Sambaza....

Hapana shaka hakuna mchezaji ambaye ni kipenzi cha wana Simba kwa miaka ya hivi karibuni kama Emmanuel Okwi. Mfalme wa himaya ya msimbazi, mfalme ambaye aliwahi kwenda kuishi kwenye ufalme wa Jangwani.

Ufalme ambao kwake yeye haukuwa ufalme wenye furaha, hakuna kitu kikubwa alichokifanya pale jangwani kwa sababu miguu yake ilikuwa jangwani lakini moyo wa kujituma na akili zake zilikuwa msimbazi. Sehemu ambayo kitovu chake kilizikwa, hakuna sehemu nyingine anayoweza kujihisi nyumbani kama msimbazi.

Shabiki wa Okwi na Simba SC

Hakuweza kustahimili raha za ugenini, kipindi kifupi kilitosha kumfanya aondoke jangwani. Alifuata furaha yake ilipo, akaenda kukaa sehemu ambayo inamtengenezea tabasamu, sehemu ambayo hufurahia kuwepo na huumia kipindi timu inapopitia wakati mgumu. Huu ndiyo mzizi wa upendo wa mashabiki unapoanzia, Emmanuel Okwi hajawahi kuwaangusha mashabiki wa Simba.

Hajawahi kuweka chozi la huzuni mashavuni mwao hata siku moja, miguu yake imekuwa kifaa tosha cha yeye kutengeneza furaha ya mashabiki kwenye paji la uso. Utaachaje kububujikwa na chozi la furaha unaposhuhudia umaridadi wa Emmanuel Okwi?.

Utaanzaje kukaa kwenye kiti uwanjani kipindi goli maridadi la Emmanuel Okwi unapolishuhudia likipenya kwenye mboni ya macho yako? Ni kitu kigumu sana, na ugumu huu ndiyo uliojengeka katika mioyo ya mashabiki wa Simba.

Furaha yao juu ya Emmanuel Okwi haifichiki, wameshondwa kujizuia. Chozi lao huteremka taratibu huku uso wao ukiwa na tabasamu kipindi wanapoona mpira upo katika miguu ya Emmamuel Okwi.

Kwa kifupi huyu ndiye fundi rangi anayetumika kupaka rangi mioyo ya mashabiki wa Simba, mioyo yao inavutia kwa sababu ya umaridadi wa rangi inayopakwa na Emmanuel Okwi.

Hata aliporudi msimu huu baada ya kukimbia mahamishoni kwa muda wengi wetu tulimbeza. Tulimuona Emmanuel Okwi ni mzee, hana tena kasi kama ile ambayo alikuwa nayo kipindi kile cha nyuma. Inawezekana unaweza usione kasi ya Emmanuel Okwi kwa sasa lakini kuna mabadilko mengi chanya ambayo yapo kwenye miguu na akili yake.

SIMBA ANAELEKEA KUWA BINGWA

PosTimuPWDLGDPts
12041404618279466
21961334320209442
31981105038153380
4198596871-36245
5196577267-19243

Mwili wake umevaa vazi la utulivu, macho yake yana mawani ya umakini na miguu yake ina bunduki yenye shabaha. Ana uhakika na anachokifanya kwa sasa, akili yake imeshapevuka tayari, hawazi tena kucheza na jukwaa kitu pekee anachowaza ni yeye kucheza na nyavu.

Nyavu za goli ziko wapi?, kipimo gani nitumie ili mpira niukwamishe kwenye nyavu?

Hii ndiyo tofauti ya Emmanuel Okwi wa zamani ma Emmanuel Okwi wa sasa ambaye tulimbatiza kuwa ni “mhenga” baada ya kuona kuwa umri wake umeenda na tukafikia hatua ya kubeza usajili wake.

Tulikosea kubeza usajilk wake ila tulipatia kusema kuwa Emmanuel Okwi ni “mhenga”, ameshakomaa tayari tena kwa kiasi kikubwa.

Hana mambo mengi yasiyo na faida uwanjani, ni mhenga haswaa, tena mwenye busara kubwa uwanjani ndiyo maana ameguka kuwa kiongozi bora katika kikosi cha Simba.

Nani alitegemea kama Emmanuel Okwi atakapokuja katika ardhi ya msimbazi anaweza akawa nahodha?

Kinachoonekana kwa sasa ndiyo tafasiri halisi ya neno “mhenga”, miguu yake haina mambo mengi yasiyo ya muhimu, kichwa chake kimejaa busara kubwa ya kuwaongoza wenzake.

Okwi akishangilia moja ya goli lake.

Timu inapoonekana kukata tamaa, miguu yake hutoa fundisho kwa wenzake kuwa hakuna kukata tamaa ndani ya muda ambao mnaweza kufanya kikubwa chenye manufaa.

Unaikumbuka mechi ya Al Masry ili iliyochezwa Dar es salaam na iliyochezwa Misri?

Yeye ndiye aliyewaonesha wachezaji wenzake kuwa tunaweza kuvuka huu mto wenye mamba wengi.

Kila mtu akawa jasiri wa kuogolea kwenye mto huo, nguvu za kupigana zilikuja baada ya kuona Emmanuel Okwi miguu yake haichoki na haijakata tamaa. Miguu ambayo mpaka sasa hivi imefanikiwa kufunga magoli 20 kwenye ligi yetu ya Tanzania bara.

Ligi ambayo alibezwa kuwa ni mhenga na hawezi kufika popote lakini miguu yake imefanikiwa kufika sehemu ambayo tulimtabiria mwanzoni mwa safari kuwa hawezi kufika.

Sambaza....