Sambaza....

Kikosi cha Azam kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam Alhamis ya Disemba 27 kuelekea mkoani Morogoro ambapo watakuwa na mchezo wa ligi kwenye uwanja wa Manungu Complex kuumana na WanaTamTam Mtibwa Sugar.

Afisa Habari wa Azam Jaffary Idd Maganga ameuambia mtandao huu kuwa kikosi kipo katika hali nzuri na kwamba maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yameanza mara tu baada ya kutoka kuwafunga Madini FC mabao 2-0 katika michuano ya Azam Sports Federation Cup.

“Kikosi kwa kweli kipo vizuri, hatuna majeruhi kwa sasa lakini pia tumeongeza wachezaji wawili akiwemo mshambuliaji Obrey Chirwa kutoka Zambia na kiungo mshambuliaji Mpondo Stephano kutoka Cameroon, pia mchezaji Frank Domayo ameanza mazoezi mepesi kabla ya kuanza yale ya Uwanjani baada ya majeraha ya muda mrefu hivyo tunazidi kuimarika,” amesema.

“Tunajua Mtibwa ni timu ngumu na hivi majuzi wametoka kwenye michuano ya Kimataifa lakini bahati mbaya wametolewa, tunajua watakuja wakitaka kushinda mchezo huo lakini hata rekodi zinaonesha sisi tunamatokeo mazuri kwenye uwanja wao, hivyo tumejipanga vizuri, ukizingatia sisi ni miongoni mwa timu mbili ambazo hazijapoteza michezo yake hadi sasa,” ameongeza.

Rekodi zinaonesha katika michezo mitano iliyopita ya ligi, Mtibwa Sugar haijawahi kuifunga Azam, wakitoka sare katika michezo minne na mmoja Azam akishinda na hiyo ilikuwa kwenye uwanja wa Manungu Complex April 2016.

Sambaza....