Sambaza....

Wakati natazama mechi ya mwisho ya Cesc Fabregas akiwa na uzi wa Chelsea kitu cha mwisho kuja katika akili yangu ni sura ya Haruna Niyonzima.

Sura yenye upole, sura ambayo imebeba taswira ya mchezaji anayejitambua sana. Mchezaji ambaye alitoka Rwanda kuja Tanzania kufanya kazi.

“Fundi” ndilo lilikuwa neno pekee ambalo lilitumika kuelezea kipaji chake. Ungeweza kuandika au kuongea maneno mengi sana kuelezea kipaji chake.

Cesc Fabregas

Lakini neno pekee ambalo lilikuwa linaelezea kwa ufasaha kipaji chake na wengi wakakuelewa ni kutumia neno “fundi”.

Miguu yake ilikuwa imebeba kila aina ya rangi nzuri duniani. Ilikuwa haijalishi ni kiasi gani mpira ulikuwa umechafuka au ulikuwa mbaya lakini kila ulipokuwa unafika kwenye kiatu cha Haruna Niyonzima ulikuwa unapakwa rangi na kuonekana mpya tena.

Upya ambao ulikuwa unavutia machoni mwa watu. Ghafla akawa kipenzi kikubwa sana cha watu. Wengi walimhusudu sana.

Walipendezwa naye sana, na alipokea mahaba ya dhati kabisa kutoka kwa mashabiki. Kama tunavyojua mashabiki wa timu za Kariakoo wakikupenda wanakuwa wamekupenda haswaa.

Na wakikuchukia wanakuwa wamekuchukia haswaa. Hawana unafiki hata chembe. Na hii ndiyo zawadi kubwa ambayo alikuwa anaipokea Haruna Niyonzima kwa mashabiki wa Yanga.

Walikuwa wanampenda sana, tena kupitiliza. Hawakuona kama kuna kiungo mwingine ambaye angeweza kuwapa burudani kama Haruna Niyonzima.

Ndiyo maana wakambatiza jina la Fabregas. Fabregas huyu ambaye leo hii anaondoka katika kikosi cha Chelsea na kwenda As Monaco.

Sababu ambayo inamuondoa Cesc Fabregas pale Darajani ndiyo sababu ambayo inamkabili kwa sasa pacha wake Haruna pale Msimbazi.

Cesc Fabregas alikosa nafasi mbele ya kina Jorginho. Bado yuko fit. Hata miguu yake ikipokea mipira inaonekana kabisa bado ana kitu.

Na yeye anaamini sana bado ana kitu kikubwa sana cha kutuonesha sisi wapenda soka. Ndiyo maana anaenda kwenye ligi ya ushindani.

Bado anaamini hajafikia hatua ya yeye kwenda kucheza bonanza huku akipokea pension yake katika nchi za China na Marekani.

Anapigana sana na hilo. Bado anaamini kesho yake ni ya ushindani. Hata kwa Haruna Niyonzima kila akipokea mpira unaona kabisa bado anaamini anauwezo wa kuendelea kupambana.

Tatizo linakuja moja tu, alipo yeye ni chagua la tatu kwa sasa. Kuna Chama pamoja na Hassan Dilunga katika nafasi yake.

Wachezaji ambao wanaonekana tayari wameshajingea uaminifu kwa kocha Patrick Assumes.

Utaanzaje kufikiria kumweka benchi Chama na kumwingiza Haruna Niyonzima?, nahisi watu wengi watakuona ni kichaa.

Siyo kwamba Haruna Niyonzima ni mchezaji mbaya. Lakini tatizo ni moja, wakati Chama anahangaika kujitengenezea ufalme wake , Haruna Niyonzima alikuwa zake Rwanda.

Hakuwa na habari kabisa. Hakujali chochote, nahisi alikuwa anajiamini sana kipindi hicho. Sawa alikuwa anadai haki zake lakini kichwani kwake alikuwa anajua akirudi Simba namba yake ilikuwepo.

Unajua kwanini?, kwa sababu Haruna Niyonzima alitakiwa na mashabiki wengi wa Simba toka zamani. Wakati yupo Yanga wengi walikuwa wanaamini anauchezaji wa Yanga.

Hiki ndicho kitu ambacho kilikuwa kinampa nguvu Haruna Niyonzima. Aliamini mashabiki wana kiu ya kumuona.

Niyonzima

Aliamini siku yoyote ambayo angerudi angepata nafasi ya kucheza tu. Hili lilikuwa kosa kubwa sana kwa Haruna Niyonzima.

Haruna Niyonzima alisahau kuwa kocha ndiye mwenye mamlaka ya kuchagua timu ambayo anaipenda yeye.

Hakuna shabiki hata mmoja anayeweza kuchagua mchezaji kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha timu husika.

Yale mahaba ya mashabiki wa Simba yalimpa kiburi sana Haruna Niyonzima, na kibaya zaidi kipindi anagoma kucheza ndicho kipindi ambacho Chama anapigana kuingia kwenye kikosi.

Chama hakufanikiwa pekee kuingia kwenye kikosi cha Simba bali alifanikiwa kuingia kwenye mioyo ya mashabiki wa Simba.

Kwa sasa ni inahitajika kazi kubwa sana kumweka benchi Chama, mtu ambaye anaonekana kabisa halitamani benchi.

Haruna Niyonzima afanyeje?, kitu kimoja anachotakiwa kukifikiria Haruna Niyonzima ni yeye kumtazama somo wake Cesc Fabregas.

Cesc Fabregas aliona umri wake unaenda sana, kama ilivyo kwa Haruna Niyonzima. Umri ambao mchezaji hatakiwi kukaa benchi na kuanza kupigana kuingia kwenye kikosi cha kwanza.

Siyo kijana mwenye umri wa miaka 23 tena ambaye tunaweza kusema kuwa ana muda mwingi wa kucheza. Umri wa yeye kuvumilia ili kupata nafasi ya kikosi cha kwanza.

Yupo umri ambao anatakiwa kuendelea kupata nafasi ya kucheza. Ni umri mkubwa , hana tena muda wa kuendelea kupigana.

Anastahili kuwepo sehemu anbayo ataaminiwa na yeye kuitumikia timu husika katika siku zake za mwisho. Cesc Fabregas anaenda As Monaco.

Sehemu ambayo anaamini atapata nafasi kubwa na yeye kuonesha uwezo wake ambao uliwekwa kwenye miguu.

Hiki ndicho ambacho Haruna Niyonzima anachotakiwa kukikumbuka kwa sasa. Atazame umri wake kisha afanye maamuzi.

Aende sehemu ambayo atapata nafasi ya kucheza. Mimi bado naamini Haruna Niyonzima hàjafa kabisa , labda yeye ndiye aamue kujiua na kujizika kwa kuendelea kusubiri kuwa ipo siku moja atamweka benchi Chama.

Sambaza....