Blog

Ngassa alishafeli! Hizi ni sinema za soka letu

Sambaza kwa marafiki....

Makala hii imewekwa tena leo lakini ni ya mwaka 2014. Ni moja ya kumbukizi tukielekea sheherekea miaka 8 ya tovuti.-


Nionavyo mimi matatizo yetu tuliyonayo hatuyatambui hivyo basi inatuwia vigumu kuyapatia ufumbuzi, na katika hili namaanisha matatizo yoote tuliyonayo hatujui yanaanzia wapi, iwe utamaduni, siasa, michezo na hata haya ya kiuchumi.

Tarehe 22 October 2008, Stephen Worgu alikubali mkataba wa miaka 4 na Al-Merreikh ambao uliwazidi Al-Ahly ya Misri, Deal hilo linakadiriwa kufikia $2.5 million, na $1 million Mshahara wa Mwaka , na $1.5 million walilipwa Enyimba. Worgu alisema pesa hiyo kubwa ilimvutia kuachana na Klabu yake ya Enyimba na kuikataa Al Ahly, juu ya uchaguzi wake huo kutoka Enyimba na kwenda Al Merreikh kwasababu za kimpira alifeli lakini kwasababu za Kimaslahi alifaulukwasababu asingepata pesa nyingine kama ile kutoka kwenye timu za Ukanda wa Afrika.

Tarehe 17 Disemba 2012 Mrisho Ngassa alikataa kujiunga na Timu ya Al Merreikh ya Sudan sababu zilikuwa ni kwamba, Muajiri wake wa kipindi hicho Klabu ya Azam ilimlazimisha yeye kwenda huko Sudan bila ridhaa yake, pia akasema kuwa Sudan kuna makato makubwa, na baadae akasema “Ana ofa Nono Zaidi” akaendelea na kuitaja timu ya Maritzburg FC ya Afrika Kusini kuwa wana nia ya kumsajili, na hata kama atasajiliwa na timu nyingine yoyote ile watakuwa tayari kuvunja Mkataba, UONGO ULIOTUKuUKA, nilijiuliza kama Maritzburg wana nia na Ngassa kwanini wasingemsajili kipindi anapatikana kwa urahisi kuliko kusubiri aingie Mkataba na Timu nyingine halafu wao waje wauvunje?, muda ukapita Akabaki kwenye Timu ya Mkopo Simba SC wa mwaka mmoja na Mwaka uliofuata akarudi Yanga SC ikielezwa ndio timu kipenzi chakebaada ya mkataba wake na Azam kufikia Ukomo.

Wakati anachezea Simba SC kwa Mkopo inatajwa kuwa alishaingia mkataba wa Awali wa kuichezea Klabu hiyo kwa muda wa miaka miwili, lakini baada ya ule mkopo kuisha akakubaliana na Yanga hivyo TFF wakaviita Vilabu vyote viwili na kuamuliwa Yanga Iilipe Simba Pesa walizompa Ngassa, ndicho kilichotokea na Ngassa kutamka hadharani kuwa amerudi kwenye timu aipendayo, HIZI NI SINEMA ZA SOKA LETU NA WACHEZAJI WETU HAZIKUANZA LEO, JANA WALA JUZI.

Mwaka 2009 Februari Mrisho Khalfan Ngassa alipata nafasi ya majaribio na kufuvu kucheza katika timu ya LOv-Ham ya Nchini Norway lakini inasemekana Klabu yake kipindi hicho iligoma ada ya uhamisho ya dola elfu hamsini, ikisema thamani ya Mchezaji huyo ni Dola laki mbili za kimarekani, Lovham wakashindwa na kuamua kuendelea na Maisha yao, Kilichonisikitisha katika suala hili lililotokea miaka mitano iliyopita Mchezaji husika hakuonyesha nia thabiti ya kutaka kwenda kucheza Ulaya kama anavyolazimisha sasa kuelekea kucheza Free State Stars FC ya Afrika Kusini.

Ikaja hadithi ya Westham United FC ya England, wachunguzi wa mambo tulijua pale hakukuwa na Dili, ikaja Seattle Sounders na baadae ikaja Al Merreikh, Mrisho Ngassa naweza kusema kuwa ndio Mchezaji mwenye bahati kuliko wote katika kizazi hiki kwa aina ya dili alizopata, na kuzikataa au kutoonesha nia ya kuzipigania dili hizo.

Mwaka 2014 Juni timu ya Taifa ikiwa inajiandaa kuelekea Botswana kwa mechi ya kujipima Nguvu Mrisho Ngassa alipata dili la kwenda kufanyiwa vipimo vya Afya na Klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini kwa nia ya kumsajili kwa msimu wa 2014/15 wa Premier Soccer League (PSL), lakini usajili huu umeshindikana kutokea hadi sasa kutokana na kudaiwa kwa Klabu yake Kipenzi ya Yanga SC kugomea Ada ya Dola elfu themanini inayotaka kutolewa na Klabu hiyo ya PSL, ikidaiwa sio thamani ya mchezaji huyo ambayo wao wanadai thamani halisi ya Mrisho Ngassa ni dola laki moja na hamsini za kimarekani.

