Meddie Kagere
Ligi Kuu

Simba kuwakosa wachezaji muhimu 9 leo dhidi ya Ruvu Shooting

Sambaza kwa marafiki....

Kikosi cha “Mpapaso Squad” Ruvu Shooting ya Masau Bwire leo kitakuwa na kibarua kigumu mbele ya mabingwa watetezi Simba SC katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara- TPL utakaochezwa katika uwanja wa Taifa majira ya saa moja za Usiku.

Ahueni huenda ikawa ni kubwa kwa kikosi cha Ruvu baada ya Simba kuwakosa wachezaji wake muhimu ambao huwa wanaunda kikosi cha kwanza.
Nahodha John Bocco, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Aishi Manula wameitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa kinachojiandaa kuwavaa Uganda katika harakati za kufuzu mashindano ya Afcon mwaka huu.

Meddie Kagere naye amejumuishwa katika kikosi cha Vincent Mashami,Rwanda Amavubi. Emmanuel Okwi na Juuko Mursheed nao tayari wameshaitwa na timu yao ya Uganda. Clatus Chama naye ameitwa kwenye timu yake ya taifa ya Zambia.

Kiujumla Simba leo itawakosa Clatus Chama, Meddie Kagere, Emammanuel Okwi, Juuko Mursheed, John Bocco, Jonas Mkude, Erasto Nyoni na Aishi Manula. Wachezaji hawa wote ni wa kikosi cha kwanza.

Tegemeo ni kwa Haruna Niyonzima ambaye hakuitwa katika kikosi cha Rwanda. Haruna ambaye alifanya vizuri katika mechi ya klabu bingwa Afrika dhidi ya AS Club Vita anatarajiwa kuibeba timu yake mabegani hii leo dhidi ya Ruvu Shooting.

Wachezaji wengine waliobaki ambao ni tegemeo ni Hassain Dilunga, Rashidi Juma, Hamis Ndemla, beki wa kushoto Mohammed Hussein Zimbwe, Mohammed Ibrahim, Mzamiru Yassin, Zana Coulibaly na Adam Salamba.

Simba ambayo ipo katika nafasi ya tatu ikiwa na alama 51, na imeshacheza mechi 20 itavaana vikali na Ruvu Shooting iliyo katika nafasi ya 16 ikiwa na alama 35 katika mechi 30 ilizocheza. Kila timu itahitaji kutoka katika nafasi iliyopo.

Kama Ruvu Shooting itapata ushindi leo itapanda mpaka nafasi ya 9, ikijikusanyia alama 38 itakuwa sawa na Coastal Union ya Tanga huku maombi ni kwa timu zingine kupata matokeo hasi.
Rekodi za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, Ruvu hawajawahi wafunga Simba, huku Simba ikionekana kutawala rekodi hizo kwani kipigo kwa Ruvu huanzia goli 2 kwenda juu. Je unadhani leo Ruvu Shooting wanaweza wakafanya maajabu kupindua rekodi?

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.