Kocha mkuu wa Klabu ya Simba
Kocha mkuu wa Klabu ya Simba
Mabingwa Afrika

“Game plan” ya Aussems ilikuwa sahihi, lakini tatizo lilikuwa hapa…!

Sambaza....

Ni raundi ya pili tu katika mzunguuko wa raundi 6 katika kundi D klabu bingwa barani Afrika, Mnyama anakubali kichapo cha goli 5-0 mbele ya AS Club Vita kutoka Congo, Kinshasa.

Kichapo hicho, kimeonekana kuwashangaza wengi na pengine wengine wameshaanza kuikatia tamaa klabu ya Simba katika michuano hiyo, hasa katika kundi lake ambalo lina wababe kama Al ahly ya Misri.

Kushangaa kipigo cha goli 5, ni kukosa uzoefu katika masuala ya Soka, yaani namaanisha anayeshangaa Simba kufungwa goli tano na timu kama Vita basi atakuwa haujui mchezo wa mpira na maajabu yake.

Baadhi ya wachezaji wa Simba, katika mchezo wao dhidi ya AS Club Vita, klabu bingwa Afrika.

Mpira ni sayansi, hii inamaanisha kuwa, ili timu ipate matokeo lazima ifuate utaratibu maalumu, wa kimbinu na mikakati kuelekea mchezo husika. Kama mpira ni sayansi, na unatumia mbinu bila shaka mbinu hizohizo ndizo zitakazo iwezesha timu fulani kupata ushindi.

Simba katika mchezo wake wa kwanza, dhidi ya JS Saoura, nyumbani, kocha Patrick Aussems alianza na kikosi hiki: Aishi Manula, Nicolas Gyan, Mohammed Hussein, Juuko Murshid, Pascal Wawa, James Kotei, Hassan Dilunga, Jonas Mkude, John Bocco, Emmanuel Okwi na Clatus Chama.

Kikosi hiki mbele ya JS Saoura kilikuwa na lengo la kushambulia, kumuanzisha Dilunga na Chama kama viungo washambuliaji (Attacking Midfielders) ni kutaka kuongeza ubunifu na kutengeneza nafasi nyingi za magoli, na kwa hili walifanikiwa kwa kiasi kikubwa japo Dilunga alionekana kuchoka haraka na wakati mwingine kukosa utulivu, hii ikapelekea kutolewa na kuingia Mzamiru Yassin ambaye kiasili ni kiungo wa kati mwenye uwezo mkubwa wa kukaba.

Aussems alimuingiza Mzamiru kwa lengo la kumsaidia kukaba kuanzia juu, na kutowaruhusu Waarabu kumiliki mpira kuanzia golini kwao, hii iliwafanya Waarabu waanze kubutua mipira mbele. Kitendo hicho kiliifaidisha Simba kumiliki mpira muda wote na kuifunga JS Saoura goli 3-0.

Kikosi kilichoanza dhidi ya JS Saoura kilikuwa na lengo la kushambulia ndio maana Dilunga na Chama walianza kwa pamoja, wachezaji wawili wenye sifa zinazofanana wapoanzishwa kwa pamoja maana yake ni kutaka walichonacho yaani ubunifu wa kupiga pasi za mwisho uwe mara mbili zaidi. Aussems alifanikiwa.

Mechi ya pili ni tofauti na mechi ya kwanza, Mnyama alikutana na Vita ambao tayari walikwisha pigwa na Al ahly ya Misri, maana yake waliingia katika mchezo huu wakitaka matokeo zaidi katika uwanja wao wa nyumbani.

Siku moja kabla ya mechi, Aussems alisema maneno haya, namnukuu – “Tunajua wataanza kutushambulia kwa  kasi kama ilivyo mila na desturi za klabu kama Vita katika michezo yake ya nyumbani”

“Kila mechi huwa tunajitahidi kuumiliki mpira na kujaribu kutengeneza nafasi nyingi za magoli, hata hapa tutafanya hivyo, sisi hatukuja kujilinda tumekuja kucheza”.

Kocha wa Simba SC, Patrick Aussems.

Maneno yake aliyathibitisha kwa aina ya kikosi alicho kianzisha, kikosi chenyewe kilikuwa hivi; Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohammed Hussein, Juuko Murshid, Paschal Wawa, James Kotei, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, na Clatus Chama.

