Sambaza....

Mshambuliaji wa timu ya Kandanda ya Mbeya City Idd Suleiman amesema kuongoza mabao Mawili Dhidi ya Mbao FC na baadae kutoka sare ilikuwa ni sehemu ya mchezo na kwamba hakuna wa kulaumiwa kwenye timu yao.

Idd ambaye alifunga bao la Kwanza katika mchezo huo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba amesema makosa madogo waliyoyafanya katika Dakika za mwisho ndiyo yaliyowagharimu kupoteza alama mbili ugenini.

“Hatukuzidiwa, huu mpira ni mchezo wa makosa tulipata goli mbili kipindi cha Kwanza na wao wakapata goli mbili kipindi cha pili, mwalimu kaona makosa tunajipanga kuelekea katika mchezo ujao dhidi ya KMC,” Idd amesema.

Suleiman amesema japokuwa wameshindwa kupata matokeo ya ushindi lakini ni bora zaidi kuliko kupoteza mchezo huo kwani umewaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.

Mbeya City wamesafiri kuelekea Jijini Dar es Salaam ambapo Jumanne ijayo watacheza na timu ya manispaa ya Kinondoni KMC.

Kwa sasa Mbeya City wamefikisha alama 18 Baada ya michezo 12, wakiwa katika nafasi ya sita yenye timu 20.

Sambaza....