Blog

Insta ya Cristiano Ronaldo imenifanya nimkumbuke Ngassa na Kaseja.

Sambaza....

“Kiyumbi nenda Instagram kuna Email nimekutumia”, huu ndiyo ujumbe wa simu wa kwanza kuusoma leo hii kwenye simu yangu kutoka kwa rafiki yangu mkubwa sana.

Sekunde sikuziruhusu zipite nyingi, vidole vyangu vilijongea taratibu mpaka Instagram, mtandao ambao umekuja kuzima zama za Facebook.

Watu maarufu ni nadra kuwaona wakitumia kwa ukubwa Facebook, Instagram imekuwa sehemu sahihi kwao wao kukutana na mashabiki wao.

Wachezaji wa Mpira wa Miguu wenye ‘Followers’ wengi katika Instagram

Account ya kwanza kukutana nayo baada ya kuingia Instagram ni account ya Cristiano Ronaldo.

Mchezaji ambaye ameweka rekodi nyingi sana katika ulimwengu wa kandanda, mchezaji aliyedumu kwa muda mrefu kwenye kiwango chako kwa miaka 10 mfululizo bila kushuka.

Ndiyo maana ikawa rahisi kwake kufunga hat tricks 50 katika maisha yake ya mpira, hata niliposikia kafunga hat tricks 7 katika michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya sikushangaa kabisa.

Hata aliyewahi kuniambia kuwa Cristiano Ronaldo ndiye mfungaji bora wa wakati wote wa michuano ya klabu bingwa barani ulaya sikuona kama ni jambo la ajabu.

Rekodi ya Wasukuma Kandanda wenye followers wengi Insta 25/10/2017

Hakuna uajabu kwenye kujituma, jitihada zake ndizo zimemfanya kuwa ndiye mchezaji pekee mwenye magoli mengi katika timu ya Taifa kati ya wachezaji wanaocheza kwa sasa.

Hii ilinipa taswira kuwa mchezaji huyu kakamilika ipasavyo na haikuwa bahati mbaya kwake yeye kuchukua Ballon D’or tano.

Maisha yalimpa alichokuwa anakitafuta kwa muda mrefu, ndiyo maana akapata mafanikio makubwa sana , mafanikio ambayo yalikuja na ukubwa wa jina lake.

Jina ambalo lilibeba mashabiki wengi duniani, mashabiki ambao anawatumia ipasavyo ili kujipatia pesa. Nilisikia amefungua hotel kubwa sana kwao Ureno.

Inawezekana hotel ikawa ni jambo kubwa sana na likawa jambo ambalo ni gumu kwa watu wenye uchumi mdogo, lakini nilipoiona account ya Cristiano Ronaldo leo asubuhi niliona namna ambavyo anatumia jina lake kuwafikia watu wengi kwa bidhaa zake.

Bidhaa ambazo zina nembo ya jina lake, jina ambalo alilitengeneza wakati anacheza mpira. Leo hii anaona maisha yake ndani ya uwanja yanakaribia kufika pumzi ya mwisho.

Hatokuwa na uwezo wa kufunga tena hat tricks kwenye michuano ya klabu bingwa barani ulaya. Hatokuwa na kasi kubwa tena ya kushambulia kwa kasi na hata ule uwezo wake wa kufunga magoli kwa mashuti utapungua na kuisha kabisa kwa siku za hivi karibuni.

Sehemu ya pili ya kufunga kwa mashuti, kukimbia na mipira kwa kasi na kufunga hattricks ni hii anayoifanya sasa hivi, kutumia jina lake kuleta bidhaa kwa mashabiki wake.

Nguo za ndani za kiume ndizo nguo za kwanza kuziona kwenye account ya instagram ya Cristiano Ronaldo.

Double trouble ?@cr7underwear

A post shared by Cristiano Ronaldo (@cristiano) on

Nguo ambazo watu wengi wataweza kumudu kuzinunua , hapa ndipo ataanza kupiga hattricks za pesa baada ya kuachana na maisha ya soka.

Nilikaa dakika kumi naangalia picha ile aliyopost Cristiano Ronaldo akiwa kifua wazi na akiwa amevaa nguo ya ndani tu yenye nembo ya CR7.

Maswali mengi yalikuwa yanakuja kichwani mwangu, moja ya swali lilikuja na picha ya Mrisho Ngassa.

Yuko wapi Mrisho Ngassa?, hili ndilo swali la kwanza, kabla ya jibu halijapatikana kichwani mwangu swali jingine lilikuja, yuko wapi Juma Kaseja?

Kipa namba moja wa Tanzania pamoja na mfungaji bora wa timu ya taifa wa muda wote baada ya Sunday Manara.

Wachezaji ambao walijenga jina kubwa kupitia umahiri wao uwanjani. Wakati Kaseja akiwa mahiri kwenye kuchomoa michomo mikali, Ngassa alikuwa mahiri kufunga kwa michomo mikali.

Juma Kaseja

Mashabiki wengi walifurahia kuwaona hawa , ilikuwa furaha kwa mashabiki kuwaona wakiwa katika uzi wa timu yao ndiyo maana walicheza timu zenye uhasimu mkubwa hapa nchini (Simba na Yanga)

Leo hii wapo Ndanda na Kagera Sugar muda siyo mrefu wataitwa wastaafu wenye jina kubwa na heshima kubwa.

Jina ambalo lilinifanya nione MN17 pale kwenye nguo ya ndani ya Cristiano Ronaldo, nembo ambayo Mrisho Ngassa angeitumia nje ya uwanja kutengeneza pesa.

Niliona nembo ya Juma Kaseja (JKone) kwenye zile nguo za ndani. Tofauti ya wenzetu na sisi ni kichwani tu.

Hakuna jambo gumu kwenye uwekezaji wa akili. Akili ukiwekeza vizuri urahisi hupatikana.

Mrisho Ngassa

Juma Kaseja na Mrisho Ngassa wanatakiwa kufikiria kuwa na wasimamizi ambao watalisimamia jina lao walilotengeneza uwanjani ili liwalipe kibiashara nje ya uwanja.

Wachezaji wengi hunufaika katika (endorsement) hakuna aliyefanikiwa katika biashara ya peke yake. Biashara nyingi zimefanikiwa kwa ushirikiano wa pamoja.

Ushirikiano huu unapatikana kwa mchezaji kuwa na wasimamizi wenye maono makubwa, maono ambayo yatasababisha walitumie jina la mchezaji kibiashara.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x