Wapo wanaoipinga Yanga SC kwa kusema wanataka kumuharibia Maisha Ngassa na kumkomoa tu kwa kuwa waliliipa kiasi cha milioni 48 Simba SC kama fidia ya kuvunja mkataba wa makubaliano ya awali ya Ngassa na Simba SC.nikajiuliza katika Dola elfu themanini kuna milioni 48 ngapi?Kwanini wamkomoe?, na wapo wanaoisapoti Klabu kwa kusema wapo sahihi kwa kuwa Gharama za wachezaji ni kubwa Duniani kote hivyo kama Free State FC wanamtaka Ngassa lazima waongeze Dau, nimetafakari sana juu ya hili lakini nilichokiona ni kwamba Ngassa alishafeli zamani sana na hana wa kumlaumu zaidi ya yeye mwenyewe.

Mchezaji mwenye wakala anaetambuliwa na FIFA kufanya madudu kama aliyoyafanya Ngassa katika siku za mwanzoni mwa maisha yake ya Soka ni jambo la kusikitisha, mengi yalisemwa na wakala wake, mengi yamesemwa na watu lakini yeye alihadaika na zile pesa zisizokatwa kodi kutoka kwa matajiri wenye asili ya Kiasia, ndio pesa hizo hizo zilizomrudisha Haruna Moshi Boban Dar es Salaam kutoka nchini Sweden, ndio pesa hizo hizo zilizomfanya Ngassa akatae kusaini mkataba Mnono wa Al Merreikh.

Leo hii nashangaa kwa mchezaji Yule ambae alishafika hadi Norway na kupewa kila kitu na kuambiwa njia sahihi za mpira zilipo na kurudi nchini kisa tu klabu yake kugomea ada ya uhamisho na yeye kutochukua hatua yoyote, leo hii analazimisha Uhamisho atoke timu yake pendwa aende Afrika Kusini? Ujasiri huu kautoa wapi? Majibu yakanijia haraka kichwani Ngassa hana uwezo wa kulazimisha uhamisho na wala hajaguswa na jambo lolote lile na akisema nitamuona Muongo namba moja.

Baada ya Tafakuri yangu yakinifu nilipata majibu kuwa Ugonjwa ni ule ule wa wachezaji wetu baada ya kupoteza mvuto katika uwanja wa Taifa huwa wanatokea kutaka kufanya uhamisho wa kwenda nje ya nchi au kutafuta timu huko kuliko jambo lolote. Ngassa kwa sasa sio Mfalme tena kwenye Klabu yake ya Yanga wala Timu ya Taifa, Yanga kuna mfalme mpya ambae ni Marcio Maximo, lakini kabla ya Maximo kuja Ufalme ulikuwa Emmanuel Okwi kila kitu alitajwa Okwi hata gharama yake ya Usajili Inajielezea yenyewe, Timu ya Taifa kuna Mfalme mpya Mbwana Samatta na Mchezaji kipenzi cha wengi kwa sasa ni Thomas Ulimwengu, hivyo inampasa kuondoka Nchini walau akajipoteze na Macho ya watu, walau atapata kujumuishwa na Kocha wa Timu ya taifa katika kikosi cha kwanza.

Nilipomaliza kuangalia mechi ya awali kati ya Taifa Stars dhidi ya Zimbabwe pale Dimba la Taifa mpya mchezaji ambae hakunivutia alikuwa ni Mrisho Ngassa, sikushangaa alipopumzishwa. Wakati Thomas Ulimwengu akipambana kupeleka mipira mbele na kulitia misukosuko lango la Zimbabwe na kuleta hatari, Ngassa hakutaka kukimbia na muda wote alikuwa anaenda kuwapora mipira wenzake miguuni na kushindwa kuendana na kasi ya mchezo mzima, sikushangaa mechi ya Marudiano mjini Harare Kocha Mart Nooij kuamua kuanza na Simon Msuva.

Ngassa huyu wa leo sio Yule wa mwaka 2009 wala 2010, muda umemuhukumu sana Ngassa, naweza kusema ni wakati muafaka sasa kwake kupigania nafasi hii aliyoipata sasa kwenda kucheza Afrika Kusini itimie, naamini kama nafasi hii ataipoteza itahitajika nguvu za ziada kutoka kwake kurudi tena kwenye ile kasi yake ya zamani katika kipindi hiki cha utawala mpya wa Wafalme Wapya.

Sioni ni jinsi gani kwa sasa Ngassa atawapindua vijana hawa Simon Msuva, Ramadhan Singano na Haruna Chanongo na Thomas Ulimwengu ambae anaweza kucheza kama mshambuliaji akitokea pembeni na kati, Kasi ya Jonas Mkude, Saidi Ndemla, Hassan Dilunga Umakini wa Mbwana Samatta na fomu ya John Bocco kwa Ngassa kupata namba katika Kikosi cha kwanza cha Stars akitokea Yanga SC ni ndoto ambayo itatimia kwa kuzidisha bidii ya mazoezi na pengine aina ya mifumo tu kumuokoa, kwake ni heri tu apate nafasi ya kwenda kukipiga Free State Stars FC kwa sasa, naamini ataenda kukabiliana na changamoto mpya kabla haijawa “too late” hii itamuongezea nafasi ya kurudishwa kwenye timu kufuatia habari zilizovuja hivi karibuni kuwa ametemwa kwenye kikosi kinachojiandaa na Mechi ya awali ya hatua ya pili ya Mtoano dhidi ya Msumbiji mnamo tarehe 20 mwezi huu wa julai.

Na Hichi ndicho tusichokijua juu ya Mrisho Ngassa wa sasa na kubaki kujidanganya tu!, Nawasilisha Changamoto natoa nafasi ya kukosolewa pia, na Mchezaji mwenyewe na Hadhira pia.

Dizo Moja

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.