Mchezp wa Simba dhidi ya TP Mazembe katika Dimba la Benjamin Mkapa
Mabingwa Afrika

Simba haoo “NUSU FAINALI”

Sambaza....

“Jasho la damu”, au “jasho na damu” vyote vinaweza vikatumika kama misamiati mipya kuelekea katika mpambano wa kukata na shoka siku ya jumamosi kule Kinshansa nchini Congo pale Kunguru, TP Mazembe anapoenda kumvaa Mnyama  katika mchezo wa Marudio klabu bingwa Afrika.

Katika mchezo wa awali Simba ililazimishwa sare ya kutofungana ingawa katika uhalisia ilistahili kupata  matokeo. Nasema walistahili kwa kuwa, wao ndio walitawala mchezo katika  idara nyingi.

Simba waliongoza kwa kumiliki mpira, walimiki kwa asilimia 54 ukilinganisha na 46 za TP Mazembe, walipiga mashuti 12 ukilinganisha na 10 ya Mazembe. Lakini ukiachana na vitu hivyo, jambo la msingi zaidi ni kujua kama Simba walitawala maeneo muhimu ambayo huenda yangewapa ushindi.

Licha ya mambo yote hayo lakini Simba walionekana kufanya vibaya kwa baadhi ya maeneo na takwimu. Mfano, wachezaji wa Simba walipoteza mipira 19 ukilinganisha na 7 ya TP Mazembe. Kupoteza mipira ni kukosa umakini, na hii inaweza ikawaathiri Simba katika mechi ya marudio.

Kingine Simba walishindwa pia katika mipira ya 1 against 1, yaani mipira ya hamsini kwa hamsini. Asilimia 58 Simba walishinda mipira hiyo, lakini TP Mazembe walishinda mipira hiyo kwa asilimia 66.

Simba pia waliongoza kwa kufanya madhambi, walifanya madhambi mara 23 ukilinganisha na TP Mazembe waliofanya mara 22. Kama Simba watafanya makosa mengi zaidi itawaruhusu TP Mazembe kutumia mipira hiyo ya kutenga kwa kuwa ni wazuri kwa kupiga faulo.

Katika dakika zote  90 za mchezo wa awali, Simba imefanya shambulizi moja tu la kushtukiza  Huku TP Mazembe wakishindwa kufanya shambulio lolote la kushtukiza. Kushindwa kufanya mashambulizi ya kushtukiza wakati timu imeingia na mfumo wa  4-4-2 ni dalili za kutoumudu mfumo huo.

Katika mchezo wa awali Simba ilianza na mfumo wa 4-4-2, Zana Oumary Coulibaly, Erasto Edward Nyoni, Sergie Paschal Wawa na  Mohammedi Husseini Zimbwe JR, Viungo wanne wa kati  walioanza ni Clatus Chotta Chama, Jonas  Mkude , James Kotei na Haruna Akizimana Fadhili Niyonzima, na kule mbele straika wawili Meddie  Kagere na John Raphael Bocco walianza. Juuko Mursheed na Emmanuel Anord Okwi ndio walioingia kuchukua nafasi za Wawa na Chama mtawalia.

Katika kikosi Hiki Simba walionekana kumiliki mpira katika eneo la kati, na hii ilimfanya James Kotei kung’ara katika eneo la chini. Kiujumla Tshabalala alionekana kung’ara zaidi ukilinganisha na mabeki wengine.

Katika eneo la kiungo, Kotei na Niyonzima walionekana kung’ara zaidi ukilinganisha na Mkude na Chama.

Kwa upande wa TP Mazembe, wao hawakuwa na tofauti yoyote ya kimfumo, wao huanza na mfumo wa 4-2-3-1 mabadiliko makubwa yakiwa kwa upande wa wachezaji  hasa katika eneo la golikipa, beki na kiungo.

Beki kama Djo Isamma Mpeko alianzia benchi na hakucheza kabisa katika mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na Godet  Masengo. Mabeki wengine waliozoeleka walianza kama Kabaso Chongo, Kevin Mondeko Zatu na Joseph Ochanya.

