Zamani

Goli la dhahabu na kifo kilichoandaliwa kwa Wataliano!

Sambaza....

Gawiza bhanamala! Hiyo ni salamu ya kwetu Usukumani, yaani habari wazee! Naamini mpo salama salmini!

Tukiacha mechi ya klabu bingwa Ulaya 2009 kati ya Chelsea na Barcelona, ambayo haina ubishi Barca ilibebwa. Mechi ya kombe la dunia 2002 kati ya wenyeji Korea Kusini na Italia bado ipo kwenye rekodi ndani ya ubongo wangu kama moja ya mechi zenye maamuzi ya hovyo na upendeleo wa hali ya juu.

Naweza kusema angalau sasa zama zimebadilika kwa kiwango kikubwa, lakini zamani kidogo ukicheza na mwenyeji basi jiandae kupita njia ya mateso ya Golgotha. Wenyeji walikuwa wanabebwa mchana kweupe hadi inaboa! Italia walipita kwenye njia hii na kweli hawakutoboa.

Italia iliyokuwa imebeba matumaini ya kuchukua ubingwa wa dunia 2002, ndoto yao ilizimika ghafla kama mwanga wa kimondo, ilipokutana na Korea Kusini hatua ya mtoano ya 16 bora, walipotolewa kwa kufungwa kwa goli 2-1 baada ya dakika 117 za uonevu kwa goli la dhahabu lililopachikwa na Ahn Jung-Hwan, huku maamuzi yakionekana dhahiri ni ya mchongo.

Tuachane na hayo ya mbeleko kwa mzawa. Huyu bwana Ahn Jung-Hwan wakati huo alikuwa anakipiga kwenye klabu inayoshiriki Serie A ligi kuu ya Italia. Mwenyekiti wa klabu hiyo mwaisa mtu mbad Luciano Gaucci kwa hasira akatangaza kuwa Ahn Jung-Hwan asikanyage tena Perugia na mkataba wake ukavunjwa tangu hapo.

Nipo tofauti na Gaucci, binafsi niliitazama ile mechi na simlaumu Jung-Hwan hata kidogo, bali maamuzi mabovu ya Byron Moreno mwamuzi kutoka Ecuardo ndio yaliyozamisha jahazi la Italia.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.