Ukiachana na Marc Wilmots, Paul Van Himst, Benard Voorhoof anayefuata sio Edin Hazard wa Chelsea bali ni mtu mwenye miraba minne, anamiliki uzito wa kilo 94, na urefu wa 1.9m sawa na futi 6 na inchi 3, tangu mwaka 2010 hadi leo ameifungia timu yake ya taifa magoli 45 katika mechi 79 alizocheza na kuwa mfungaji bora wa muda wote.
Gharama za uhamisho wake kutoka Everton mwaka 2017 zilikuwa ni Euro milioni 85. Ukiachana na Neymar, Ronaldo, Mbappe na yeye yupo 10 bora kwa gharama kubwa za usajili. Huyu ndie Romelu Menama Lukaku Bolingoli.
Amechezea vilabu vingi kabla ya kutua Old Traford. Alishawahi kukiwasha na Chelsea miaka ya 2011-2014 lakini mwaka 2012 akiwa Chelsea alipelekwa kwa mkopo West Bromwich Albion, akicheza mechi 35 akifunga magoli 17, kisha akapelekwa kwa mkopo Everton mwaka 2013 kabla ya kununuliwa jumla jumla mwaka 2014-2017 na hapo ndipo ufalme wa Lukaku ukaonekana.