Katika eneo la kiungo wa chini, TP huanza na viungo wawili, ambapo Miche Mika alianza na Christian Koffi. Katika viungo wa watatu wa juu, Abdoulaye Sissoko, Tresor Mputu na Rainford Kalaba walianza huku Jackson Muleka akibakizwa kama mshambuliaji wa mwisho.

Katika kikosi hicho cha TP Mazembe ni wachezaji watatu pekee tegemeo hawakuanza katika kikosi cha kwanza cha kocha Pamphile Mihayo Kazembe, nao ni golikipa Ibrahim Mounkoro, beki wa kulia Djo Issama Mpeko na kiungo wa kulia Meschak Elia.

TP Mazembe walijaribu kucheza kwa kutanua mpira , kuhakikisha wanailazimisha Simba ijiachie eneo la kati na walifanikiwa kufanya hivyo hata baada ya mabadiliko waliyoyafanya kwa kumuingiza Meschak Eliya, Nathan Sinkala na Glody Likonza.

Christian Koffie

Kupitia mfumo wao wa 4-2-3-1, TP walionekana kuimarika zaidi eneo la kati na la ulinzi, kwani pindi timu iilipokuwa inashambuliwa, ilikuwa na mabeki watano, yaani kiungo mmoja kati ya Miche Mika na Christian Koffi alishuka chini zaidi kusaidia ulinzi. Miche Mika alionekana kung’ara zaidi katika mchezo huu, alifanya kila liwezekanalo kuhakikisha safu yake ya ulinzi inakuwa salama.

Timu ilipokuwa inashambulia, ilikuwa na wachezaji watano kama washambuliaji, yaani Box-box Midfielder mmoja wa chini hupanda juu kuungana na viungo watatu wa kati na mshambuliaji Muleka na kuwa na jumla ya wachezaji watano mbele.

Je Simba Ifanyeje ili kupindua meza?

Natarajia mbinu za kiuchezaji ndizo zitakazo wapa matokeo Simba, kule Kinshasa hakuna mashabiki wa Simba kama wa uwanja wa taifa. Maana yake lazima Patrick  Aussems aje na “game plan” yenye tija kwa timu kutokana na aina ya wachezaji aliokuwa nao.

Katika mechi ya awali alitumia mfumo wa 4-4-2, naona hii ni kutokana na majeraha ya Okwi. Lakini Okwi angekuwa fiti kwa asilimia 100, Aussems angetumia mfumo wa 4-3-3. Na hata mimi nashauri mfumo huu ndio ukatumike kupindua meza kule Congo.

Mashabiki wa Simba Sc

4-4-3 hutumia mabeki wanne, Simba wakianza na Zimbwe kushoto, Coulibaly kulia, katikati Juuko na Nyoni. Hapa beki itakuwa imekaa sawa. Mfumo huu hutegemea utimamu wa viungo watatu wa kati ili kuleta “fluidity na Flexibility” ya timu . Timu itakuwa na uwezo wa kumiliki mpira, kukaba na kuufikisha mpira eneo wanalotaka.

Aussems anaweza kuanza na James Kotei kama kiungo wa chini, kwa sababu ni mechi ya ugenini huyu kazi yake iwe ni kuilinda beki pekee (defender) kwahiyo Kotei atumike kama MLINZI WA WALINZI.

Mfumo huu unamuhitaji “controller” yeye awe anaunganisha vyema eneo la kati, na kushusha presha ya timu yake na timu pinzani, huyu ni kiungo wa kati (central Midfielder) hapa Mkude anafaa zaidi, hasa kutokana na aina ya mpira anaocheza.

Mwisho kabisa eneo hili linahitaji “Mpishi” yaani “ creator” huyu ndiye kiungo mshambuliaji anayeunganisha eneo la kati na la ushambuliaji. Clatus Chama anastahili kucheza nafasi hii. Faida kubwa aliyokuwa nayo ni uwezo wa kukaba kuanzia juu na kushambulia kwa kupiga pasi za mwisho na mafanikio wakati wa kukokota mpira ( successful dribbling).

Mkude na Chama wacheze juu kidogo ya Kotei. Na hapo ndipo Mkude hubeba majukumu makubwa zaidi, kwani anatakiwa achezee katikati ya Chama (creator) na Kotei (defender), yeye ni “Controller”. Mfumo huu ndio uliompa mafanikio makubwa Pep Guardiola, akiwa na viungo kama Sergio Busquets, Andres Iniesta na Xavi, wakipewa majukumu kama ya Mkude, Kotei na Chama.

