Ligi Kuu

MZFA Watoa ufafanuzi, kutokuwapo kwa Ambulance Kirumba.

Sambaza....

Chama cha soka mkoa wa Mwanza (MZFA) kimetolea ufafanuzi kuhusiana na kutokuwapo kwa gari la wagonjwa (Ambulance) kwenye uwanja wa CCM Kirumba wakati Mbao FC wakicheza na Coastal Union ya Tanga kwenye michuano ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara.

Katibu Msaidizi wa MZFA Khalid Bitebo amesema ni kweli gari la wagonjwa halikuwepo na ndio maana ikawalazimu kutumia gari aina ya Harrier kumbeba mchezaji wa Coastal Union Adeyuni Saleh aliyendoka wakati mchezo huo ukiendelea.

Bitebo amesema sababu iliyopelekea hali hiyo ni wasimamizi wa Ligi kwa maana ya Bodi ya ligi walituma kwa kuchelewa mabadiliko ya ratiba ya mchezo huo ambao awali ulipaswa kufanyika saa 10:00 Jioni lakini ukarudishwa kuanza saa nane mchana jambo ambalo hata walipojaribu kuwaomba tena watu wa Ambulance, tayari gari hilo lilikuwa kwenye shughuli nyingine.

“Tulipata taarifa kwa kuchelewa kuwa mchezo ambao ulipaswa kufanyika saa 10 uchezwe saa nane mchana, nah ii ilitokana na warusha matangazo kwa maana Azam kuomba muda huo ili kupata nafasi ya kurusha matangazo ya mchezo wa Lipuli FC na Azam FC,”

“Sasa tayari tulishapanga kuwa watu wa huduma ya kwanza waje saa kumi, na hata tulipobadilishiwa ratiba tuliwataarifu tena lakini tayari walikuwa kwenye shughuli nyingine, jambo hili kwetu limekuja kama funzo, hatukuwa na namna nyingine ya kumsaidia mchezaji Yule zaidi ya kumuwahisha kwa gari lilikuwapo uwanjani,” Bitebo amesema.

Mchezaji Adeyum alidondoka uwanjani katika dakika ya 45 baada ya kupoteza fahamu lakini hata hivyo wakati wakiwa katika harakati za kumkimbiza hospitalini, Adeyum alirejea na fahamu na kuruhusiwa kukaa Jukwaani kwa dakika zote za mchezo zilizobaki.

Katika mchezo huo Mbao FC ilipoteza kwa bao 1-0, shukrani kwa Raizin Hafidhi aliyefunga katika dakika ya 59 ya mchezo huo.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.