EPL

Alaumiwe Sanchez au Arsenal?

Sambaza....

Hatimaye Alexis Sanchez siyo mchezaji tena wa Arsenal, ni habari isiyofurahisha kwa mashabiki wa Arsenal lakini ndiyo ukweli wenyewe. Haijalishi unaumiza kiasi gani lakini unatakiwa kukubaliana nao.

Kuondokewa na mchezaji muhimu katika kikosi chako. Mchezaji ambaye alikuja kuimarika zaidi katika kikosi chako lakini akakuacha na maumivu.

Siyo mara ya kwanza kwa Arsenal kuachwa na wachezaji nyota hasa hasa katika utawala wa Arsene Wenger. Wengi waliondoka tena waliokuwa wanaonekana muhimu sana ndani ya kikosi.

Kikosi cha Arsenal kiliyumba eneo la kiungo alipoondoka Patrick Vieira, hakukuwepo mtu wa kuziba nafasi yake kwa wakati huo lakini aliwaacha Arsenal.

Huzuni iliwajaa mashabiki wa Arsenal. Kabla hata kidonda chao cha kuondokewa na Patrick Vieira hakijapona, mshambuliaji wao Thierry Henry aliwaacha pia.

Mfungaji bora wa muda wote wa timu, moja ya vipaji vikubwa kuwahi kutokea katika ligi kuu ya England.

Kipaji ambacho kiligeuka kuwa kipenzi kwa wapendasoka duniani hasa hasa mashabiki wa Arsenal.

Lakini aliwaacha, tena kipindi ambacho timu inafanya mabadiliko nje ya uwanja kwa kuhama wa uwanja wa Highbury na kuhamia uwanja wa Emirates.

Kilikuwa kidonda kikubwa sana, kilichukua muda mrefu kupona, wakati kinaelekea kupona kilitoneshwa tena , safari hii Cesc Fabregas ilikuwa zamu yake kuondoka.

Mashabiki waliumia, nyota mwingine akiwaacha tena kipindi ambacho walikuwa wanampenda na kikosi cha Arsenal kilikuwa kinamwihitaji, lakini Fabregas hakujali hilo mpaka akajiongezea pesa kwa ajili ya kujinunua.

Iliwaumiza wengi, wakiwa wanajiuliza tatizo nini , Samir Nasri akaondoka, Sagna akaondoka , Alex Song akaondoka , Clichy naye akaondoka.

Kikosi kikayumba kwa sababu asilimia kubwa ya wachezaji walioondoka ndiyo walikuwa muhimu kwenye kikosi cha kwanza.

Wakabaki na Robin Van Persie kama mchezaji.muhimu kwa wakati huo.

Robin Van Persie aliwaambia Arsenal wasajili wachezaji nyota kwa ajili ya kushindana na makombe makubwa kama ligi kuu na klabu bingwa barani ulaya.

Lakini klabu hakimsikiliza akaondoka na kwenda katika timu ya Manchester United , sehemu ambayo aliamini kuna wachezaji ambao wanauwezo wa kushindania makombe makubwa.

Alipofika Manchester United alichukua kombe la ligi kuu ya England huku Arsenal wakibaki kumpigia makofi ya kumpongeza.

Sababu ni moja tu inayowatoa wachezaji nyota pale Arsenal , nayo ni timu kuwa na kikosi ambacho hakina uwezo wa kushindania makombe makubwa.

Dunia ya sasa wachezaji wengi wanawaza vitu viwili, sehemu ambayo wanaweza kupata makombe makubwa na sehemu ambayo wanaweza kulipwa vizuri.

Vitu vyote hivo kwa Arsenal hakuna, hakuna timu ya kushindana kwa ajili ya makombe makubwa na kulipa mishahara ambayo kwa sasa wachezaji wengi hutamani kupata.

Vyote hivo havipo kwa kiasi kikubwa katika timu ya Arsenal. Wachezaji hupigana kwa ajili ya timu ili ifanikiwe lakini timu huwaangusha.

Leo hii watu wengi wanamlaumu Sanchez lakini hawakumbuki alama aliyoiweka katika timu ya Arsenal.

Hawakumbuki goli alilofunga katika nusu fainali ya FA 2015 dhidi ya Reading, hawakumbuki goli alilofunga mwaka huo huo kwenye fainali ya FA dhidi ya Aston Villa.

Hawawezi pia kukumbuka goli alilofunga kwenye nusu fainali ya FA dhidi ya Manchester City lililowapeleka fainali ya FA. Sanchez muda wote alijituma kwa ajili ya timu. Alihakikisha anatumia uwezo wake timu yake ikipata mafanikio.

Magoli 80 ndani ya timu ni kielelezo tosha kuwa Sanchez alikuwepo pale kwa ajili ya kuhakikisha Arsenal inafanikiwa.

Lakini ilikuwa tofauti na kwa Arsenal. Timu ilikuwa haina mpango wa kununua wachezaji wa kariba ya Sanchez. Wachezaji ambao watakuwa na uwezo wa kupigania makombe makubwa.

Image result for sanchez

Ndiyo maana mpaka timu ilishindwa kufuzu klabu bingwa barani ulaya msimu huu.

Ni mchezaji gani mkubwa ambaye atafurahia kukaa na kuona hayupo kwenye mashindano makubwa kama ya klabu bingwa barani ulaya ( UEFA)?

Jibu ni hapana, kama jibu ni hapana basi haina haja ya kumlaumu Sanchez kuondoka na kwenda sehemu ambayo anaiona anaweza akapata kitu kikubwa.

Cha muhimu Arsenal wanatakiwa kuifanya timu yao iwe timu ambayo mchezaji yoyote mkubwa atamani kucheza katika timu yao

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x