Kagere
Ligi Kuu

Kagere yuko kama hayuko

Sambaza....

MFUNGAJI wetu bora wa ligi msimu uliopita Meddie Kagere anapitia kipindi kigumu kwa sasa. Hafungi tena kila wiki. Msimu uliopita kila wiki alikuwa anafunga. Alikuwa moto kweli kweli.

Msimu huu yuko hovyo kiasi, makali yake yamepungua, lakini kuna sababu tatu zinazofanya tumuone Kagere wa namna hii. Twende pole pole huko chini nitakuelezea sababu zenyewe.

Licha ya namba za ufungaji kumkataa Kagere, lakini ndiyo kinara wa ufungaji msimu huu. Hapa kunashangaza. Kuna maswali tunatakiwa kujibiwa na washambuliaji wa timu nyingine. Wasitupuuze.

Inakuwaje Kagere aonekane kushuka kiwango cha ufungaji, lakini bado anawaongoza wafungaji wengine? Ana mabao 11. Naomba nirudie swali. Inakuwaje Kagere aonekane kushuka kiwango cha ufungaji, lakini bado anaongoza wafungaji?


Na.MchezajiTimuNafasi
1rwaMeddie KagereMshambuliaji22
2tanWaziri JuniorMshambuliaji13
3tanPeter MapundaKiungo12

Washambuliaji watujibu swali hili. Mada hii nitarudi nayo siku nyingine. Turudi katika zile sababu tatu. Mosi Kagere anakamiwa. Ni kweli anakamiwa, lakini hili halipaswi kumfanya apungue makali yake. Duniani kote wachezaji nyota hukutana na wakati mgumu kiwanjani, lakini haiwafanyi waonekane wawe hovyo.

Wachezaji nyota ulimwenguni wanakutana na hali hii, lakini wakija kiwanjani wanatuonyesha wao ni wachezaji wa namna ipi. Kagere atuonyeshe.

Meddie akiwa katika mazoezi

Ajitazame upya. Ni wakati wa kujitathimini (Self – assessment). Inakuwaje msimu uliopita awe mwiba mchungu, leo hii asue sue? Arudi uwanja wa mazoezi. Asitegemee tena mazoezi ya timu.

Sababu ya pili kukosekana kwa Emmanuel Okwi na muda mwingi John Bocco kuwa na majeraha ni moja ya sababu inayofanya tumuone Kagere wa namna hii. Msimu uliopita safu ya ushambuliaji muda mrefu iliundwa na yeye Okwi na Bocco, watatu hawa walicheza asilimia 98 ya mechi za Simba na kufanya vyema.

Lakini msimu huu muda mrefu Kagere amecheza peke yake. Okwi hayuko tena kikosini, Bocco alikuwa na majeraha amepona, lakini bado hajawa vizuri kwa asilimia 100. Anguko la Kagere linatokana na mambo mengi, ana matatizo yake binafsi na ana matatizo mengine yaliyomzunguka.

Kama Okwi, Bocco wangekuwepo kikosini, kisha Kagere akawa na kiwango hiki tungetafuta sababu nyingine, lakini kukosekana kwao na Kagere kuwa na kiwango hiki, ni moja ya sababu ambayo hata Kagere mwenyewe anaweza kuitumia kujitetea juu ya kiwango chake.

Sababu ya mwisho ni uchovu. Hili la uchovu huwa linawakuta wachezaji wengi. Inawezekana Kagere anamalizwa na hili. Njia ya kuutibu ugonjwa huu ni mchezaji kupewa mapumziko na timu yake.

Simba watakubali Kagere akae nje michezo kadhaa ili kurudisha mwili katika hali yake? Ni swala gumu ambalo Simba hawatataka kulisikia.

Mwisho kabisa Simba wamvumilie Kagere. Lakini wajue wazi wakiendelea nae hivi wanammaliza na watajiaminisha kuwa hana jipya amechoka na watamuacha. Mchezaji anapata muda wa kupumzika katika timu nyingine anaibuka tena na kuwa staa. Hii imewahi kutokea mara nyingi.

Sambaza....