Sambaza....

Hatajwi lakini yupo, haonekani lakini ana asilimia kubwa za ushindi kwa klabu yake, ana kaba njia zote za ushambuliaji kwa timu pinzani, anapandisha mashambulizi, asipokuwepo yeye timu huzidiwa sehemu ya kati,yeye ndiye roho ya timu kwa sasa.

Alizaliwa miaka 25 iliyopita, kule nchini Ghana katika mji wa Accra, ana urefu wa mita 1,80  sawa na futi 5 na inchi 11, ni kiraka anayeimudu nafasi ya kiungo na beki ya kati akivalia uzi namba 3, mkataba wake unamalizika june 30 mwaka huu.

Kabla ya kuja Tanzania alichezea timu mbalimbali , timu hizo ni timu ya Corner Babies mwaka 2002-2007, Golden Foot Academy mwaka 2007-2009, Liberty Professionals mwaka 2010-2014 akicheza mechi 65 akiifungia magoli matatu pekee, kisha akaenda kwa mkopo  BA Stars mwaka 2014-2015 akicheza mechi  25 akifunga goli 1, mwaka 2015-2016  aliichezea  Al-Oroubah mechi 8 pekee kabla ya kujiunga na Mnyama mwaka 2016. Je ni nani huyoo…..?

James Agyekum Kotei, baada ya kutua Msimbazi ilimuwia vigumu kupata namba moja kwa moja, nyota yake ikaanza kung’ara chini ya kocha Mkameruni Joseph Omog, akichezeshwa kama mbadala wa Jonas Mkude.

James Kotei na Mohamed Hussein.

Mechi ambayo Kotei huenda haji kuisahau ni ile ya fainali ya kombe la Azam mwaka 2017, iliyochezewa pale makao makuu, Jamuhuri Dodoma dhidi ya Mbao FC na kuishuhudia Simba ikiibuka na ushindi wa goli 2-1, Shiza Kichuya akifunga goli la penati dakika za lala salama. Katika mchezo huo Kotei ndiye aliyekuwa mchezaji bora “man of the match”, kiukweli aliupiga mwingi hadi aliboa.

Ilimchukua muda kwa Mghana huyu kuchukua namba jumla jumla kutoka kwa Jonas Mkude ambaye tayari alikwisha waaminisha Watanzania kuwa yeye ndie kiungo wa chini aliye mahiri zaidi. Kocha Omog ndiye aliyemfanya Kotei aonekane kwani alianza kumpiga benchi mchezaji mwandamizi, Mkude na kumpa namba Kotei.

Faida iliyokuwa ikionekana kwa Kotei kipindi kile dhidi ya Mkude ni uwezo wa kupiga pasi za mbele (forward passes) na uharaka akiwa na mpira. Ikiwa ni tofauti na mkude ambaye alikuwa anapiga pasi za nyuma ( back passes) na kukaa na mpira muda mrefu yaani yuko “Slow”.

Baada ya Omog kuachana na Simba SC kocha mpya Pierre Lechantre alitafuta njia nzuri ya kuwachezesha wote yaani Kotei na Mkude, hapo ndipo majukumu ya Kotei na Mkude yakaanza kutofautiana uwanjani. Kwani wakicheza pamoja, utabaini kuwa wote wanachezea chini lakini Mkude akiwa juu kidogo ya Kotei, na kubadilishana udhibiti wa maeneo, yaani mwingine akiwa kulia na mwingine anakuwa kushoto.

Hadi sasa, anayechukua sifa za kiungo wa chini, mkabaji ni Kotei na Si mkude. Kotei ndiye mlinzi halisi wa safu ya walinzi wanne. Mpira ukipotelea kwa Clatus Chama, mtu wa pili kumkuta ni Jonas Mkude, kabla haujamfikia Paschal Wawa, lazima umpite kwanza Kotei, hapo ndio ile maana ya Mkude kuwa kiungo wa kati (central midfielder)inapotokea, yaani Mkude humiliki eneo la kati, kati ya Chama (attacking midfielder)  na Kotei (down/holding midfielder).

 James Kotei  ana sifa kuu tano, kuzielewa lazima uwe umemuangalia katika michezo mingi ya ligi, kimataifa, kirafiki na mashindano mbalimbali.

Kwanza, Kotei ni mzuri kuisoma “mikimbio” ya washambuliaji wakati timu ikiwa haina mpira. Kibarua hiki kinamfanya awe kiungo bora kwa sasa, kwani akishaisoma mikimbio yao ni rahisi kwake kuzuia pasi isipigwe kwenye eneo lenye mshambuliaji hatari na kumpa nafasi ya kufunga.

Usomaji huu unamfanya Kotei kubaini mapengo ya mabeki na kuyaziba. Ni zaidi ya mara mbili kwa kotei kuokoa mipira inayotaka kuingia golini, huku golikipa na mabeki wakiwa wameshapitwa. Mechi dhidi ya Mbao kule Dodoma, JKT Tanzania, Mkwakwani Tanga, KMKM Zanzibar  na Mbao Mwanza alifanya hicho kitu. Huwezi kufanya kama Kotei kama haupo mchezoni (Game concentration).

Pili, Kotei ni mzuri kukaba kwa kutokea nyuma (blind side defending). Ni kawaida kwa James Kotei kuunasa mpira kutoka kwa adui akimkaba kwa kutokea nyuma. Kuna wakati mchezaji wa kariba ya Kotei unatakiwa kukimbia bila kutoa kishindo lengo ni kumvamia na kumpokonya mpira adui aliyekupa kisogo.

