Denis Nkane na Kibwana Shomari wakiwa na medali zao za mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika
Tahariri

Achana na Matokeo Yanga na Simba Zimefanikiwa Afrika

Sambaza....

Kuna manadiliko makubwa katika soka letu. Kwangu Simba na Yanga zimefanikiwa sana msimu huu. Matokeo sio kitu cha kukijadili sana kulinganisha na huko tulikotoka.

Tujadili direction ya tulikotoka, tuliko na tunakopaswa kwenda. Tuko kwenye barabara nzuri. Tupashikilie tu hapa tulipopashika. Zamani timu zetu zikienda kucheza na timu za Kaskazini kuanzia AirPort, mitaani hadi hotelini timu inaonyeshwa ishara ya kufungwa 5 na kiwanjani kweli tulikuwa tunafungwa Idadi ya mabao hiyo. Ilikuwa kawaida tu. Lakini sasa mambo yamebadilika.

Timu za Kaskazini hazina raha kucheza dhidi yetu. Nadhani tumeona ilichokifanya Simba majuma kadhaa yaliyopita pale Morroco. Pia tumewaona Yanga walichokifanya jana usiku pale Algeria. Kuanzia pale Morroco hadi Algeria, timu zetu zifurahie kwa tunachokiona sasa na zisiumizwe na matokeo. Kushinda Kombe la Klabu Bingwa Afrika. Kushinda na Kombe la Shirikisho ni suala la mchakato. Haushindi tu.

Nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto akivaa medali ya mshindi wa pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu zetu kwa sasa ziko kwenye huo mchakato. Ilikuwa ngumu tuibuke ghafla kusikojulikana kisha tushinde makombe haya, bila kupitia njia hizi tunazopitia sasa. Ilikuwa ngumu. Ngumu mno. Hivi sasa tuko katika uelekeo mzuri. Watu hawapaswi kujisikia unyonge. Wanapaswa kufurahia kwa kukumbuka tulipotoka.

Soka letu limefanikiwa sana, shida ni moja tunayapima mafanikio yetu kwa kuwatazama waliofanikiwa zaidi, kisha hawakai katika kanda yetu. Lakini tutoke hapa tuwatazame Waganda, Wakenya, Waburundi. Timu za wenzetu ziko hoi ICU, zinapumulia mashine, kwetu kuingia Robo na Nusu hadi Fainali ni jambo ka kawaida, inakuwaje tuwe hatujafanikiwa?

Jamani tumefanikiwa sana.

Sambaza....