijalishi alikaa benchi kwa muda mrefu lakini yeye hufikiria hicho tu. Ni jinsi gani ataipa Yanga ushindi. Ndilo swali kubwa ambao huzunguka kwenye vichwa vya wachezaji wa Yanga.

Na yote haya yameanzia kwa Mwinyi Zahera kwa kuwaaminisha faida ya wao kupata ushindi. Kwenye ushindi ndiko kuna njia ya mafanikio makubwa.

Huwezi kupata mafanikio bila kupata ushindi. Ushindi huwafanya watu wakufuatilie na wanapokufuatilia ndipo hapo unaweza ukapata njia ya kutokea.

Mwinyi Zahera amekuwa kama baba, kaka na rafiki kwa wachezaji wake. Kitu ambacho wakati mwingine wachezaji huona ni deni la kumlipa kila wanapoingia uwanjani.

Akili zao huwaza namna ya kumlipa deni kocha wao. Mwisho wa siku timu inafanya vizuri tena ikiwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.

Sambaza....