Mchezo wa mwisho wa Simba Kimataifa
ASFC

Baada ya Kipigo Katika FA Hii Hapa Rekodi Mbovu Yakupoteza Iliyowekwa na Simba

Sambaza....

Wekundu wa Msimbazi Simba jana walipoteza mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la FA mbele ya Azam Fc na hivyo kuwafanya kucheza michezo mitatu mfululizo bila kupata ushindi msimu huu.

Sasa Simba imekwenda mechi tatu mfululizo bila kupata ushindi wakifungwa mara mbili na kutoka sare moja katika michezo ya michuano yote waliyoshiriki msimu huu huku wakitolewa katika michuano miwili.

Mara ya mwisho Simba kupata ushindi ilikua ni katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad April 22 ambapo walishinda bao moja kwa sifuri katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Baada ya hapo Simba imeambulia vipigo viwili na sare moja.

Wachezaji wa Simba wakati wa upigani mikwaju ya penati katika mchezo dhidi ya Wydad Casablanca

Simba ilianza kupoteza kwa bao moja bila April 28 katika Ligi ya Mabingwa dhidi ya Wydad ambapo walifungwa bao moja bila katika dakika 90 za mchezo. Matokeo yale yalikua ni mema kwao kwani ilikua ni sare lakini baada ya dakika 90 bado kwenye matuta walishindwa kufurukuta na hivyo kuondoshwa katika Ligi ya Mabingwa.

May 3 tena Simba walishuka dimbani dhidi ya Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC na kupata sare ya bao moja kwa moja na hivyo kufifisha kabisa matumaini yakumfikia Yanga aliyepo kileleni na hivyo kupoteza taji lingine msimu huu.

Na kipigo cha mwisho ni dhidi ya Azam Fc katika nusu fainali ambapo Simba walipoteza kwa mabao mawili kwa moja  na hivyo kuondoshwa kwenye kombe hilo na kuifanya Simba kutoka tena patupu msimu huu bila kombe lolote.

Simba Sc

Kwa matokeo hayo ya michezo mitatu ya mwisho ya Simba ni kama imeamua hatma ya Simba msimu huu kwani ni wazi sasa Wanamsimbazi hao wanamaliza msimu bila kupata ubingwa wowote maana tumaini pekee lilibaki katika Kombe la FA. 

Ni wazi sasa uongozi wa Simba ukae chini na ujitathmini ni wapi wamekosea msimu huu na kuanza kuweka mipango madhubuti kuelekea msimu ujao wa Ligi za ndani lakini pia katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Sambaza....