Yusuph Mhilu (Kagera) akizidi kumtoka Makame (Yanga)
Ligi Kuu

YANGA wamrudishe nyumbani MHILU

Sambaza....

George Lwandamina , huyu ndiye mtu wa kwanza kuziamini njozi zake za usiku kwenye miguu ya Yusuph Mhilu. Kwa muda ule hakuwa na mtu wa kumwamini tena.

Obrey Chirwa aliamua kuisusia Yanga , akaona kilimo cha matikiti maji ni bora zaidi kuuza kipaji chake kwenye soko kubwa la Kariakoo.

Akaamua kwenda zake Zambia , akamwacha George Lwandamina akiwa hana cha kufanya. Ndicho kipindi ambacho ilikuwa ngumu kutambua mbele ya Yanga.

Ndicho kipindi ambacho furaha haikuwa sehemu ya maisha kwenye klabu ya Yanga. Miguu ya wachezaji ilikuwa haina furaha , akili zao zilikuwa zimejawa huzuni na matokeo yao yalikuwa yakusikitisha.

George Lwandamina alikimbiwa na watu muhimu kwa kipindi kile ndani ya Yanga . Kulia kwake hakukuwepo na Yusuph Manji tena ambaye ndiye alikuwa uti wa mgongo wa timu.

Kushoto kwake hawakuwepo viongozi timilifu wa Yanga. Wengi walijiuzuru, Yanga ikabaki inaendesha bila kufahamu inaendeshwaje. Hakukuwepo na mwenyekiti , wajumbe wa kamati tendaji wakawa wameisusa Yanga.

Obrey Chirwa hakumuonea huruma tena Mzambia mwenzake George Lwandamina akaamua kumkimbia na kwenda kulima matikiti nyumbani kwao Zambia.

Hata aliyewahi kuwa mshambuliaji wa hatari kwa wakati huo kwenye kikosi cha Yanga , Donald Ngoma alikuwa anamadhurio mazuri kwenye wodi kuliko uwanjani. Muda mwingi alikuwa anauguza majeraha ya goti lake.

Utafanya nini kama kocha kipindi ambacho washambuliaji unawategemea hawapo kwenye kikosi chako na ukigeuka kuangalia nyuma hakuna anayeweza kuziba nafasi zao ?

Ilihitaji njozi za usiku , njozi ambazo zilitakiwa kumuomba Mungu akuoneshe ni yupi mtu sahihi kwenye kikosi chako ambaye anaweza kusimama kama Goliati kwenye uwanja wa vita.

Picha ya Yusuph Mhilu ndiyo ilikuwa inatembea sana kwenye njozi za George Lwandamina. Imani yake aliiwekeza kwenye miguu ya Yusuph Mhilu.

Hatimaye akawa mshambuliaji ambaye alimsaidia sana George Lwandamina , alifunga akitokea pembeni , huu ndiyo ulikuwa utamaduni wa Yanga. Kabla yake alikuwepo Simoni Msuva na Mrisho Ngassa.

Hawa ni aina ya wachezaji ambao walikuwa wanafunga kwa kutokea pembeni , aina ya mchezo wa Yanga. George Lwandamina aliona hiki kwake akamwamini , tuliamini kuwa huyu atakuwa hazina ya Yanga.

Kwa bahati Mbaya hakuaminika kwenye kikosi cha Yanga. Kagera Sugar wakamwamini , wakampa nafasi , nafasi ambayo anaitumia kuwaangamiza wapinzani wakimemo Yanga. Adhabu kwa Yanga ni kuwakumbusha kuwa alikuwa mtu sahihi kwenye kikosi cha Yanga.ĺ


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.