Sambaza....

Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba Sports Club wamezidi kudhihirisha ubora wao katika michuano ya Kimataifa baada ya kuwachapa Mbabane Swallows ya Eswatini kwa mabao 4-1 katika mchezo wa hatua ya kwanza ya michuano ya ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba ambao waliingia kwa kasi katika mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Pacifique Ndabihawenimana kutoka Burundi walianza kupata bao la kwanza katika dakika ya nane tu kupitia kwa John Raphael Bocco aliyonganisha pasi ya Mghana Nicolas Gyan.

Simba waliendelea kuliandama lango la wapinzani wao katika mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam lakini kukosekana kwa umakini kwa washambuliaji Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kagere kukawafanya Mbabane kuwa huru zaidi.

Hatimaye katika dakika ya 23 mlinzi wa Mbabane Guevane Nzambe akaisawazishia timu hiyo ambayo mwaka huu ilicheza hatua ya makundi ya kombe la shirikisho kwa shuti kali ambalo lilimshinda mlinda mlango Aish Manula na kujaa wavuni.

Wakidhani ya kwamba bao hilo litawaokoa, Emmanuel Okwi aliangushwa ndani ya 18 na mwamuzi Pacifique Ndabihawenimana akaamuru mkwaju wa penati uliopigwa kwa ufundi na John Bocco na kuiandikia Simba bao la pili lililodumu hadi kipindi cha pili.

Na katika dakika ya 84 Meddie Kagere akaiongezea Simba bao la Tatu baada ya makosa ya mlinda mlango Sandanelwe Mathabela aliyerudishiwa mpira lakini kabla ya kuuondosha akateleza na kumkuta Kagere aliyefunga kirahisi.

Zikiwa zimebakia dakika sita mpira kumalizika Simba wakazidi kulishambulia lango la Mbabane na juhudi hizo zilizaa matunda katika dakika ya 90 baada ya Cleutus Chama kufunga bao la nne baada ya kupokea pasi kutoka kwa Hassan Dilunga.

Matokeo hayo yanawapa matumaini makubwa Simba kusonga mbele kwani kama Mbabane watataka kusonga mbele basi watalazimika kushinda mabao 3-0 watakapokutana Jumanne ijayo kwenye uwanja wa Mavuso Sports Centre, mjini Manzini.

Mara baada ya mchezo huo kumalizika kiungo wa Mbabane Swallows Tony Tsabedze akasema kuwa mabao mengi waliyoyapata Simba yanawapa ugumu kuelekea katika mchezo ujao lakini hawatakatishwa tama na badala yake watajaribu kupambana katika mchezo ujao.

“Tumeruhusu mabao mengi leo, hii kwetu sio nzuri kwani tutalazimika kushinda mabao mengi nyumbani ili kuweza kusonga mbele, tumeruhus mabao matatu marahisi kabisa katika mchezo huu, hatukuwa makini lakini sasa tunaangalia namna ya kurekebisha makosa haya kabla ya jumanne,” amesema.

Kwa Upande wake nahodha msaidizi wa Simba Mohamed Hussein amesema matokeo haya ni mazuri lakini kuelekea katika mchezo ujao ni lazima wajitahidi kupata walau mabao mawili lakini wakihakikisha hawaruhusu kufungwa.

“Tumepata ushindi mzuri, nasema ni mnono lakini tunatakiwa kutobweteka, mchezo ujao ni muhimu kupata bao lakini kujizuia sisi kutofungwa ili kusonga mbele hatua inayofuata,” amesema.

Mshindi wa mchezo huo atakutana na mshindi kati ya UD Songo ya Msumbiji ambayo imekubali kichapo nyumbani kwake cha mabao 2-0 au Nkana ya Zambia iliyoshinda mabao hayo jioni ya leo.

Sambaza....