Sambaza....


Amekuwa mchezaji muhimu sana kwenye kikosi cha Yanga msimu huu. Ndiye mpishi bora kwa sasa kwenye ligi kuu Tanzania bara.

Kinachonisikitisha sana siku hizi watu hawamuongei sana. Wamepunguza sana siyo kama zamani ambavyo walikuwa wanafanya.

Kipindi kile ambacho tuliwahi kuamini kuwa huyu ndiye biandamu pekee ambaye alishushwa na MUNGU.

MUNGU hakutumia muda wake kumuumba kwa udongo ambao alitumia kutuumba sisi , tuliamini alitumia udongo wa tofauti kabisa.

Udongo wa dhahabu, na asilimia kubwa ya udongo huo wa dhahabu uliwekwa kwenye miguu yake. Miguu yenye thamani kubwa sana.

Miguu ambayo ina kila aina ya muziki kwa ajili ya kutoa burudani. Ukitaka muziki wa Jazzy upo kwenye miguu ya Ibrahim Ajib.

Ukitaka Hip-Hop utasikiliza mashairi makali kupitia miguu ya Ibrahim Ajib mpaka kichwa kiume. Hata siku ambayo unajihisi kumwambia maneno matamu mpenzi wako basi unauwezo wa kusikiliza muziki mzuri wa RnB kupitia miguu ya Ibrahim Ajib.

Na ukafanikiwa kupata mistari mizuri kabisa ya kumwambia mpenzi wako na ukatengeneza tabasamu kwenye uso wake.

Huyu ndiye Ibrahim Ajib alishushwa kwa ajili ya kutoa burudani haswaa. Macho yetu yanajivunia kutazama miguu yake.

Ingawa hofu yetu miguu hii inaweza kuzeekea hapa hapa kwenye ligi yetu hii ambayo haina hata viwanja bora. Tuachane na hili maana kila siku tumepiga kelele sana.

Tumepiga kelele tukiamini kuwa Ibrahim Ajib hastahili kabisa kuendelea kuwepo kwenye ligi yetu ndiyo maana kila tumepiga kelele sana.

Turudi hapa ndugu zangu, kwa msimu huu Ibrahim Ajib amekuwa mchezaji muhimu sana ndani ya kikosi cha Yanga.

Najua dunia ya mpira siku zote humkumbuka mtu ambaye hufunga goli. Goli hukumbukwa siku zote kuliko hata yule aliyetengeza goli.

Hii ndiyo dunia ya mpira , huwezi kupingana nayo. Ndiyo dunia ambayo inaamini sanaa ya kufunga ni ngumu sana kuzidi sanaa yoyote uwanjani.

Ndiyo maana wafungaji wana thamani kubwa sana kuliko wengine. Hili halina ubishi, liko wazi kabisa. Hata kwa Yanga , Makambo kwa sasa ana thamani kubwa sana kuzidi Ibrahim Ajib.

Lakini hii haitoi uhalisia wa moja kwa moja kuwa Ibrahim Ajib kwa sasa ni mchezaji muhimu sana kwenye kikosi cha Yanga.

Ana pasi 13 za mwisho mpaka sasa kwenye ligi kuu ya Tanzania bara. Hii yote inaonesha ni jinsi gani ambavyo alivyo muhimu kwenye upatikanaji wa magoli.

Huyu ndiye uti wa mgongo wa magoli ya Yanga msimu huu kwenye ligi kuu ya Tanzania bara. Moja ya wachezaji ambao mpaka sasa hivi wameifanya Yanga iwepo pale na yeye yupo.

Tena jina lake liko juu kabisa kwenye orodha ya wachezaji muhimu kwenye klabu hiyo. Lakini tatizo linakuja hapa kila mwana Yanga anapomfikiria Ibrahim Ajib.

Mkataba wake unaisha mwishoni mwa msimu huu. Kila mwana Yanga akilitafakari hili nguvu humwiishia mwilini.

Kuna wakati hujiona kuwa wanaelekea kumpoteza mtu muhimu kwenye kikosi chao na ikizingatia kwa sasa klabu yao inapitia nyakati ngumu sana kiuchumi.

Watambakizaje?, kipi watakifanya ili Ibrahim Ajib aendelee kuvaa jezi ya njano na kijani?, ni swali ambalo mimi binafsi nimeona tayari Yanga wameshalitolea jibu.

Mwinyi Zahera anajua sana kucheza na akili. Kitendo cha Mwinyi Zahera kumpoka unahodha Kelvin Yondan na kumpa Ibrahim Ajib ni kitendo kikubwa sana kwenye harakati za Yanga kumshawishi Ibrahim Ajib kuendelea kubaki.

Hujajiuliza kuna wachezaji wangapi ambao sana sifa ya kiuongozi lakini hawajapewa?, ina maana Kamusoko hakuonekana kwenye jicho la Mwinyi Zahera.

Ajibu katika purukushani

Hapana shaka alionekana , ila Mwinyi Zahera alitazama kitu cha tofauti kwa Ibrahim Ajib. Alitaka kumfanya Ibrahim Ajib atambue yeye ni muhimu sana kwa sasa kwenye klabu ya Yanga.

Mwinyi Zahera ametaka kumuonesha ni kwa kiasi gani ambavyo Ibrahim Ajib wanavyomjali. Upendo ni kitu kikubwa sana kwa mwanadamu.

Mwinyi Zahera amempa upendo Ibrahim Ajib. Upendo ambao utamfanya aonekane ni mtu muhimu sana na anayependwa kwenye kikosi cha Yanga.

Hii itakuwa njia ya kwanza rahisi kumshawishi Ibrahim Ajib kusaini mkataba mpya tena mwishoni mwa msimu huu, ndiyo maana naona huu ndiyo usajili wa kwanza kwa Yanga kwa mwaka huu wa 2019.

Sambaza....