Sambaza....

Inawezekana mechi ya mwisho kuwakutanisha Uganda na Tanzania ikawa imewapa Uganda nguvu sana.

Walikuwa wababe wa Tanzania mbele ya mashabiki wao pale Nambole.

Leo hii wanakutana tena katika mechi ya kuwania kufuzu AFCON, ambapo katika mechi ya mwisho ya kuwania kufuzu Afcon kuwakutanisha Uganda na Tanzania ilifanyika mwaka 1984 na Tanzania kushinda goli 3-1 katika ardhi ya Uganda.

Leo hii tena wanakutana katika ardhi hii , ardhi ambayo iliwahi kumbeba nduli Idd Amin , Nduli ambaye aliwahi kuadhibiwa na majeshi ya Tanzania.

Hali ya vikosi ikoje ?

Kwenye timu zote hakuna mchezaji aliyeripotiwa kuwa na majeraha.

Maeneo gani muhimu katika mechi ya Leo ?

Kuna maeneo kadhaa ambayo yanaweza kuamua mechi ya Leo.

Je rekodi ya kocha wa sasa wa Uganda akiwa na timu ya taifa ya Uganda ina nafasi gani katika mchezo wa Leo ?

Tangu aichukue Uganda kutoka katika mikono ya Moses Basena na kucheza mechi yake ya kwanza tarehe 14 mwezi wa 1 mwaka 2018, kocha wa timu ya taifa ya Uganda mwalimu Desabre amefanikiwa kushinda mechi moja , kutoka sare michezo mitatu na kufungwa mechi nne katika mechi ambazo ameiongoza timu ya taifa.

Hii ni rekodi mbaya kwake kwa sababu inaonesha hajapata timu ya ushindi mpaka sasa hivi, hivo inaweza ikamfanya awe na mazingira magumu katika mechi ya leo kwa sababu timu yake imekuwa timu ya kuhangaika kutafuta ushindi.

Vipi kuhusu ujio mpya wa Emmanuel Amunike ? Unaweza kuwa na msaada mkubwa kwa upande wa Tanzania?

Ni mapema mno kumhukumu Emmanuel Amunike kwa matokeo yoyote yatakayotokea Leo. Ni mechi yake ya kwanza tena akiwa na wachezaji wapya kwa kipindi kifupi.

Ila kuna faida moja ambayo Taifa Stars wanaweza kuipata kutoka kwa Emmanuel Amunike.

Emmanuel Amunike anajua soka la Afrika, ana uzoefu nalo hivo anaweza kutumia uzoefu huo ili timu yake ipate matokeo.

Pia, Emmanuel Amunike ni mtu ambaye amecheza katika kiwango cha juu katika soka na timu kubwa duniani hivo anajua namna ya kuwafanya wachezaji wapigane kwa ajili ya kutafuta matokeo.

Ipi mbinu ya Desabre katika mechi kadhaa ambazo ameiongoza Uganda?

Mfaransa huyu amekuwa mhumini wa soka la kushambulia sana ndiyo maana amejaza wachezaji wengi ambao wana akili ya kushambulia zaidi, mfano William Luwagga Kizito, Moses Opondo, Faruku Miya, Emmanuel Okwi na Denis Nsibambi.

Kipi ambacho Taifa Stars wakifanye kulingana na mbinu hii ya mwalimu Desabre wa Uganda?

Moja ya madhaifu makubwa ya Taifa Stars ni jinsi wachezaji wanavyokuwa na makosa mengi binafsi kipindi ambacho timu inaposhambuliwa kwa presha ya juu. Hivo kipi kufanyike? Utulivu uwe mkubwa ndani yao, utulivu huleta umakini katika mchezo hivo ni ngumu kufanya makosa mengi binafsi.

Taifa Stars ina umbo kama la baunsa?

Hapana shaka hii sentensi ni sahihi kwa asilimia kubwa kwa sababu timu ya taifa ya Tanzania haina uwiano mzuri. Inawachezaji wengi bora katika eneo la kushambulia pekee.

Yani maeneo yatakuwa na ushindani mkubwa ndani ya uwanja?

Kuna maeneo matatu ambayo yatakuwa na ushindani mkubwa kutoka na aina ya wachezaji waliopo.

Eneo la kwanza ni kati ya Mshambuliaji wa Taifa Stars , Mbwana Ally Samatta na beki wa Uganda Muurishid Juuko. Mbwana Samatta ndiye mchezaji tishio katika mechi hii kutokana na kiwango chake ambacho amekionesha kwenye klabu yake ya KR Genk, hivo Waganda watakuwa wanamwangalia yeye muda wote kama mchezaji hatari na hivo watamkabidhi jukumu Juuko kwa ajili ya kumkaba.

Eneo la pili ni kati ya Khalid Aucho na Himid Mao.

Khalid Aucho ni moja ya kiungo mbunifu ndani ya kikosi cha Uganda, hivo ili kumfanya asitengeneze nafasi nyingi kwa washambuliaji wa Uganda inabidi Himid Mao awe anaharibu mipango yote inayoanzia kwa Khalid Aucho.

Eneo la tatu ni kati ya Abdi Banda na Emmanuel Okwi. Emmanuel Okwi anawajua vyema wachezaji wa Tanzania kwa sababu amecheza ligi ya Tanzania kwa muda mrefu, hivo atakuwa na nafasi kubwa ya kuanza katika mchezo wa leo. Mtu ambaye anategemewa kumchunga ili asilete madhara ni Abdi Banda.

MWISHO:

Uganda ndiye anayeongoza kundi hili akiwa na alama tatu, wakati Tanzania ana alama moja. Na, kwenye mechi hii Tanzania anaingia kama “Underdog’s”. Hii inaweza kuwa na faida na hasara kwao kutegemea na watakavyoichukulia mechi hii.

Mfano, wakikubali kuwa ni ” underdog’s ” watacheza kwa utulivu , utulivu ambao utawapa nafasi ya kuwa makini katika maamuzi yao.

Lakini wakiogopa kuwa wao ni underdog’s watacheza kwa hofu na kutokuwa makini katika maamuzi yao.

Uganda wataingia wakiwa wanajiamini kwenye mechi ya Leo, hivo kujiamini kwao kama watajiamini kwa kiwango kikubwa kutawafanya wasiwe na maamuzi yenye utulivu ndani yao na hii inaweza kuwa na faida kwa Tanzania.

Sambaza....