Blog

Simba ipo mgongoni mwa CHAMA

Sambaza....

Uliitazama Simba ya msimu Jana?, ile Simba ya moto , ile Simba ambayo ilikuwa na washambuliaji wawili hatari zaidi.

Hapana shaka Emmanuel Okwi ndiye alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Simba msimu jana, ndiye alikuwa baba.

Pamoja na kwamba Simba ilikuwa na wachezaji wengi wenye vipaji lakini huyu ndiye aliyekuwa mmiliki halali wa hii timu. Ndiye alikuwa uti wa mgongo wa Simba.

Kuna wakati Emmanuel Okwi alikosekana, na Simba ilikosekana kabisa uwanjani. Ilikuwa haina uwezo wa kushinda, hata kipindi ambacho ilikuwa inashinda ilikuwa inatumia nguvu nyingi sana.

Haukuwepo urahisi kwao wao wa kushinda kipindi Okwi anapokosekana!, na mwisho wa siku alifanikiwa kuwa mfungaji bora wa kikosi cha Simba na ligi kuu ya Tanzania.

Msimu mpya ulianza, msimu ambao ulikuwa na vingi ambavyo vilikuwa vinatia mashaka katika kikosi cha Simba.

Sababu kubwa ya mashaka hayo ni Masoud Djuma, huyu ndiye ambaye alikuwa anachelewesha vitu vingi ndani ya Simba.

Alifanikiwa kuwaaminisha watu wengi kuwa Simba anaiweza yeye tu!, alifanikiwa kwenye hili, watu wengi wakamwamini sana.

Na kuna wakati waliwahi kumkataa Patrick Assumes, wengi wao waliamini kupitia rangi ya Masoud Djuma.

Wengi walimuona kama Pep Guardiola mweusi, na hii ni kwa sababu moja tu, alifanikiwa kutengeneza timu ambayo wengi walikuwa wanaiamini sana tena kupitiliza.

Timu ambayo ilikuwa kwenye mgongo wa Emmanuel Okwi, timu ambayo kiasi kwamba ikifumuliwa tu kidogo, Simba ilikuwa haina uwezo wa kufurukuta.

Ndipo hapo ukawa mwanzo wa Masoud Djuma kuaminiwa sana kuliko kiumbe chochote kwenye benchi la ufundi la Simba.

Hii ikawa ngumu sana kwa Patrick Assumes kutengeneza timu ambayo alikuwa anaitaka. Kila alipokuwa anajaribu kutengeneza timu aliyokuwa anaitaka alishindwa.

Hakuwa huru sana kipindi alipokuwa pembeni na Masoud Djuma. Lakini alipoondoka Masoud Djuma, ndipo hapo tukaiona Simba mpya.

Simba ambayo ilikuwa katika mgongo wa mtu mwingine kabisa , ambaye ni Chama. Mzigo wote ulitolewa katika mgongo wa Emmanuel Okwi na kuwekwa kwenye mgongo wa Chama.

Huyu ndiye anayeamua kwa sasa timu icheze vipi. Huyu ndiye aliyetengeneza uso wa Simba. Kwa sasa uso wa Simba unang’ara sana.

Unafurahisha sana kuutazama uso wao. Huchoki kuitazama Simba kwa sababu tu ya Chama.

Ndiye mchezaji kwa mechi za hivi karibuni amefanikiwa kuhusika kwenye magoli mengi kuzidi mchezaji yeyote ndani ya kikosi cha Simba.

Ndiye mchezaji ambaye ameibeba Simba kwenye mechi hizi za kimataifa kwa kuhusika tu kwenye magoli muhimu.

Magoli ambayo yameifanya Simba kuingia hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Africa. Ndiye bosi halali wa kikosi cha Simba kwa sasa.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x