EPL

Wenger tazama muda umekuacha

Sambaza....

Miaka 21 imepita, miaka yenye rangi mbili ndani ya maisha ya Arsene Wenger ndani ya kikosi cha Arsenal.

Hapana shaka rangi nyeupe ilitanda katika ngozi ya mwili wake ndani ya miaka 10 ya kwanza.

Miaka ambayo alifanikiwa kupata mafanikio makubwa katika soka la England.

Mafanikio ambayo yalimpa heshima kubwa sana ambayo vizazi vingi vitaikumbuka.

Ndiyo miaka kumi ambayo alifanikiwa kupata kushinda makombe matatu pekee aliyonayo ya ligi kuu ya England, kombe ambalo kwa sasa linaonekana gumu kwake kushinda tena.

Hapana shaka nyakati hizi zenye majira ya ushindani na mapinduzi makubwa ndani ya mpira duniani hazitoi nafasi kwake yeye kushinda tena kombe hili.

Upinzani mkubwa umeongezeka, mapinduzi ya uwekezaji mkubwa wa timu mbalimbali ndani ya uwanja yanafanyika kwa kiasi kikubwa ndiyo maana siyo jambo la kushangaza Manchester City imetoka kwenye kisigino mpaka kichwani.

Mapinduzi ambayo yanaipa nafasi Chelsea kuwa timu ambayo ina mafanikio makubwa ndani ya miaka kumi iliyopita mbele ya Arsenal.

Mapinduzi haya hayaishii kwa kuyatazama katika matumizi makubwa pekee ya kununua wachezaji pekee, yanaenda mbele zaidi ya hapo. Unaweza ukanunua wachezaji kwa gharama kubwa lakini ukakosa kocha mwenye mbinu za kisasa zinazoendana na wakati huo.

Mbinu ambazo zitatumika ndani ya uwanja na nje ya uwanja kuwaongoza wachezaji wako.

Mbinu ambazo zitawafanya wachezaji wajiamini kila wanapoingia uwanjani.

Hii imekuwa tofaufi ndani ya kikosi cha Arsenal kwa sasa, wachezaji hawajiamini, hawajitumi kwa ajili ya timu.

Makosa mengi binafsi yamekuwa ndani yao, safu ya ulinzi imekuwa ikifanya makosa yale yale miaka nenda rudi.

Ile Arsenal iliyofanikiwa kumaliza ligi bila kufungwa ( Invincible) na kwenda mechi 49 bila kupoteza mchezo wowote ndani ya ligi kuu ya England haipo tena kwenye mikono ya Arsene Wenger.

Mikono ya Arsene Wenger imeshikilia Burnely iliyovaa vazi la Arsenal. Mikono ambayo imetapakaa rangi nyeusi.

Rangi nyeupe haipo tena kwenye ngozi ya mwili wake kama awali, giza limeshatanda katika maisha yake.

Hana uhakika wa kukimbia tena kwa sababu miguu yake haina nguvu, akili yake haifikirii kwa kiwango kikubwa kama ilivyokuwa awali.

Image result for Arsene Wenger

Uwezo wa kuiongoza tena Arsenal katika mafaniko ya hali ya juu umepungua , miaka kumi yake bora ya awali imeshapita.

Yuko ndani ya miaka kumi ambayo yuko kwenye chungu cha moto, miaka kumi ambayo inaweza kufuta heshima yake aliyofanikiwa kuiweka ndani ya miaka kumi iliyopita.

Historia haimbebi tena kipindi hiki kigumu anachopitia, Arsenal haiitaji kocha wa aina yake tena ili kushindana katika mashindano makubwa.

Damu mpya inahitajika kuinusuru Arsenal kipindi hiki kigumu walicho nacho.

Kipindi hiki Arsenal hamwihitaji tena Arsene Wenger kwa sababu kadri muda unavyozidi kwenda anatengeneza Arsenal dhaifu.

Arsenal ambayo tangu mwaka huu uanze imepoteza michezo saba na kuruhusu goli kwenye mechi kumi zilizopita.

Safu yake ya ulinzi siyo imara tena, haiwezi kulinda kibarua cha Arsenal Wenger. Safu ya ushambuliaji haina nguvu za kutetea kazi ya Arsene Wenger

Hata mbinu zake kwa sasa siyo silaha tena za kumlinda, hana silaha yoyote ya kujitetea kwa sasa. Silaha zake zimekosa makali tena.

Hawezi kuwepo kwenye vita ya kugombania nyama aliyenona.

Kitu pekee ambacho kinaweza kumpa heshima kubwa kwa sasa ni kukubali kuondoka kwa heshima kuliko kusubiri aondoke kwa aibu.

Image result for wenger emirates stadium

Amefanikiwa mengi pale Arsenal, yeye ndiye alikuwa msaada mkubwa kwa klabu kujiendesha kwa bajeti ndogo ili wajenge uwanja wa Emirates.

Uwanja ambao utakuwa kumbukumbu kwa vizazi vya Arsenal na jina lake litabaki kwenye hilo, ni bora akubali kwa sasa muda umemwacha na hana nguvu tena za kuukimbiza hivo anatakiwa kumwachia mtu mwenye mbio aukimbize kwa manufaa ya Arsenal.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x