Sambaza....

Klabu ya soka ya Alliance School ya jijini Mwanza imetoa taarifa ya usajili walioufanya katika dirisha dogo la usajili ambalo limefungwa usiku wa kuamkia leo.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Afisa Habari Jackson Luka Mwafulango, imeonesha kuwa Alliance imewasajili wachezaji watano akiwemo mshambuliaji wa kutegemewa wa Stand United ya Shinyanga Mrundi Bigirimana Blaise na Hussein Javu wa Mtibwa Sugar ambaye aliwahi kupita Yanga SC.

Aidha wachezaji wengine ambao wameongezwa kwenye kikosi cha Alliance ni pamoja na Adam Ibrahim Abdallah kutoka Ruvu Shooting ya Pwani, mlinda mlango John Mwenda Chacha na Paulo Maono wa Biashara United ya mkoani Mara.

“Tumefanya usajili huu kwa kuzingatia maoni ya mwalimu Malale Hamsini, lengo letu ni kuona tunatoka katika sehemu ambayo tupo na kupanda zaidi, hili litafikiwa kama wachezaji wote wale ambao tumewasajili na waliopo kuonesha moyo wa kujituma na kujua thamani ya klabu yao,” Mwafulango amesema.

Aidha katika taarifa hiyo, Alliance FC wamethibitisha kuwaachia wachezaji David Richard Uromy, Salim Juma Sheshe na Issa Backy ambao wote wametolewa kwa mkopo kuelekea klabu ya Pamba FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza huku Said Lubawa akiachiwa kabisa kuelekea Singida United sawa na Kelvin Faru akielekea Namungo FC ya mkoani Lindi.

Sambaza....