Mabingwa Afrika

Simba Ikitaka Jambo Lake Hakuna wa Kuwazuia.

Sambaza....

Jumamosi saa kumi jioni Simba watakua nyumbani kuwakaribisha Wydad Casablanca katika Dimba la Benjamin Mkapa katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika mchezo wa kwanza.

Katika kuelekea kwenye mchezo huo tayari uongozi wa Klabu ya Simba wameanza hamasa kwa mashabiki wao kuelekea mchezo huo muhimu katika kutimiza ndoto yao ya kucheza nusu fainali.

Katika hamasa hizo msemaji wa klabu ya Simba amewaambia mashabiki wa Simba kitu pekee wanachokiwaza sasa ni kuwafunga Wydad na kuwatoa katika mashindano mabingwa hao watetezi kutoka Morocco.

“Hakuna jambo lingine lolote tunaweza kuwaza kwa sasa zaidi ya kumfunga Wydad. Kila Mwanasimba anayo nafasi ya kuisaidia Simba kuandika historia ya kuitoa Wydad. Simba ni ya watu, na watu wakiamua jambo lao hakuna linaloshindikana,” alisema Ahmed Ally na kuongeza furaha yao si kumfunga Yanga tuu.

“Furaha yetu rasmi itapatikana baada ya kutinga nusu fainali. Hii ya kuwafunga Yanga ni kuwazodoa, malengo yetu ni kwenda nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa. Kuwafunga hawa ambao tumewazidi kila kitu ni kuwakomoa tu, tumeshawafunga sasa tunawaangalia Wydad.

Ahmed Ally akiongea na Wanasimba wa Chalinze

Mashabiki mkitimiza wajibu wenu kwa kuja uwanjani kushangilia, benchi la ufundi likiwapa maelekezo mazuri wachezaji na wachezaji wakitimiza wajibu wao Wydad hawana pa kutokea,” Ahmed Ally aliongeza.

Msemaji huyo pia aliwashukuru Wanasimba wa Chalinze na kusisitiza Simba ni ya watu wote lakini wanajua mtihani mzito uliopo mbele yao na wapo tayari kwenda kuandika historia ya mwaka 2003 walipowatoa Zamalek.

“Tunawashukuru Wanachalinze kwa kukubali ombi letu la kuja kuzindulia hamasa hapa. Siku ya leo ni uzinduzi wa hamasa kuelekea mchezo dhidi ya Wydad. Mara zote tumekuwa tukifanyia Dar es Salaam lakini safari hii tumeamua kufanyia nje ya Dar. Simba ni kubwa na kila Mwanasimba ana haki sawa kama ilivyo kwa Wanasimba wa Chalinze,” Ahmed Ally na kuongeza

Wydad Casablanca wapinzani wa Simba katika robo fainali.

“Mechi ni ngumu, tutacheza na mabingwa watetezi, timu kubwa zaidi yetu lakini Wanasimba tukishikamana, Wydad wakija hata na Wamorocco wote hawana pa kutokea. Kila Mwanasimba lazima ajue ana wajibu mkubwa kututoa robo kwenda nusu fainali.

Tunataka kutoka kwenye robo fainali, robo kwetu sio mafanikio, ni mtindo wetu wa maisha, mafanikio ni kumtoa Wydad. Inaonekana ni ndoto lakini Simba tunazungumza tunayoweza kuyafanya. Simba tumewahi kuyafanya, mwaka 2003 tulifanya kama hivi,” Ahmed Ally alimalizia.

Wekundu wa Msimbazi Simba kabla ya msimu kuanza waliweka malengo ya kucheza nusu fainali baada ya kuchezo robo fainali mara kwa mara ya michuano hiyo mikubwa Afrika na sasa ni lazima waifunge Wydad Casablanca ili kuishi ndoto zao

Sambaza....