Sambaza....

Ukiwa mtaani kwa sasa, mambo ni bomba kabisa kwani kila shabiki wa soka nchini hasa wale waumini wa soka la ndani basi ni furaha tupu. Ni mara chache sana kukuta mashabiki wote wanafurahi lakini kwa wale wa timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam Fc wote wanafuraha kwa kuwa timu zao zimewatoa kimasomaso katika mechi za hivi karibuni yaani jana na juzi.

Yanga ilikuwa kule Mbeya kupepetana na Maafande wa Prisons na kufanikiwa  kupata alama zote tatu huku mfalme akiwa ni Amis Tambwe.  Azam wamepata ushindi mbele ya Stand United, shujaa akiwa ni kinda  Yahya  Zayid.

Na kimataifa, katika klabu Bingwa Afrika, Simba  imeshusha kipigo cha Mbwa koko cha mabao 4-0 dhidi ya Mbabane Swallows, Mashujaa wakiwa ni Clatus Chama, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Na katika shirikisho Afrika, Mtibwa Sugar imeichapa Dynamo goli 1-0, shujaa akiwa ni Haruna Chanongo.

Ukitazama wafungaji katika timu hizo kubwa mbili, wote ni wageni, kwa maana ndio wanaounda idadi ya wachezaji 10 wanaotakiwa kwa mujibu wa sheria nchini katika timu zao.

Tambwe, aliifungia Yanga bao 2

Tangu Shirikisho la Soka Nchini (TFF) chini ya Rais Wallace Karia kupitia  kwa kamati ya utendaji ya TFF kupitisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa  kusajiliwa na vilabu vya Tanzania  July 12 mwaka huu kumekuwa  na mjadala mzito juu  ya athari ya maamuzi hayo kwa maendeleo ya soka nchini na timu ya taifa kwa ujumla wake.

Nakaumbuka  maneno ya mchezaji wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania Ally Mayay Tembele wakati wa mjadala huu alisema kuwa, kupita kwa sheria hii kutaleta tija kwa taifa hasa kuifanya ligi yetu kuwa maarufu, Afrika mashariki na Afrika kwa ujumla.

Maneno yake yanasadiki ukweli  kwa hivi sasa, kwani ligi ya Tanzania inafuatiliwa na watu wengi nje ya Tanzania, wengi wakitaka kuwaona wachezaji wao wanachokifanya  ndani ya klabu zao.

Mchezaji kama Chama, bila shaka Wazambia wanafurahia  kazi yake na wanapenda kumuangalia wakati wa mechi, hii ni sawa na watanzanaia kumuangalia Samatta akiichezea KRC Genk. Ligi ya ubelgiji imekuwa maarufu Tanzania kwa sababu ya mtu mmoja tu “SAMATTA”

Bila shaka mjadala huo umepoteza umaarufu kwakuwa  mambo ni tofauti na watu walivyotazamia, wachezaji wa kigeni wamekuwa wakizibeba timu zao pale zinapokwama, katika mashindano yote.

Harakati za mabadiliko ya idadi ya wachezaji wa kigeni hazikuanza leo, tangu kwa Rais Leodegar Chila Tenga, ambapo walikuwa 5, Jamali Malinzi akaiongeza idadi hiyo na kuwa  7  huku watakaoruhusiwa kucheza katika mchezo mmoja  ni  watano, chini ya Rais Karia, idadi ikaongezeka maradufu na kuwa 10 na wanaruhusiwa kucheza wote.

Labda niulize hivi una mchezaji mwenye kiwango poa kama Clatus Chama  na unafikiria juu ya wachezaji 10? Huyu chama tunayemjua sisi alikuwa ndiye mchezaji wa mwisho kusajiliwa akitokea Dynamos  ya Zambia na kufikisha idadi ya wachezaji wa kigeni msimbazi kuwa  9.