Kikosi hiki ni sawa na kile cha kipindi cha pili dhidi ya JS Saoura, ingizo jipya akiwa ni Mzamiru Yassin. Kuanza kwa Mzamiru  kulikuwa na lengo maalumu, nalo ni kusaidia ukabaji eneo la kati, kutibua umiliki wa mpira na mipango ya viungo wa kati wa Vita na kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

Wakati Simba wakianza na kikosi hicho, AS Vita walianza na Nelson Luk golini, mabeki Luzolo Sita, Bangala, Botuli, Shabani, viungo wanne, Munganga (nahodha), Ngoma, Kasegu, na Muzinga, washambuliaji wawili Makusu na Kisinda.

Kwa mechi kama hizi, Aussems hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuwabana Vita kuanzia juu, yaani kuweka viungo watatu wenye uwezo mkubwa wa kukaba, hapa namaanisha Mkude, Kotei na Mzamiru walianza kwa lengo la kumiliki kiungo cha kati, kwa kuwazuia  Munganga, Ngoma, Kasenga na Muzinga kutofurukuta.

Viungo wa Simba wamejikuta wakifeli kutimiza majukumu yao kutokana na sababu tano nilizoziona. Sababu zenyewe ni hizi hapa;

Kwanza, Utimamu wa miili. Physique  ya viungo wa Simba ilionekana kuwa mbovu ukilinganisha na viungo wa Vita. Katika mpira kuna wakati wachezaji hupimana uzito wa misuli yao, mipira ya hamsini kwa hamsini mara nyingi wachezaji wa Simba walikuwa wakizidiwa. Hii ina maana kuwa, hawakuwa na uwezo mkubwa wa kupoka mipira kutoka kwa mpinzani, lakini ni rahisi kwao kupokwa mipira na kushambuliwa kiurahisi. Chama alipokonywa mpira kisha goli likafungwa.

Clatus Chama, ni miongoni mwa Viungo wenye ubunifu mkubwa ndani ya kikosi cha Simba.

Pili, usahihi wa pasi zao. Kuanzia dakika ya 30 Simba ilianza kuonyesha uhai baada ya kuanza kumiliki mpira katika eno la kati. Lakini hata hivyo pasi zao kuelekea golini kwa AS Vita hazikuwa na uharaka mkubwa, huku baadhi ya wachezaji wa Simba wakishindwa kuendana na kasi ya mchezo ndio maana, hata walipojaribu kupiga one- two ziliishia miguuni mwa AS Vita.

Nilimshudia Jonas Mkude akipiga “back-pass” tatu. Hii huenda kwake ilikuwa na maana nyingi, ikiwemo ya kukosa mtu wa kumpasia mbele yake, lakini kwa upande wangu, tena kwa mechi kama ile, hakutakiwa kupiga pasi za nyuma nyingi kama alivyofanya. Kupiga pasi za nyuma ni kukaribisha mashambulizi katika eneo lako, hii ni hatari mno kwa timu iliyokwisha zidiwa.

Tatu, ni kukosekana kwa utulivu. “Game concentration” ilionekana kuwa ndogo sana kwa wachezaji wa kati hasa Clatus Chama na Mzamiru ambao kiukweli walionekana kutokuwa na madhara kabisa. Utulivu ulikosekana kabla ya kupokea pasi, wakati wa kumiliki mpira na wakati wa kutoa pasi, Mzamiru alishindwa kufanya yote hayo akiwa kiwanjani ndio maana mapema tu, akafanyiwa mabadiliko, na kumuingiza Dilunga.

Nilimuona Chama katika sura nyingine ya unyonge, ukilinganisha na nilivyo mzoea. Alikosa kujiamini, utulivu ulikuwa haupo, hakupiga pasi zake za hatari, hakutembea na mpira japo hata hatua tano, alikuwa taratibu sana “slow” akiwa na mpira na hiki kiliwafanya wapinzani kujipanga  na kuwafanyia udhibiti” marking” wachezaji wengine na kumkosesha nafasi ya kupiga pasi. Kiufupi, Mzamiru Yassin na Chama walifeli vibaya katika kulidhibiti eneo la kati.

Nne, “poor marking”. Mpira una njia zake, mchezaji mzuri hasa katika nafasi ya kiungo hasa cha chini lazima awe na ubunifu mkubwa katika kuisoma mikimbio ya wapinzani na kuziba nafasi za kupiga pasi za mwisho kuelekea maeneo hatari.  Jonas Mkude na James Kotei walishindwa kuwalinda mabeki wao ambao walionekana kuzidiwa maarifa na washambuliaji wa Vita.

