Ligi Kuu

Zifahamu mbinu za ‘Siri ya Urembo’ za Simba Sc

Sambaza....

Msimu mpya tayari umeanza, timu zote 18 zikiwa katika ari kubwa ya kuhakikisha zinavuna alama nyingi kwa kadri ziwezavyo ili kujitengenezea mazingira mazuri ya kugombania ubingwa la ligi kuu Tanzania Bara 2020/21.

Ligi ya msimu huu sio ndefu kama ilivyokuwa ya Msimu 2019/20, kwani msimu huu jumla ya timu 18 zinashiriki, tofauti na msimu uliopita timu 20 zilichuana na mwisho wa siku Simba wakaibuka vinara kwa kujikusanyia jumla ya alama 88 na kuwafanya kuwa mabingwa kwa mara tatu Mfululizo.

Je Simba watafanya tena maajabu msimu huu? Majibu ya swali hili ni magumu kidogo, kwani inabidi kuzingatia vitu  vingi ili kuoata majibu yake. Miongoni mwa vitu hivyo, ni usajili wa timu husika, Usajili kwa klabu zingine, Kiwango cha wachezaji wapya na waliopo, hali ya kiuchumi ya klabu husika, hali za wachezaji, morali na afya zao, mbinu za uchezaji  na aina ya kocha aliyopo na vingine vingi.

Vyote kwa pamoja huchangia ubingwa wa timu Fulani kwa msimu husika. Mbali na vitu hivyo, acha tukazitazame takwimu kiundani kidogo, ili kujua ni timu ipi ina nafasi nzuri kwa msimu huu.

Kwa mujibu wa Takwimu zinazopatikana katika mtandao wa Kandanda.co.tz zinaonyesha kuwa kwa mismu mitatu mfululizo Simba ipo kileleni kwa kujikusanyia alama nyingi zaidi ukilinganisha na klabu zinagine. Takwimu hizo zinaonyesha hivi.

Simba ipo katika nafasi ya kwanza ikiwa na jumla ya alama 250 kwa misimu yote mitatu, msimu wa 2017/18 ikijikusanyia alama 69 na kushika nafasi ya kwanza, msimu 2018/19 ikijikusanyia alama 93 na kushika nafasi ya kwanza, huku msimu uliopita wakijikusanyia jumla ya alama 88 na kubeba ndoo ya VPL.

Timu ya pili baada ya Simba ni Yanga ambayo kwa misimu mitatu imejikusanyia jumla ya alama 210. Takwimu zinaonyesha Yanga ya msimu 2017/18 ilijikusanyia alama 52 ikishika nafasi ya 3, msimu 2018/19 ikipata alama 86 na kushika nafasi ya pili huku msimu 2019/20 ikijikusanyia jumla ya alama 72 na kuangukia katika nafasi ya pili.

Tatu ya Tatu kwa kujikusanyia alama nyingi kwa misimu mitatu ni Azam Fc, yenyewe imejikusanyia jumla ya alama 203, huku msimu wa 2017/18 ikijikusanyia alama 58 na kushika nafasi ya 2, Msimu 2018/19 ikipata alama 75 na kushika nafasi ya 3, bila kusahau Msimu 2019/20 walijikusanyia alama 70 na kuendelea kushika nafasi ya 3.

Timu ya Nne ni Tanzania Prisons ya Mbeya, Wajela jela hao, wanaingia katika rekodi kwa kukusanya alama nyingi zaidi kwa misimu mitatu mfululizo. Wao Msimu 2017/18 walijikusanyia alama 48 wakishika nafasi ya 4 katika msimamo wa ligi, msimu 2018/19 wakijikusanyia alama 46 na kushika nafasi ya 12 huku msimu 2019/20 wakimaliza na alama 49 katika nafasi ya 10.

Takwimu hizi zina maana gani? Hii ni tafsiri tosha kuwa, timu yoyote itakayozifunga timu hizi nne, basi ina nafasi kubwa ya kushika nafasi nne za juu msimu huu.

Kuzifunga timu hizi, sio tu faida kwa timu kushika nafasi za juu zaidi lakini pia timu hiyo itakabidhiwa tuzo Maalumu kutoka kwetu kama TIMU GALACHA KWA MSIMU 2020/21.

Mtandao wako wa Kandanda Umejipanga kutoa zawadi hiyo ya heshsima kwa timu itakayojikusanyia alama nyingi zaidi miongoni mwa timu hizi nne za juu kwa misimu mitatu mfululizo.

Kwa mfano, timu kama Mbeya City inawezaje kuzifunga timu hizi zote 4? Ili kujua hili acha tuzitazame timu hizo kiundani, hasa kwa upande wa Ubora wake, udhaifu na aina ya vikosi vilivyopo.

