Ligi Kuu

Yanga wanashindana na Manara, Simba inashindana na ligi Ligi.

Sambaza....

Kuna uongo unaoaminishwa kuwa ni ukweli , uongo ulioenea sana. Uongo uliojipenyeza katikati ya masikio ya watu, kwa bahati mbaya ukaingia kwenye akili za walio wengi.

Na kwa bahati mbaya zaidi uongo huo unaonekana ndiyo ukweli. Unaonekana ndiyo suluhisho kwa kila kitu ambacho wao wanakiamini ili kutibu tatizo lao.

Yanga wanaamini wana tatizo moja tu. Hawana Haji Manara wao. Hapa ndipo wanapoanza kujidanganya na kujiaminisha huu uongo unaoonekana ni ukweli.

Uongo ambao unatetewa kwa nguvu zote kabisa. Ni kawaida kwa mwana Yanga kumkuta sehemu akinyanyua kinywa chake na kusema kuwa hatuna Haji Manara kwetu.

Na kuna wengine wanatumia muda wao mwingi kutolea mfano kipindi cha Jerry Muro. Kipindi ambacho wanaamini Jerry Muro alikuwa amefunika nyota ya Haji Manara kwa shuka jeusi.

Hakupata nafasi hata ya yeye Haji Manara kung’ara mbele ya Jerry Muro. Wanakikumbuka sana hiki kipindi, kipindi ambacho wao wanaamini Jerry Muro aliwafanya wawe jasiri.

Aliwafanya wawe mashabiki ambao siyo wanyonge, kwao wao kuziweka mbavu nje, huku wakiwa wametanua makwapa yao na vifua vyao vikiwa vimetuna mbele lilikuwa jambo la kawaida sana kwao.

Yote haya ni kwa sababu ya Jerry Muro. Hiki ndicho wanachokiamini mpaka sasa. Huwaambii kitu kuhusu hiki kitu. Wao wanaamini kabisa viwanja havijai kwa sababu hawana Jerry Muro na hawana Haji Manara wao.

Wao wanaamini timu haifanyi vizuri kwa sababu tu hakuna hamasa inayotaka kwenye vinywa kama vya Jerry Muro na Haji Manara.

Huu ni uongo usioonekana na unalazimishwa kufutwa vumbi ili uonekane ni ukweli. Wamesahau vingi sana mpaka sasa hivi. Wamesahau mdomo wa Jerry Muro ulikuwa unanyanyuliwa na pesa za Yusuph Manji.

Pesa ambazo zilikuwa zinaleta ushindi ndani ya Yanga. Ushindi ambao ulikuwa unafanya mashabiki waje uwanjani. Hiki kitu hakipo tena Ila kimehamia kwa Simba.

Simba wanapesa za Mohammed Dewji, pesa ambazo zinafanya kunyanyua mdomo wa Manara. Mdomo ambao kwa kipindi cha Jerry Muro kilikuwa hakina uwezo wa kunyanyuka kwa sababu tu hawakuwa na Mohammed Dewji.

Hawakuwa na matokeo chanya uwanjani . Matokeo ambayo kwa kipindi hicho mashabiki wa Simba walikuwa hawaendi uwanjani kwa wingi kwa sababu ya matokeo mabovu.

Hiki ndicho kinachowakuta Yanga. Wanamatokeo mabovu . Hawamkosi Haji Manara au Jerry Muro , wanakosa matokeo bora ya kuleta hamasa ya kwenda uwanjani.

Leo hii Yanga inahangaika kuunda kamati za hamasa huku wakiwaza Haji Manara kama mtu anayeleta hamasa kitu ambacho siyo kweli. Wanamuwaza sana Manara kuliko kuwaza kupata matokeo mazuri kama ambavyo Simba wanavyoshindania kombe la ligi kuu kwa sasa.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.