Meddie Kagere Akipokea tunzo
Blog

Tunzo za Simba ni tusi kwa Yanga!

Sambaza....

Tuko kwenye dunia ya ushindani, dunia ambayo milango na madirisha yake yana nembo ya neno linaloitwa Biashara.

Huwezi kuingia na kuishi kwenye dunia hii kama hujaruhusu akili kufikiria kibiashara, macho kuona kibiashara na masikio kusikia kibiashara.

Hivi ndivo vitu ambavyo vitakufanya uifurahie dunia na uione ni moja ya sehemu sahihi na bora kuishi, tofauti na hapo utabaki mtu wa kulaumu na kutia huruma kila uchwao.

Utabaki mtu wa kukufuru kila siku kwa sababu tu akili yako hujataka kuitesa isifikirie kibiashara, macho yako hujataka kuyafanya yaone kibiashara hata masikio yako hujataka kuyafungua yasikie kibiashara.

Dunia tuliyopo kila kitu ni biashara na hili tumekuwa tukiliimba kila uchwao, kila jua linapochomoza na kila jua linapozama, tumekuwa tukisisitiza mpira uangaliwe kwa jicho la kibiashara.

Tumekuwa tukiwaambia viongozi wengi wenye dhamana ya kuongoza mpira wetu waongoze kwa kutazama kwa jicho la kibiashara.

Tumeongea sana!, tumeandika sana! , tumesisitiza sana na kuwahimiza sana! , kwa kifupi tumekuwa hatuchoki kuwakumbusha kila siku.

Kuwakumbusha umuhimu wa wao kutengeneza mazingira bora na sahihi ambayo yanaweza kuwavutia wafanyabiashara wengi kuja kuwekeza pesa.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, akiwa katika Ifar iliyoandaliwa na klabu hiyo.

Kwenye biashara kitu cha muhimu na ambacho unaweza kukisema ni cha kwanza ni jinsi bidhaa yako inavyoonekana mbele ya jamii.

Thamani ya bidhaa yako, umbo la bidhaa yako ikoje ?, uso wa bidhaa yako yako ukoje ? Unavutia kuangaliwa na watu kwa ajili ya kuweka pesa kwenye bidhaa yako ?

Neno Simba au Yanga ni bidhaa, bidhaa ambayo wenye nayo hujivunia kuwa na mashabiki wengi kama mtaji, kitu ambacho ni kweli lakini kinaweza kikawa siyo sahihi kwa asilimia kubwa.

Kwanini nasema hivo ? , unaweza ukawa na mashabiki wengi sana ambao wakasimama kama mtaji wa kuwavutia wawekezaji waje kuwekeza lakini ukaiendesha klabu katika jicho ambalo siyo la kibiashara.

Kukawa hakuna utawala bora, hakuna uwekaji sahihi wa mapato ya klabu , kukawa na ufujaji wa pesa , na vitu vingine vingi.

Lakini kuna vitu kadhaa ambavyo ni vichache ambavyo huongeza thamani ya bidhaa ya klabu ambavyo haviangaliwi sana.

Timu ni moja ya bidhaa ndani ya klabu. Na timu ndiyo kiungo muhimu ambacho kinaweza kusababisha mtu aje awekeze pesa ndani ya klabu.

Timu ikifanya vizuri ndani ya uwanja inakuwa inauzika virahisi nje ya uwanja. Na mwekezaji siku zote hutazama namna ambavyo bidhaa inazungumzwa nje ya uwanja ambako ndiko kuna wanunuzi wengi.

Utoaji wa tunzo ndani ya klabu ni kitu kingine ambacho huongeza thamani kubwa sana kwenye bidhaa.

Bidhaa huonekana na thamani kubwa kwa kuweza kutoa tunzo za ndani ya klabu husika. Na mwekezaji siku zote hutazama kuwekeza sehemu ambayo ina thamani kubwa.

Hapa ndipo sehemu ambayo Simba imefanikiwa kuwatukana Yanga. Jana Yanga imetukanwa sana na Simba.

Imeoneshwa kuwa kwa sasa hawana wao Yanga hawana thamani kubwa ukilinganisha na wapinzani wao Simba.

Hili ni tusi kubwa sana , tusi ambalo Yanga wanatakiwa kukaa na kuona aibu na kutoruhusu tena kuendelea kutusiwa kila uchwao na Simba.

Wanatakiwa kuumizwa na matusi ya namna hii na kufikiria namna bora ya wao pia kuiongeza thamani bidhaa yao kwa manufaa ya wao binafsi.

Kwa manufaa ya wao kuendelea kuishi bila kulia lia kwenye dunia hii ya kibiashara, dunia ambayo unatakiwa kuongeza thamani bidhaa yako ili uendelee kuishi bila tatizo.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.