Ligi Kuu

Nilichojifunza kwenye kipigo cha Simba dhidi ya Kagera Sugar.

Sambaza....

Leo hii Simba ilikuwa inacheza mechi ambayo wangekabidhiwa kombe lao , furaha kubwa kwao ilikuwa ni kukabidhiwa kombe wakiwa hawajafungwa hata mechi moja kwenye ligi kuu lakini Juma Kaseja akaharibu matamanio yao. Kipi nimejifunza kwenye mechi hii?

1: Hapana shaka Watanzania tunapenda matukio ya muda mfupi na siyo matukio ya muda mrefu, kwetu sisi hatujafikia sehemu ambayo tunaweza kujivunia kuwa mpira ni sehemu ambayo tunaweza tukaitumia kama sehemu ya starehe. Mwitikio wetu wa kuja uwanjani unatokana na tukio fulani. Tukio la Raisi John Pombe Magufuli kuwepo uwanjani ni moja ya tukio kubwa ambalo liliwasukuma mashabiki wa Simba kuhudhuliwa kwa wingi uwanjani kuliko sababu ya timu kuwa bingwa.

2: Pamoja na kwamba mashabiki wengi hawajafanya mpira wa miguu kuwa ni sehemu ya starehe ila kukiwepo na mpango mzuri utasababisha mashabiki waone mpira ni sehemu ya starehe. Timu, shirikisho la soka Tanzania (TFF) na serikali vinatakiwa kutengeneza mazingira mazuri ambayo mashabiki wengi watavutiwa nayo na kuona kwenda kuangalia mechi uwanjani ni moja ya starehe bora.

3: Hapana shaka aliondoka Simba, mikono ya Kagera Sugar ilikuwa haina hiyana kumpokea katika nyumba yao na wakampa heshima yote kama golikipa bora aliyewahi kutokea katika ardhi hii ya Nyerere kuanzia miaka ya 2000 mpaka sasa. Heshima hii aliipokea kwa mikono miwili na mioyo kunjufu na alishiriki kikamilifu kuhakikisha Kagera Sugar ya msimu uliopita kuwa ni moja ya timu tishio kwenye ligi yetu, msimu uliopita ulipoisha nafasi ya msimu huu kukimbia ilifika, Kagera walianza kwa kuchechemea ila leo wanaelekea kumaliza ligi wakiwa wamesimama na leo hii Juma Kaseja kawabeba mgongoni na kumwanga sufuria la pilau ya Simba.

4: Wakati miguu ya Emmanuel Okwi ilipokuwa nyuma ya mpira uliokuwa umetengwa kwa ajili ya penalti, akili yangu iliniambia mbio za Emmanuel Okwi kufikisha magoli 21 zilikuwa zinaenda kutimia lakini kitu kilichokuja kuangusha mafikirio yangu ni pale miguu ya Emmanuel Okwi ilipokuwa imejaa furaha zaidi ya umakini na kusahau kuwa wanatakiwa kumaliza mechi wakiwa hawajapoteza hata mechi moja ili sherehe yao ifane zaidi.

5: Mwanzo wa kupoteza kwa Simba mechi hii ulianzia nje ya uwanja siku kadhaa kabla ya mchezo huu kuchezwa. Kila shabiki alikuwa anatambwa kuhusu mechi hii kitu ambacho siyo kosa kwa mashabiki maana ndiyo kazi yao waliyokuja kuifanya duniani. Viongozi walijiingiza kwenye mtego wa mashabiki na wao wakavua suti ya uongozi na kuvaa suti ya ushabiki hali ambayo iliingia kwenye mishipa ya wachezaji wa Simba. Waliona kazi wameshamaliza tena, hakuna wa kuwafunga na watawafunga Kagera Sugar mbele ya Raisi, kitu hiki kiliongeza kujiamini kwao. Wakajiamini kupitiliza hata umakini ukatoweka ndani yao. Hawakuwa wanacheza kama timu ambayo ilikuwa na mpango wa kushinda mechi hii ya leo, furaha na kujiamini kulikuwa kumewajaa kupitiliza kuliko umakini wa mechi husika.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x