Blog

Namungo inapanda ligi kwa ajili ya mechi za Simba na Yanga?

Sambaza....

Kuna ligi kuu mbili hapa Tanzania. Kuna ile ambayo inatambulika na FIFA (ligi kuu Tanzania bara) na ile ambayo inatambulika na watu wa mpira hapa nchini.

Hii ni ligi kuu ya Simba na Yanga. Nadhani hii ndiyo ligi kubwa na yenye mvuto kuliko ile ligi kuu ya Tanzania Bara. Kinachoipa nguvu hii ligi ya Tanzania bara ni FIFA.

FIFA inaitambua hii ligi na ndiyo ligi inayotoa mwakilishi kwenye miçhuano ya CAF. Hiki ndicho kinachoipa nguvu hii ligi , tofauti na hapo haina cha ziada.

Mvuto wa ligi uko hapa (kwenye ligi kuu ya Simba na Yanga). Hapa ndipo mvuto wa ligi upo. Kuna msisimko mkubwa sana kwenye hii ligi.

Mashabiki huwa wanasisimka sana kwenye hii ligi. Na huwa wanajaa viwanjani kwenye hii ligi kuu ya Simba na Yanga.

Siku ambayo moja ya hizi timu inapocheza viwanja hujaa sana, mabanda umiza hutapika sana. Kwa kifupi huzifuatilia sana hizi timu kuliko ligi kuu.

Narudia tena , mashabiki wengi hufuatilia hii ligi ya Simba na Yanga kuliko ligi kuu ya Tanzania bara. Hata siku ambayo zitakutana zenyewe kwa zenyewe nchi husimama.

Dakika tisini hutosha kusimamisha nchi, nchi husisimka sana, na nchi hugawanyika Mara mbili.

Yani vipande viwili hugawanyika, upande wa jangwani wenye rangi za njano na kijani, pamoja na upande wa msimbazi wenye rangi nyekundu na nyeupe.

Kwa kifupi asilimia kubwa ya mboni za wapenda mpira hutamani kuzitia machoni hizi timu. Ndiyo maana timu nyingi za daraja la kwanza hupanda kwa ajili ya mechi za Simba na Yanga.

Utakuta vyama vya soka katika mikoa tofauti ikiwekeza nguvu kubwa kwa ajili ya kupandisha timu ligi kuu. Kwa macho ya nyama unaweza kuona wanapandisha timu kwa ajili ya ligi kuu Tanzania bara.

Lakini siyo kweli, viongozi wengi huwekeza nguvu kwa ajili ya kupandisha timu ili icheze ligi ya Simba na Yanga pekee.

Yani sababu za moyoni kabisa kama ukiwauliza kwanini mnataka kupanda ligi kuu watakuambia jibu moja, tunapanda ligi kuu kwa ajili ya mechi za Simba na Yanga.

Yani Simba na Yanga zipate nafasi za kuja katika mkoa husika kwa ajili ya mechi. Hii ndiyo sababu kuu zingine ni uongo mtamu tu ambao utakufanya uwasikilize.

Uongo ambao umefanywa na timu nyingi sana. Ndiyo maana kuna wakati timu inapopanda ligi kuu , ile nguvu ya kuiunga mkono hupungua kwa kiasi kikubwa sana.

Huwezi kuona tena wale viongozi wa kisiasa, wafanyabiashara , viongozi wa chama cha soka cha mkoa husika wakihamasisha uungwaji mkono wa timu husika.

Timu nyingi hutelekezwa , muda huu huwa hazikumbukwi kabisa kwa sababu hitaji lao lilikuwa kupandisha timu kwa ajili ya ligi kuu ya Simba na Yanga.

Yani Simba na Yanga waje tu mkoa husika, watu wajae uwanjani. Na kuna wakati viongozi hao hao ambayo hushiriki kwa nguvu kubwa kupandisha timu, ndiyo hao hao hushiriki kuzihujumu timu zao zinapokutana na Simba na Yanga.

Hakuna timu ambayo inapanda kwa malengo makubwa, malengo ambayo yanamaono makubwa ndani yake. Ndiyo maana nyingi huwa zinakufa.

Timu nyingi zina mechi nne tu ( mbili za ugenini kati ya Simba na Yanga, na mbili za mwisho ni za uwanja wa nyumbani kati ya Simba na Yanga).

Yani hata ndiyo malengo ya timu nyingi kupanda ligi kuu. Zinapanda kwa ajili ya kucheza hizi mechi nne tu. Ukiwauliza viongozi wengi wa timu zinazopanda ligi kuu kuhusu mipango mikakati ya timu yao kwa miaka mitano ijayo.

Unaweza ukaishia kutukana. Timu haina mpango mkakati hata wa miaka mitano, hakuna. Yani timu inaenda enda tu bila malengo yoyote.

Kipi wanakiwaza kama timu?, ipi falsafa ya timu husika?, itachukua muda gani hiyo falsafa kuwekezwa kwenye timu husika?

Wanamalengo ya muda gani ili waje kuchukua ligi kuu ya Tanzania bara?, wengi malengo yao ni kushinda hizo mechi nne nilizokutajia hapo juu.

Wana mpango gani kuhakikisha timu inakuwa na uhakika angalau wa kufika hatua ya makundi ya michuano ya CAF? , yani baada ya miaka mingapi watakuwa wamefika huko ?

Watafikaje huko ?, watawekeza kwa wachezaji vijana tangu wakiwa na umri mdogo, wavumbue vipaji vyao, wavilee na kuvitumia kwa ajili ya timu kubwa kwa kuwekeza falsafa yao ndani ya hao vijana?

Au watatumia mtindo wa kusajili wachezaji nyota wakiwa wakubwa wameshakomaa tayari?, vipi watawezeja kupata hizo pesa?

Wanampango gani wakupata wadhamini, kuwatunza na kuwavutia wengine waje kuwekeza ndani ya timu yao?

Vipi kuhusu vijana wanaowazalisha watakuwa na mahusiano na timu gani kubwa kwa ajili ya kuwapekeleka hao vijana kwa ajili ya kufanya majaribio kwenye hizo timu ?

Kuna mengi ya kujifunza lakini mwisho wa siku hakuna anayetamani kujifunza, tunatamani kujifunza namna ya kupanda ligi kuu ya Simba na Yanga.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x