Sambaza....

Kelele tulizipiga sana, tuliandika sana, watu wakaongea sana kwenye redio kama ni wimbo ungekuwa wimbo unaohusu kuhamasisha wakazi wa Kariakoo wamiliki viwanja vyao binafsi. Viwanja ambavyo vingewawezesha watu wa Kariakoo waondokane na adha ya kuomba omba kila wakati.

Ni aibu kubwa sana vilabu kama Simba na Yanga vyenye umri mkubwa kuwa vinaomba omba viwanja na wakati mwingine kunyimwa na wamiliki. Miaka yao ni mingi mno, umri wa mtu mzima ambaye angefaa kuwa na maendeleo makubwa sana, maendeleo ambayo yangemfanya aishi kwa amani na furaha kwenye umri huu alionao.

Azam Complex, Uwanja wa Azam Fc

Lakini imekuwa tofauti sana kwao, hakuna maendeleo makubwa ndani ya hivi vilabu vya Simba na Yanga ingawa vina umri mkubwa sana.

Inasikitisha na kuuma pale unapogundua hata viwanja vya mazoezi havijawahi kujengwa na vilabu hivi. Wamekuwa wakipoteza pesa nyingi sana kukodi viwanja vya mazoezi kila uchwao.

Tuliimba sana huu wimbo wa kuhamasisha, wimbo wetu ukaonekana kama umewaingia viongozi wa Simba na Yanga, habari mpya zikaanza kupenyeza kwenye ngoma za masikio yetu.

Habari ya Bunju ilikuja kwa kasi sana, tukaoneshwa shamba ambalo Simba walinunua kwa ajili ya kujenga Bunju Arena, wanachama wakafurahia hiyo habari

Wakahamasika vya kutosha hata baada ya wao kutakiwa na viongozi kubeba panga ili wakafyeke shamba la Bunju walienda , hii yote ilikuwa kujitolea kwa ajili ya timu yao.

Hii yote ilikuwa kwa ajili ya kukwepa masimango mengi ya wao kutokuwa na uwanja, kiu yao kubwa ilikuwa kuona timu yao ikiwa na uwanja wake ambao utakuwa unawafanya wawe huru kuutumia.

Viongozi wa Simba walipotembelea Bunju

Hata baada ya kuombwa kuchangia mifuko ya simenti, hawakusita kutoa hata mfuko mmoja wa simenti. Nafsi zao zilihamasika sana kichwani mwao walikuwa na ramani ya Bunju Arena.

Ramani ambayo ilikuwa inaonesha jinsi ambavyo uwanja wao utakuwa mzuri tena wa kisasa, nyasi za bandia ziliagizwa ndipo hapo moto ukazidi kuwa mkali kwenye mioyo ya watu.

Kila mtu alihamasika sana, ilionesha wengi walikuwa tayari kutoa hata mia moja kwa ajili ya kuisaidia klabu imiliki uwanja wao.

Lakini mwisho wa siku ukali wa moto umeanza kupungua, miaka mingi imepita tangu watu wafyeke nyasi kule Bunju lakini hakuna hata tofali moja lililosimama kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa Bunju Arena.

Hata zile simenti zilizotolewa kuna hatari kubwa zimeishia muda wake wa matumizi, vitu vingi vimebadirika na vinaenda kwenye kasi ndogo tofauti na kasi ya mwanzo.

Ndiyo maana niliposikia kasi waliyoanza nayo Yanga kule Gezaulole nilitamani kuupa nafasi kwanza muda.

Niliamini muda una majibu yote muhimu kuhusu na hicho kitu, jiwe la msingi liliwekwa kwa ajili ya ujenzi wa uwanja na hostel ambao ulitakiwa kuanza mara moja.

Na huu ujenzi ulikuwa nje ya makubaliano ya kukodisha timu, lakini tangu Yanga wapewe eneo hilo hakuna kitu kikubwa walichokifanya.

Viongozi wa Yanga wakiwa katika eneo walilopewa na Manji, ambalo sasa ni eneo la serikali.

Sarakasi hizi za Bunju na Gezaulole zinatosha kuonesha kuwa tunapenda sana kuanza kwa moto tena maneno mengi yakiwa yametujaa midomo mwetu.

Midomo yetu hushindwa kuiamrisha miguu kupiga hatua za kusonga mbele, ndiyo maana ni ngumu sisi kuwahi maendeleo makubwa kama wenzetu.

Kuna haja ya sisi kuacha kuongea sana na kukaa kwenye meza za kibiashara na kuziendesha vilabu vyetu kibiashara.

Bunju Arena ingejengwa na shirika la nyumba la Taifa kwa makubaliano ya kibiashara kama ya kuuita uwanja ule kwa jina la shirika la nyumba ya Taifa kwa muda wa miaka ambayo itatumika kulitangaza jina la shirika la nyumba la Taifa kupitia nembo ya Simba.

Hakuna biashara iliyofikia sehemu kubwa inayofanywa na mtu mmoja, biashara zote hufanywa kwa ushirikiano wa wafanyabiashara wenye maono ya kufikia biashara kubwa duniani

Sambaza....