Simba Sc.

Katika misimu yote mitatu, Simba imefundishwa na Makocha watatu, Mfaransa Pierre Lecchantre, Mbelgiji Patrick Aussems na sasa Sven Vandenbroeck.

-Meddie Kagere (Simba Sc

Katika misimu yote mitatu na misimu ya nyuma kabla hapo, falsafa za Simba zimekuwa hazibadiliki. Wao miaka yote hushambulia kwa kumiliki eneo la kati, huku mabeki wao wa pembeni wakionekana kushambulia muda wote.

Silaha yao kubwa ni pasi fupi fupi na wakati mwingine hupiga ndefu pembezoni mwa uwanja, ili kuwapa nafasi mabeki wa pembeni kushambulia.

Hii ina maana kuwa, Timu yoyote itakayoambua kidhibiti Simba eneo la kati na mabeki wa pembeni basi itapata alama tatu muhimu. Siri kubwa katika hili ni kuwa na viungo wanaokaba kwa kasi, na kutowapa viungo wa Simba  muda mrefu wa kubaki na mpira mguuni mwao na kuendelea kumiliki mpira.

Msimu uliopita, Simba imeambulia alama 2 tu kutoka kwa Tanzania Prisons ya Mbeya, huku mbinu kubwa iliyotumika ikiwa ni hii.

Yanga SC.

Katika misimu yao mitatu, Yanga imefundishw ana makocha watatu, akiwemo George Lwandamina, Mwinyi Zahera, Luc Eymael huku Msimu huu wakimuajili Zlatico Krmpotic.

Yanga nayo, imejikuta ikibaki na falsafa yake mama ya kushambulia kupitia kwa mawinga na mabeki wake wa pembeni.

Hapa namaanisha ili kuidhibiti Yanga ni kuwalazimisha wasichezee pembeni mwa uwanja. Timu yoyote itakayofanikiwa kuwadhidbiti mawinga wa Yanga na Mabeki wake wa pembeni kupiga Krosi, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuvuna alama tatu au kupata japo alama moja.

Azam FC

Katika misimu yote mitatu, Azam imefundishwa na makocha zaidi ya watatu, Stewart Hall, Hans Pop, Ettiene Ndayiragije na sasa Aristica Cioaba.

Azam wamejaribu kubadilika badilika kulingana na kocha husika, kuna muda waliwatumia zaidi viungo kumiliki dimba la kati na kushambulia, lakini kwa siku za hivi karibuni, Azam ya Cioaba imekuwa ikiwatumia zaidi mawinga na mabeki wa pembeni kushambulia katika mfumo wa 4-4-2.

-Nizar Khalfani akimkabidhi Tunzo ya Galacha wa Hatrick mshambuliaji wa Azam fc Obrey Chirwa.

Tofauti pia na msimu huu katika mchezo wa awali ambapo Azam walitumia mfumo wa 4-3-3, huku majukumu ya mabeki wa pembeni na mawinga wakitumika kupiga Krosi na V-Pass. Hii ndio maana ya Wadada kutajwa kuwa beki bora na mwenye pasi za mwisho nyingi nyuma ya Clatus Chama wa Simba.

Mbinu za Kuifunga Azam ni sawa na zile za kuifunga Yanga tu, yaani timu yoyote isikubali, mabeki wa pembeni  wa Azam na Mawinga wao kushambulia kwa kulitawala eneo la pembeni mwa uwanja.

Tanzania Prisons.

Wajela jela wakitokea Mkoani mbeya, kwa sasa watatokea Mkoani Sumbawanga. Katika misimu yao mitatu, hawakuwa na mabadiliko makubwa katika benchi lao la ufundi, kwani hadi sasa imefundishwa na makocha wawili tu Salumu Mayanga na Abdallah Mohamedi kabla ya kumrejesha Salumu Mayanga tena.

Lakini hata hivyo, Prisons wamekuwa wakisifika kwa Mpira wao wa Nguvu nyingi. Sifa yao kubwa ni kukaba kwa kasi, kuziba mianya ya pasi na kuwanyima wapinzani nafasi ya kumiliki mpira na kutengeneza nafasi za wazi zaidi.

Bila shaka timu kama hizi huwa zinafungwa magoli machache zaidi, kwani goli kufungwa ni matokeo ya nafasi za wazi zinazotengenezwa na timu pinzani.

Hii ndio maana halisi, kwanini Simba imeambulia alama mbili pekee katika mechi zote mbili za msimu uliopita.

Je ni timu gani, itapata tuzo ya Timu GALACHA Msimu 2020/21? Acha tusubiri na kuupa nafasi muda, kwani una majibu ya haya yote.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.