Sambaza....

Jana kulikuwa na mchezo wa ligi ya mabingwa barani Africa kati ya Simba na Nkana Red Devil ya Zambia.

Simba walifanikiwa kufuzu hatua ya makundi, lakini moja ya mashujaa walioibuka katika mchezo huo ni kiungo wa Simba, Chama.

Kipi kinampa ubora Chama ?

1: UWEZO WA KUCHEZA MIFUMO TOFAUTI.

Jana alifanikiwa kucheza ndani ya mifumo miwili ndani ya mchezo mmoja. Kipindi cha kwanza alicheza ndani ya mfumo wa 4-3-3, akiwa kiungo wa juu ya Jonas Mkude na James Kotei.

Lakini alipotoka Meddie Kagere , Simba walibadilisha mfumo na kucheza mfumo wa 4-4-2 ( iliyokuwa katika umbo la Diamond). Ambapo yeye na Hassan Dilunga walikuwa wanatokea pembeni kuingia katikati (mbele yao walikuwepo Emmanuel Okwi na John Bocco).

Baada ya Emmanuel Okwi kutoka na kuingia Shiza Kichuya, Simba walicheza mfumo wa 4-5-1 muda mwingi na ndiyo mfumo ambao ulimwezesha Chama kufunga goli la ushindi.

KUPIGA MASHUTI

Hii ni moja ya sifa moja wapo ambayo Chama anayo. Anauwezo mkubwa wa kufunga kwa mashuti, mfano kwenye mchezo dhidi ya Mbambane Swallows na mchezo dhidi ya Nkana Red Devil uliochezwa Zambia alifunga kwa shuti.

KUTOA PASI ZA MAGOLI.

Ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho za magoli. Ni kiungo mbunifu na anayetengeneza magoli ndani ya uwanja. Mfano hata mechi ya Jana alifanikiwa kutoa pasi moja ya mwisho ambapo Jonas Mkude alifunga.

KUFUNGA

Pamoja na kwamba ana uwezo wa kutoa pasi za mwisho za magoli lakini pia ana uwezo wa kufunga pia. Amefunga magoli manne mpaka sasa hivi katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Africa.

KUKABA

Moja ya sifa ambayo inampa nafasi kubwa ya kuwa ndani ya kikosi ni yeye kuwa mzuri hata kipindi ambacho timu haina mpira.

Mfano mechi ya Jana , Simba wamefanya (Hard-pressing) maeneo yote ya uwanja. Na moja ya watu ambao walikuwa wakipress kwa nguvu ni Chama.

UMILIKI WA MPIRA.

Chama ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira bila kupoteza na kuifanya timu kuendelea kuwepo ndani ya uwanja kwa muda mrefu.

KUSOMA MCHEZO (VISION).

Chama ana uwezo mkubwa wa kusoma mchezo pamoja na maono makubwa ndani ya uwanja. Mfano ana uwezo wa kusoma mchezaji yupi yuko kwenye nafasi sahihi na nzuri kwa ajili ya kumpa mpira.

KUTAMBUA & KUTUMIA UWAZI.

Hii ni sifa kubwa ambayo wengi wameshindwa kuwa nayo. Chama ana uwezo mkubwa wa kutambua UWAZI ndani ya uwanja na kutumia uwazi kwa manufaa ya timu.

Mfano goli ambalo alilifunga Jana, kakimbilia eneo ambalo kulikuwa na uwazi (spaces) na akapokea mpira ambao alikuwa na uwezo nao mkubwa kuufanya kuwa goli.

Sambaza....