Mashabiki wa Simba Sc
Blog

Simba ilishajiandaa kushindwa, Sven hana lawama.

Sambaza....

Sauti ya Shabiki wa Kandanda ni sehemu ambayo hukusanya maoni ya mashabiki kutoka katika mitandao ya kijamii. Haya ni maoni ya shabiki.


Dakika tisini zimetamatika kwa Simba kupoteza fainali ya pili mfululizo mbele ya Mtibwa Sugar katika michuano ya kombe la Mapinduzi mjini Unguja.

Kama kumbukumbu zetu zipo sawa ni Simba hii hii ambayo ilifungwa na Azam mwaka jana katika kombe la Mapinduzi mjini Pemba.

Pengine mchezo wa jana ni maumivu mengine kwa Wanasimba katika kipindi cha muda mfupi, maumivu ya kupata sare kwenye dabi ya Kariakoo yalikuwa bado hayajaisha kwenye mioyo yao.

Sven akiwa na timu yake ya ufundi

Kama haitoshi matokeo waliyoyapata mbele ya Mtibwa Sugar ni kama kuwekwa msumari wa moto kwenye kidonda kibichi.

Chini ya tajiri Mo Dewji matarajio yalikuwa makubwa, hakuna shabiki yoyote wa Simba aliekuwa akitembea kinyonge, walivimba, waliwadhihaki watani wao kwa hali ngumu wanayoipitia.

Ni mashabiki wa Simba pekee ambao waliamini kuwa wao wana timu bora zaidi Afrika Mashariki, Simba yenye John Bocco, Emmanuel Okwi, James Kotei, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Haruna Niyonzima na wengineo lukuki.

Baada ya miaka 15 Simba ikafika tena hatua ya makundi katika michuano ya CAF, jitihada zililipa.

Njaa ya mafanikio, upendo baina yao, sapoti ya mashabiki ndio zilikuwa silaha muhimu kwa Simba ili kumuangamiza mpinzani.

Baada ya msimu wa mwaka jana kuisha Simba ikaachana na wachezaji wengi ambao kwa namna moja ama nyengine waliifanya Simba ipate mafanikio baada ya kipindi cha muda mrefu.

Wachezaji kama James Kotei, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Zana Coulibally, Nicolaus Gyan, Juuko Mursheed.

Siku chache mbele Simba ikafanikiwa kufanya maingizo mapya ya wachezaji Wilker Da Silva, Francis Kahata, Deo Kanda, Gerson Fraga, Santos Da Silva, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Miraji Athuman na Sharaf Shiboub.

Ni kweli Simba kabla ya hapo ilikuwa inahitaji kufanya usajili lakini sio usajili wa karibu kikosi kizima.

Lilikuwa ni jambo la busara kama wangejitahidi kubakisha wachezaji wao muhimu waliowapa mafanikio na kujazia nafasi chache ambazo ilikuwa ni lazima wafanye maingizo mapya.

Miongoni mwa sababu inazozifanya timu zetu zifanye vibaya basi ni hili la kujenga timu kila msimu unapoanza, hatuwezi kufika kwa staili hiyo.

Hakuna timu yoyote duniani inayoweza kupata mafanikio kwa baada ya kila msimu kuibomoa timu na kuijenga upya. Simba lazima wakubali kuwa hapa waliteleza.

Mtibwa wakishangilia bao lao pekee

Wachezaji kukaa pamoja kwa muda mrefu kuna faida nyingi, kwanza kuzoea wao kwa wao namna wanavyopaswa kucheza uwanjani.

Lakini pia nje ya uwanja watajenga mahusiano mazuri na kuzoeana jambo ambalo kwa asilimia kubwa ni chachu ya timu kuweza kufanya vizuri.

Lakini pia swala la kubadili mabenchi ya ufundi mara kwa mara ni tatizo jengine kwa timu zetu.

Watu wengi wameonekana kumtupia lawama kocha wa Simba Mr Sven, binafsi sioni kama lawama hizo anastahili kwa namna yoyote ile. 

Kocha ni mpya ndani ya timu, bado anapambana kuijenga timu na kutafuta kikosi cha kwanza, unapomlaumu ni kama kumkosea heshima.

Naliheshimu sana kombe la Mapinduzi, lakini Sven hakuwa na mahala pengine pa kutafuta kikosi chake cha kwanza na muunganiko wa timu zaidi ya kwenye michuano hii.

Mwisho wa siku jambo jengine linalowaumiza mashabiki wengi wa Kitanzania ni kuingia na matokeo yao uwanjani, mpira haupo hivyo.

Tubaki kuwaheshimu wapinzani na kuziheshimu dakika tisini ambazo kama umejipanga vizuri unakuwa na nafasi kubwa ya kushinda mchezo.


Imeandikwa na Swaleh Mawele.
Whatsapp: 0657230793 Instagram: @Mawele_Jr


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.