Wachezaji wa Simba SC, Jonas Mkude, John Boko na Hassan Dilunga,

Sifa hii ya Kotei pia anayo Mkude, ambaye hutumia nguvu zake za miguuni kuuficha mpira baada ya kumpa msuli adui. Kwa kule Ulaya bila shaka N’Golo Kante, Sergio Busquet, na Casemiro wanazijua kazi hizi kwa usahihi mkubwa.

Tatu, kuingilia mchezo yaani kufanya “Interception”. Ni ngumu kufanya Interception kama huna uwezo wa kuusoma mchezo na mikimbio ya wachezaji wa timu pinzani. Kotei kama kiungo mkabaji anaziba zaidi maeneo hatari ya kupitisha pasi za mwisho, wakati mwingine hufanikiwa kuzinasa pasi hizo zikielekea eneo hatari zaidi.

Kotei ni mtibuaji wa malengo ya timu pinzani, kwa kuzizuia pasi zao zenye madhara kwa Simba. Kazi hii ya kuzuia pasi  mpenyezo “penetration pass” husaidiana kwa ukaribu na Jonas Mkude.

Nne, kupiga pasi ndefu. Kilichokuwa kinamuweka benchi mkude kipindi cha Omog ndicho anachokifanya Kotei yaani kupiga pasi ndefu kwenda mbele.  Akiona kuna nafasi upande wa winga ya kulia au kushoto na katikati hupiga pasi ndefu kumfikia mchezaji anayemtaka. Kwa sasa pasi kama hizi sio nyingi kwa kotei kutokana na aina ya kikosi kilichopo. Mkude aliusoma mchezo na kubaini makosa yake na sasa ni miongoni mwa wachezaji wanaopiga pasi ndefu, pia Paschal Wawa naye ana uwezo mkubwa wa kufanya hivyo.

Sergie Paschal Wawa akikokota mpira katika mechi dhidi ya JS Saoura uwanja wa Taifa.

Pasi ndefu hupigwa kutokea nyuma kama eneo la kati la wapinzani kuna utitiri wa watu, kwahiyo njia nyepesi huwa ni kupiga pasi ndefu. Kwa pale Real Madrid bila shaka nikimtaja Tone Kroos au N’Golo Kante naamini utanielewa vizuri.


N’Golo Kante, kiungo wa Chelsea ya Uingereza. Alifanya kazi kubwa wakati wa kocha Antonio Conte darajani na kuisaidia Chelsea kubeba kombe la EPL msimu 2016/2017.

Tano ni kupiga pasi fupi fupi za kwenda mbele.  Simba ya Patrick Winand J. Aussems  yenye falsafa ya kumiliki mpira na kucheza kwa burudani inamfanya James Kotei naye kuwa mzuri zaidi kwa kupiga pasi fupi za mbele. Kwa lugha ya mtaani tunasema “anagusa”. Aina hii ya uchezaji ya Kotei huwa hasa baada ya timu pinzani kuziba mianya ya pasi mpenyezo, na badala yake pasi hizi hupigwa ili kuwasogeza maadui eneo la Simba ili kuweza kupenyeza mipira kuelekea eneo hatari la mpinzani.

Mechi dhidi ya JS Saoura ilidhihirisha ninachokisema hapa. Saoura walipaki basi, ikabidi Simba waanze kuwaita taratibu katika eneo lao ili wapungue katika eneo lao la ulinzi. Kwa kumiliki mpira kwa pasi fupi fupi kuliifanya Simba itoke na ushindi dhidi ya Mwarabu.

Mwisho kabisa Kotei ni mzuri kwa kuzuia mipira kwa kutumia nguvu, kwa kupiga “tackle “ za nguvu. Mara nyingi “tackling” zake hufanikiwa. Aina ya viungo kama Kotei kote duniani huwa na asili ya “undava” hukaba kwa kutumia nguvu, hutumia mwili, miguu na mikono kuupoka mpira kutoka kwa mpinzani. Kupata kadi za njano na nyekundu kwao ni kawaida.

Asipokuwepo yeye, eneo lote la kiungo huzidiwa katika kuhimili mashambulizi ya timu pinzani. Akiwepo yeye huongeza “Pressure” kwa washambuliaji wa timu pinzani wakati timu ikiwa haina mpira.

Ni vigumu sana, kumpita Kotei ”man to man” yuko tayari wewe uende lakini mpira ubaki kwa njia yoyote ile. Ana sifa zote za kuwa kiungo mkabaji wa chini ndio maana hadi sasa ameichezea Simba mechi 60 za ligi na kuifungia goli 1  pekee tena dhidi ya Mbao katika sare ya 2-2 kule mkoani Mwanza, hii ni kwa sababu muda mwingi ana hakikisha safu yake ya ulinzi inakuwa salama (defending defenders).

Hadi leo, Jonas Mkude akicheza peke yake katika eneo la chini huwa anakosa ladha hadi pembeni yake awepo James Kotei. Mechi ya kombe la mapinduzi dhidi ya Mlandege ilidhihirisha hiki. Kotei anamrahisishia Mkude kazi ya kupandisha mashambulizi kwa kumiliki eneo la kati.

Kikosi cha Simba katika dua ya pamoja baada ya mazoezi. inaaminika kuwa James Kotei ndiye mchezaji anayeongoza dua zote kabla na baada ya mazoezi na mechi.

Taarifa kutoka ndani ya Msimbazi zinadai kuwa Mghana huyu hutumika kuomba dua wakati wote timu inapohitaji kufanya hivyo, yaani wakati wa kuanza mazoezi , wakati wa kumaliza mazoezi na wakati wa kuanza mechi. Kotei ni muhimili wa Simba kiimani na uwanjani.

Sambaza....