Ligi Kuu

Bado Ngassa ana ndoto ya kucheza Soka la kulipwa !

Sambaza kwa marafiki....

Unaweza ukaona ni kama utani, tena utani wa ngumu lakini huu ndiyo ukweli ambao unatoka kwenye kinywa cha Mrisho Ngassa. Kijana ambaye aliwahi kuwa mfano wa vijana wengi kipindi cha nyuma kutokana na kipaji chake kikubwa cha kucheza mpira.

Na wengi wanaamini kwa miaka hii ya kuanzia 2006 , Tanzania haijawahi kupata mchezaji mwenye kipaji kikubwa kama Mrisho Ngassa. Na wengi wanaamini kitu pekee ambacho kimemwangusha Mrisho Ngassa mpaka Leo hayupo sehemu ambayo Mbwana Samatta hayupo ni kukosa wasimamizi.

Hakuwa na wasimamizi sahihi wa kipaji chake, wasimamizi ambao wangemshauri namna gani ya yeye kuwa mchezaji wa kimataifa.

Wasimamizi ambao wangesimama kidete kuhakikisha Mrisho Ngassa anakuwa mchezaji wa kulipwa katika nchi mbalimbali za ulaya.

Wasimamizi ambao wangemkumbusha muda sahihi wa mazoezi yake binafsi na mazoezi ya timu, na kumkumbusha umuhimu wa juhudi katika mazoezi.

Wasimamizi ambao wangemkumbusha umuhimu wa kuwa na nidhamu ya kupumzika kwa ajili ya mwili wake. Muda sahihi wa kupumzika baada ya kutoka mazoezini.

Na kuachana na tabia ya kushinda kwenye sehemu za starehe kwa ajili ya kufanya starehe ambazo hazina afya kwa kipaji chake.

Wasimamizi ambao wangemkumbusha kutobweteka na sifa ambazo alikuwa anazipata kutoka kwa mashabiki wa ligi yetu, na kumkumbusha safari ambayo anatakiwa kusafiri.

Hakuwa ana aina hii ya watu, alikuwa amezungukwa na watu wengi ambao hawakuwa na msaada mkubwa sana kwa kipaji chake.

Kiasi kwamba mpaka muda huu Mrisho Ngassa hakucheza katika hali ya soka la ushindani kama ambavyo kiwango chake kilivyo.

Hakufanikiwa kupata nafasi ya kucheza ligi kubwa barani ulaya ingawa alifanikiwa kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Westham.

Nahisi hiki ndicho kinachomuumiza sana Mrisho Ngassa. Wakati akiwa kwenye kiwango kikubwa hakufanikiwa kucheza katika ligi kubwa ulaya.

Muda huu umeenda sana kwa Mrisho Ngassa. Kipaji chake kimeshaenda kupumzika kwa bahati mbaya yeye ajili yake ndiyo inaamka kipindi hiki.

Anataka sasa kuwa mchezaji wa kulipwa kipindi ambacho wengi wanaona haiwezekani ila yeye anaamini inawezekana kabisa!.

Ni kitu kikubwa sana chenye ushujaa. Baada ya mechi dhidi ya Mbao FC, kinywa chake kilitamka matamanio yake ya kucheza Ulaya tena kwa mara nyingine, natamani sana afanikiwe ila ningefurahia hii kauli angeitoa kipindi kile Mrisho Ngassa yuko hai.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.