La Liga

Griezmann kuondoka Atletico Madrid.

Sambaza....

Klabu ya soka ya Atletico Madrid kupitia katika kurasa zake za mitandao ya kijamii imethibitisha kwamba mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa Antoine Griezmann hatokuwa na timu hiyo kwa msimu ujao licha ya kwamba mkataba wake unaisha mwaka 2023.

Atletico Madrid imesema kwamba mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 tayari ameshazungumza na viongozi wa juu wa klabu na kwamba tayari klabu inafahamu kuwa mchezaji huyo ambaye thamani yake ni €120 million ataondoka klabuni hapo.

“Antoine Griezmann ameiambia klabu kuwa hatokuwa sehemu ya Rojiblanco kwa msimu ujao,” wameandika kwenye ukurasa wao wa Twitter.

Baada ya muda kidogo Antoine naye akaweka video kwenye ukurasa wake akisema “Baada ya kuzungumza na Cholo (Kocha Diego Simeone), na baadae na Miguel Angel na watu wa juu wa klabu, sasa nataka kuzungumza na nyinyi mashabiki ambao kwa wakati wote mmenipa upendo wa hali ya juu,”

“Nataka kuwaambia wote kwamba nimechukua maamuzi ya kuondoka kwenye klabu, nimekuwa na misimu mitano mizuri sana hapa na mara zote mtakuwa ndani ya moyo wangu, kiukweli ilikuwa ngumu kuchukua maamuzi haya lakini nilihisi napaswa kuchukua, ningependa kuwashukuru wote kwa upendo wenu kwa muda wote wa miaka hii mitano,” Griezmann amesema.

Griezmann ameichezea Atletico Madrid michezo 252 na kuifungia mabao 133, akiisaidia klabu hiyo kucheza fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya mwaka 2016 walipofungwa na Real Madrid na mwaka 2018 walitwaa taji la Uropa kwa kuwachapa Marseille kwenye fainali.

Mshambuliaji huyo ambaye anatajwa kujiunga na Barcelona ya Uhispania alitwaa kombe la dunia mwaka 2018 akiwa na Ufaransa lakini pia aliiwezesha nchi yake kucheza fainali ya Mataifa Ulaya dhidi ya Ureno jambo lililomfanya kumaliza nafasi ya tatu kwenye tuzo za Ballon d’Or kwa mwaka 2016.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.