James Kotei alionekana kwa kiasi chake kidogo kuwa na uwezo wa kuisoma mikimbio ya washuliaji, ndio maana aliokoa goli liliokuwa likizama wavuni, lakini hata hivyo hakuwa na muendelezo. Vivyo hivyo kwa Mkude, Mzamiru na Chama nao walikosa kitu kama hicho. Na hiki si kwa eneo la kati pekee, bali hata mabeki  ndio maana hata goli la kona walilofungwa lilikuwa ni makosa ya “poor marking” kwa wachezaji wa Simba. Beki wa Vita aliruka akiwa peke yake bila hata mtu mmoja kumtia kashikashi.

Tano ni kukosekana kwa maandalizi ya kutosha juu ya “game plan” yenyewe. Kuandaa “ game plan” sio tendo la mara moja, kwa klabu zenye mifumo mizuri ya uendeshaji  huchukua hadi wiki moja. Kabla ya kuandaa “ game plan” kocha lazima aijue timu pinzani kwa vitu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwajua wachezaji wa timu pinzani. Sio lazima awajue wote lakini lazima kocha ajue, ni wachezaji gani ni hatari katika hiyo  timu na wanacheza kwa staili gani.

Kufuatilia takwimu za timu husika. Akili ya kocha lazima iwe na mchoro sahihi wa timu anayoenda kukabiliana nayo. Hiki kitamsaidia kuijenga timu yake jinsi ya kuikabili timu hiyo na kisha kupata matokeo. Lazima aijue mifumo inayotumika na timu pinzani, na katika kila mfumo ni mchezaji gani ndio muhimili wa mfumo huo. Kujua hayo yote kutamfanya aiandae timu yake kukabiliana na mfumo wowote utakaojitokeza mbele yake.

Kuijua mikimbio ya wachezaji wa timu pinzani. Hiki ni kitu muhimu sana kwa kocha kukijua kabla ya kupanga kikosi na majukumu kwa wachezaji wake. Hiki kitamfanya ajue timu pinzani hushambulia kupitia wapi na yeye ampange nani ili kwenda kutibua mipango ya timu pinzani, kwa kitaalamu wanaita “blocking pattern”. “blocking pattern”. Hupatikana baada ya kuijua kiundani mikimbio ya timu pinzani.

Kujua aina ya pasi wanazopiga, yaani mipira yao ya mwisho huidondosha katika eneo gani, na lina uhatari kiasi gani “harsh tendencies” lazima kocha ajue aina ya mashambulio ya wapinzani waliyoyazoea, huwa wanafanya nini wakiwa katika yadi ya 10-20 ya mpinzani. Majibu ya maswali haya ni kuja na mfumo wa kuzuia mipango yao na kusuka mipango ya kupata ushindi.

Hadi hapo, nikikwambia “MPIRA NI SAYANSI” utakuwa umenielewa , yaani lazima kuwe na matumizi ya mbinu baada ya kumsoma mpinzani wako, mpira ni mchezo wa kutega na kutegua  mbinu za mpinzani. Simba walishindwa kuzisoma kwa usahihi mbinu za mpinzani, kutegua na kutega mbinu zao za kupata ushindi.

Miongoni mwa wafungaji wa magoli matano dhidi ya Simba SC katika mchezo wa pili, raundi ya makundi, klabu bingwa Afrika.

Kwa kichapo kile, ukilinganisha na “game plan” ya Aussems ni dhahili kuwa, kocha alishindwa kuwaandaa wachezaji wake katika milengo ya upinzani. Kulikuwa na tofauti kubwa ya utimamu, utulivu, upigaji wa pasi sahihi, marking na nguvu kati ya wachezaji wa Simba na wale wa Vita, hivyo bila kupepesa macho, Simba walistahili kuadhibiwa kama walivyoadhibiwa.

Ni imani yangu kuwa, Aussems ni kocha mzoefu na soka la Afrika, atarekebisha makosa na kuipeleka Simba hatua ya mbele zaidi, si muda wa kukata tamaa kwa kuwa ndio kwanza Simba imecheza michezo miwili kati ya 6 waliyokuwa nayo, bado kuna mechi 4 zikiwemo 2 za nyumbani na 2 za ugenini, Simba inaweza kufanya lolote na likawezekana.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x