Hii ina maana kuwa TFF ndiyo iliyomleta Chama Msimbazi, laiti kama sheria ingekuwa  mwisho ni wachezaji 7 huenda tusingemuona  Chama.

Hatimaye sheria hii inawanufaisha Simba katika harakati zake za kucheza hatua za makundi  Klabu Bingwa Afrika ikiwa ni moja ya mbinu za kutimiza agizo la Rais wa Nchi John Pombe Magufuli la kuitaka Simba ifike mbali katika mashindano ya kimataifa.

Hii haimaanishi kuwa, katika klabu zetu hakuna wachezaji wa kigeni ambao hawana kiwango  cha kuwazidi wachezaji wa nyumbani na bado wanalipwa mishahara mikubwa  kuwazidi wazawa. Na hili ili lilete tija kwa  soka nchini bila shaka vilabu vinatakiwa kujipanga zaidi hasa katika kuweka vigezo vya usajili kwa wachezaji wa kigeni.

Kwa Klabu kama Simba ambayo muda mwingi huwa inajinasibu kufanya usajili wake kwa kufuata kigezo cha mchezaji huyo kuwa sehemu ya kikosi cha timu yake ya taifa bila shaka  kigezo hiki kitaisaidia timu  kupata wachezaji bora na wanaostahili kucheza ligi ya Tanzania.

Pia timu ziwe na msingi wa kuwa na mawakala (team agents) wenye pua za kunusa viwango na vipaji kwa wachezaji. Mfano Clatus Chama hakuja Simba kwa kujileta mwenyewe bali kupitia kwa wakala wake, kampuni ya Bro Soccer Management  na kampuni hii ndiyo inayowasimamia wachezaji kama John Boko, Aishi Manula, Mudathir Yahya wa Tanzania. Pia hata beki wa kulia wa Simba usajili mpya, Zana Coulibaly naye yuko chini ya mawakala hawa.

Simba na wachezaji wengine wameitumia fursa ya kampuni hii kupata wachezaji bora kama Chama na Coulibaly. Timu lazima iwe na uwezo wa kuwajua mawakala wanaoweza kuwapa wachezaji wenye viwango vikubwa.

Endapo kama TFF watavilazimisha vilabu kuweka vigezo vya usajili wa wachezaji wa kigeni basi machungu ya kuwepo kwa  lundo la wachezaji wa kigeni wanaozidiwa viwango na wachezaji wa ndani hayatakuwepo na badala yake soka litakuwa kwa kasi ya 4G.

Hakuna ubishi kuwa mjadala wa wachezaji 10 umeshakufa, na walioua mjadala huu ni wachezaji wenyewe wa kigeni  wanaopata nafasi ya kucheza katika klabu zao akiwemo Chama, Okwi, Tambwe na kagere.

MJUE CLATUS CHOTA CHAMA ,TRIPPLE C, MWAMBA WA LUSAKA.

Ni mchezaji wa kimataifa wa kulipwa kutoka Zambia, alizaliwa tarehe 18 june,  1991 ana miaka 27.

Ni mchezaji wa Simba, ana mkataba wa miaka miwili,  kuanzia Julai 1, 2018 mkataba wake utamalizika June 21, 2020.

Ana uzito wa kilo 65 na urefu wa mita 1,77m

Wakala wake ni Bro Soccer Management.

Nafasi anayocheza ni kiungo mshambuliaji.

Mguu anaotumia ni wa kulia.

Thamani yake kwa sasa ni  Paundi 90k.

Kaka yake Andrian Chama  ni mchezaji wa klabu ya Green Buffaloes ya Zambia na anacheza na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Felix Sunzu katika klabu hiyo.

Kabla ya kutua Simba alicheza Nchanga Ranger mwaka 2012-2013, kisha Zesco United 2014-2016 na baadaye L. Dynamos ya Zambia mwaka 2017-2018 na mwisho kutua mtaa wa Msimbazi.

 

Sambaza....