Kwa upande wa washambuliaji, Meddie Kagere anastahili kuwa straika wa mwisho (central Forward). Anafaa kucheza hapo kutokana na sifa kuu ya kukaa eneo moja ukilinganisha na John Bocco. Huku Bocco na Okwi kucheza pembeni ili kumsaidia Meddie kuweka presha katika eneo la beki ya kati.

Emmanuel Okwi akichezea kama mshambuliaji wa pembeni (wide forward) huwa ni hatari zaidi akiwa na mpira na hata wakati wa kushuti. Kucheza kama Cristiano Ronaldo katika eneo hilo kutaipa mafanikio makubwa klabu ya Simba katika mchezo wa marudiano.

Mabeki wa pembeni, Zimbwe Jr na Coulibaly, ni lazima wakawe makini zaidi, lazima wawe na uwezo wa kujua ni wakati gani wanatakiwa kushambulia, yaani “overlapping”. Ku-overlap kunahitaji nafasi ya kufanya hivyo, kama watafanya kwa wakati sahihi, Simba itanufaika lakini kama watakosea kufanya “timing” nzuri watajikuta wanafeli.

Okwi na Bocco lazima wajue, jukumu lao kubwa mbali na kushambulia wanahitaji kukaba kuanzia juu, na wanaweza kuupanua uwanja zaidi, kuchezea nje ya boki la 18, lakini wakati Mabeki wa pembeni wanapopanda wao inatakiwa waingie ndani kuongeza nguvu eneo la Meddie Kagere.

Kagere

Kagere lazima akae pale mbele bila kutoka na kuliacha eneo hilo, unajua kwanini? Kwa sababu mabeki wa Mazembe kama Chongo na Zatu hupanda kushambulia wakijua timu wanayocheza nayo ni ya kawaida. Kama Kagere atafanya hivi maana yeke anawalazimisha mabeki hao wa kati kufanya makosa ambayo yanaweza yakawa faida kwa mnyama.

Ni matarajio yangu kuwa, Okwi atakuwa msaada mkubwa kwa kikosi cha Msimbazi, hasa kwa mipira ya kushambulia kwa kushtukiza, na mipira mirefu ikijumuishwa na kasi na uwezo wa kupiga nje ya 18. Pia atatumika kupunguza kasi ya Beki mmoja wa pembeni kati ya Ochanya na Issama kushambulia kama Wing-back.

Kotei na Mkude watakuwa na kazi kubwa sana, kuhakikisha timu inatulia na Manula haguswi ovyo na hafikiki kirahisi. Tukumbuke, Mazembe huanza na viungo watano katikati, wawili wakiwa chini na watatu juu.

Kama Simba watacheza kwa mkakati hasa kushambulia na kukaba, Simba lazima watinge nusu fainali.  Kwa kutumia mfumo huu, Simba ikiwa inashambulia itakuwa na wachezaji 7 yaani mabeki wawili wa pembeni, wakiungana na Chama na Mkude na washambuliaji 3 wa juu, jumla yao itakuwa 7.

Wakati wa kushambuliwa Simba itakuwa na walinzi watano, akiongezeka James Kotei, lakini balaa litatokea endapo TP Mazembe watafanya mashambulizi ya kushtukiza, hasa katika kipindi cha Mpito, maana yake nyuma Simba itakutwa na mabeki watatu pekee ambao ni Kotei, Nyoni na Juuko.

Michezo ya Ugenini ina nidhamu yake ya uchezaji na mfumo wa 4-3-3 unaweza ukawa ni mfumo wa ushambuliaji au kujilinda kulingana na aina ya wachezaji wanaotumika na wajukumu waliyopewa. Mfumo unaweza kubadilika na kuwa 4-2-3-1, yaani Kotei na Mkude wawe chini zaidi, Chama aungane na John Bocco na Okwi katikati  na Kagere abaki peke yake juu.

Je Unadhani Simba wanaweza kupindua Meza? Unahisi Simba watakwama wapi?

Kandanda inawatakiwa kila la Heri, Simba katika mchezo wake huu wa marudiano siku ya Jumamaosi.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x